Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-03 14:51:55    
Shamrashamra za kila aina katika Tamasha la Utamaduni wa Russia

cri

Tarehe 21Machi marais wa China na Russia walihudhuria ufunguzi wa "Mwaka wa Russia" nchini China. Katika kipindi hicho cha "Mwaka wa Russia", shughuli nyingi za maingiliano kati ya China na Russia zinafanyika, na miongoni mwa shughuli hizo, tamasha la utamaduni wa Russia lilipamba moto na kuwaonesha Wachina utamaduni mkubwa wa Russia.

Mliosikia ni muziki "Lele ya Sikukuu" uliotungwa na mwamuziki mashuhuri wa Russia Bw. Shostakovitch, na ulipigwa na Kundi la Simfoni la Jumba la Opera la Russia. Jioni tarehe 22 kwenye ufunguzi wa Tamasha la Utamaduni wa Russia uliofanyika katika ukumbi mkubwa wa umma mjini Beijing wasanii wa Jumba la Opera la Russia walionesha michezo yao ambayo ilishangiliwa sana na watizamaji elfu kadhaa katika ukumbi huo.

Jumba la Opera ya Russia limekuwa na miaka 230, kundi la wasanii katika jumba hilo linajulikana kwa kuonesha michezo ya Kirussia. Kwa ajili ya tamasha hilo jumba hilo limetuma wasanii 280 wakiwa katika kundi la simfoni, opera, balet na kwaya. Michezo waliyoonesha katika ukumbi huo iliwafanya watazamaji wajisahau kwa furaha.

Tamasha la Utamaduni wa Russia ni moja ya shughuli za Mwaka wa Russia nchini China, ambao umeanzia tokea tarehe 22 Machi mwaka huu hadi mwezi Januari mwaka kesho. Msaidizi wa waziri wa utamaduni wa China Bw. Ding Wei alileza,

"Russia ni nchi kubwa ya kisanaa, athari yake ni kubwa kwa China na hata dunia nzima. Aina za sanaa zinazooneshwa na wasanii wa Russia nchini China ni nyingi zikiwa ni pamoja na dansi ya balet, muziki wa simfoni, nyimbo na ngoma, opera, muziki wa kisasa na tamthilia, ili kuonesha usanii wa Russia kwa pande zote."

Katika siku za tamasha hilo, picha za mafuta za Russia pia zinaoneshwa katika Jumba la Sanaa la Beijing. Uchoraji wa picha za mafuta nchini Russia umekuwa na historia ya miaka 300. Picha 110 zinazooneshwa zinawakilisha historia ya maendeleo ya uchoraji wa picha za mafuta tokea karne ya 18 hadi ya 21. Siku hizi watazamaji wanamiminika na wanavutiwa bila kutaka kuondoka mbele ya picha. Baadhi ya watazamaji walitulia mbele ya picha moja ya watoto wawili waliolala usingizi mnono kwenye lundo la nyasi kavu, jinsi walivyo inawasisimua na kuwavutia sana watazamaji. Mtazamaji Bi. Fu Aiyun alisema kwa msisimko,

"Picha za mafuta za Russia ni maarufu sana duniani, picha za hapa zinanigusa hisia zangu. Ni fahari kubwa kuweza kuona picha hizo zilizochorwa na wachoraji wakubwa katika karne kadhaa zilizopita, kama usingekuwepo Mwaka wa Rusia nisingeweza kuziona."

Licha ya picha hizo zilizokuwepo kwa karne kadhaa pia kuna maonesho ya sanaa ya Rusia ya leo katika jumba hilo la sanaa la Beijing. Kutokana na picha na sanamu zinazooneshwa, watazamaji wanaweza kufahamu utatanishi wa fikra za wasanii kuhusu mabadiliko ya kihistoria na mitindo mipya ya uchoraji wao. Mkuu wa Jumba la Sanaa la Beijing Bw. Fan Di'an alisema,

"Kwa muda mrefu wachoraji wa China wanaheshimu na wamejifunza mengi kutoka picha zilizochorwa tokea karne ya 18, na kutoka picha 110 zinazooneshwa tumeona nyayo za miaka 300 ya uchoraji wa picha za mafuta nchini Russia. Na pia tunafurahia maonesho ya sanaa ya Russia iliyo Wazi ambayo yametuonesha sanaa za wasanii wazee na vijana wa leo. Maonesho hayo mawili ya picha za zamani na za kisasa yametosheleza mahitaji ya watazamaji wa China ya kuona sanaa za aina tofauti za Russia."

Imefahamika kwamba licha ya maonesho hayo mawili, pia kuna maonesho ya "johari ndani ya kasri la Kremlin mjini Moscow".

Mwaka huu, mbali na maonesho ya aina mbalimbali yanayoandaliwa na serikali ya Russia pia kuna maingiliano mengi ya kiraia kati ya China na Russia. Tarehe 13 Machi, "Tamasha la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya China na Russia" lilifanyika katika Chuo Kikuu cha Beijing. Wanafunzi zaidi ya 50 kutoka vyuo vikuu vya Moscow na St. Petersburg na wanafunzi wa China kutoka vyuo vikuu mbalimbali mjini Beijing walihudhuria tamasha hilo.

Wasikilizaji wapendwa, mliosikia ni wimbo ulioimbwa na wanafunzi wa Russia katika tamasha hilo. Ingawa lugha ni tofauti lakini sanaa inaeleweka kwa wote, wanafunzi wa nchi mbili China na Russia mara kwa mara wanashangilia michezo kwa makofi. Mwanafunzi anayetoka Chuo Kikuu cha St. Petersburg msichana Anna alisema,

"Tamasha hilo ni muhimu sana kwa ajili ya kuzidisha maelewano kati ya vijana wa nchi mbili na hasa kwa vijana wa Russia kuifahamu China, kwa sababu miongoni mwetu wengi ni mara ya kwanza kuja China."

Idhaa ya kiswahili 2006-04-03