Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-30 16:46:24    
Watu wa vizazi vitatu na maendeleo ya uhakikisho kutoka serikalini nchini China

cri

Nchini China, uhakikisho kutoka serikalini ni suala linalofuatiliwa na watu wa hali mbalimbali katika miaka ya karibuni. Hivi majuzi mwandishi wetu wa habari alitembelea familia moja hapa mjini Beijing, ambapo watu wa vizazi vitatu wa famila hiyo walielezea mitizamo yao kuhusu pesa za kujikimu kutoka serikalini.

Familia hiyo inaitwa Li. Mzee Li Jiaji amestaafu miaka karibu 22 iliyopita. Hivi sasa kila asubuhi anakwenda kwenye busatani kufanya mazoezi ya kujenga mwili, na kukutana na marafiki zake, ambao pia ni wazee waliostaafu. Siku nyingine pia wanabadilishana maoni kuhusu malipo ya kiinua mgongo. Mzee Li alisema, (sauti 1) "Nilipostaafu pensheni ilikuwa Yuan 75 tu kwa mwezi, ambayo ilikuwa inaendelea kuongezeka katika miaka iliyopita na kuzidi Yuan elfu moja kwa hivi sasa. Inatosha, lakini itakuwa vizuri zaidi ikiongezeka."

Mzee Li alikuwa anafanya kazi ya useremala kiwandani kwa kipindi cha miaka 31 tangu mwaka 1953 mpaka mwaka 1984 alipostaafu.

Ingawa sasa kiwango cha pensheni kimeinuka sana, lakini bado kinalingana na kiwango cha pesa za uhakikisho wa maisha ya kimsingi kilichowekwa na serikali ya mji wa Beijing.

Serikali ya China ilitangaza utaratibu wa bima za kazi mwaka 1951, ambapo waraka huo wa kisheria ulihusu sheria ya huduma za jamii. Kuanzia hapo, China ilijenga utaratibu wa bima za kazi kuhusu uzeeni, afya, ajali kazini na uzazi, isipokuwa bima ya kutokuwa na ajira. Na viwanda vilikuwa ni chanzo kikuu cha fedha za kuhakikisha huduma hizo.

Hadi kufikia miaka ya 90 ya karne iliyopita, kutokana na mageuzi ya kiuchumi, ilionekana kuwa haifai kwa viwanda kubeba majukumu yote ya kijamii katika uchumi wa soko huria. Kwa hiyo kwa mujibu wa utaratibu mpya uliotolewa na serikali ya China mwaka 1997, fedha za huduma za jamii zinachangiwa na pande tatu za viwanda, serikali na watu binafsi, kwa hiyo wafanyakazi wenyewe pia wanapaswa kuweka akiba kwenye akaunti binafsi kabla ya kustaafu.

Katika hali hii, mzee Li ambaye alishastaafu miaka mingi iliyopita anapewa pensheni ndogo kwa kukosa mchango kutoka kwenye akaunti yake binafsi.

Profesa Li Shaoguang wa Chuo kikuu cha umma cha China alifafanua kuwa, (sauti 2) "Kwa watu waliostaafu kabla ya mwaka 1997, pensheni wanayopata ni ya kiwango cha chini, kwani walipofanya kazi viwanda vilikuwa vinabeba jukumu la kuwawekea pesa kwenye bima ya malipo ya uzeeni, na wafanyakazi wenyewe hawakutakiwa kuweka pesa. Sababu nyingine inayowafanya wawe na kiwango kidogo cha pensheni ni hali duni ya wastani wa mishahara walipokuwa kazini."

Mtoto wa mzee, Bw. Li Junpeng ni miongoni mwa wanaonufaika na utaratibu huo mpya. Alistaafu miaka miwili iliyopita kutoka kwenye kampuni moja inayomilikiwa na taifa.

(sauti 3) "Mwaka jana kiwango cha pensheni kilirekebishwa kwa mara nyingine tena, sasa napewa Yuan elfu 2. Kiasi hiki si kikubwa wala si kidogo, lakini ni kizuri zaidi kuliko kile cha wazee wa kizazi cha baba yangu."

Bw. Li anaonekana kuridhika na pensheni yake. Kwa mujibu wa utaratibu mpya wa mwaka 1997, hatua tofauti zinachukuliwa kwa watu waliostaafu kabla ya mageuzi ya kiuchumi, walioanza kazi kabla yake na baada yake.

Profesa Li Shaoguang alichambua akisema, (sauti 4) "Kwa watu walioanza kazi kabla ya mageuzi ya kiuchumi, pia kuna kipindi ambacho wafanyakazi wenyewe hawakuhitajika kuweka fedha kwenye akaunti binafsi za bima ya malipo ya uzeeni. Kwa hiyo serikali inatoa ruzuku za kiasi fulani kwa watu waliostaafu kabla ya mageuzi ya kiuchumi na walioanza kazi kabla ya mageuzi. Aidha, kutokana na wastani wa mishahara kuendelea kuongezeka, hakika Bw. Li mdogo ana pensheni kubwa zaidi kuliko ile ya baba yake."

Katika familia ya Li, mtu anayepuuza umuhimu wa pensheni na bima ya tiba ni Li Xiaopeng, kijana mwenye umri wa miaka 28, ambaye ni mjukuu wa mzee Li. Baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu, alipata ajira katika kampuni inayowekezwa vitega uchumi vya nje. Tokea siku alipotia saini mkataba wa ajira, kampuni yake inamlipia pesa za bima ya malipo ya uzeeni, bima ya tiba na bima ya kukosa ajira. Hata hivyo, akifananishwa na vijana wengine ambao ni kizazi kinacholindwa na bima hizo tatu, kijana Li hatilii maanani manufaa hayo ingawa babu yake anamkosoa kwa kutothamini neema aliyo nayo.

Katika familia hiyo, wazee wanazingatia uhakikisho wa maisha, ambapo kijana anafurahia kukopa kwa ajili ya kununua gari. Kijana Li Xiaopeng alijitetea, akisema (sauti 5) "Hivi sasa ukifanya kazi katika kampuni zinazotumia vitega uchumi vya nje na kampuni za watu binafsi, unalindwa na bima hizo tatu. Na kampuni zote halali zinabidi kuwalipia wafanyakazi bima hizo tatu. Lakini hakuna kijana atakayetegemea bima hizo katika siku za kustaafu, kwani hivi sasa tunachuma pesa nyingi zaidi, na zitatosheleza mahitaji ya siku zijazo."

Profesa Li Shaoguang alieleza kuwa, kutokana na kukamilika kwa akaunti binafsi na kuwepo fedha za kujikimu zinazotengwa na serikali, suala la pensheni halizungumziwi mara kwa mara na watu wa kizazi cha Li Xiaopeng.

Tangu mwaka 2005, imetokea wito na mapendekezo ya kuwashirikisha wakulima kwenye mfumo wa bima za jamii.