Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-05 20:01:42    
Jumuiya ya kimataifa yaimarisha ushirikiano ili kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia

cri

Mkutano wa elimu na mafunzo na malengo ya maendeleo ya milenia ya Umoja wa Mataifa ulifunguliwa hivi karibuni mjini Beijing. Wajumbe zaidi ya 100 kutoka Shirikisho la kimataifa la baraza la uchumi na jamii na mashirika yanayofanana (IAESCSI) na baraza la uchumi na jamii la Umoja wa Mataifa walijadili masuala kadhaa yakiwemo kupugnuza kwa umasikini na elimu. Watu waliohudhuria mkutano huo walitoa mwito wakisema kuwa, ni lazima jumuiya ya kimataifa iimarishe ushirikiano ili kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia, yakiwemo kupunguza kwa umaskini na kueneza elimu ya msingi katika miaka 10 ijayo.

Malengo manane yaliyoamuliwa na wakuu wa nchi mbalimbali mwaka 2000 kuhusu kupunguza nusu ya idadi ya watu maskini kabisa duniani na kueneza elimu ya msingi duniani ifikapo mwaka 2015. Takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, hivi sasa bado kuna watu maskini kabisa zaidi ya bilioni 1 duniani, ambao wanatumia chini ya dola moja ya Kimarekani kwa siku, na watoto zaidi ya milioni 100 hawawezi kupata elimu kutokana na umaskini, tatizo hilo ni kubwa zaidi katika sehemu zilizoko kusini mwa Sahara barani Afrika.

Kwenye mkutano huo, naibu mwenyekiti wa baraza la uchumi na jamii la Benin Bw. Tabe Gbian alisema, kuwapatia watu maskini elimu ni changamoto kubwa kwa nchi nyingi barani Afrika.

"Kiwango cha elimu katika bara la Afrika ni cha chini kuliko mabara mengine. Tunakabiliwa na tatizo la ukosefu wa fedha kwa ajili ya maendeleo ya elimu. Tunahitaji kutatua tatizo hilo haraka, kwani elimu ni msingi wa maendeleo ya mambo yote. Malengo ya maendeleo ya milenia ni muhimu sana katika kutatua tatizo hilo."

Mkuu wa ofisi ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya baraza la uchumi na jamii la Umoja wa Mataifa Bibi. Hanifa Mezoui alisema, katika nchi na sehemu zilizo nyuma kabisa kiuchumi duniani, kuendeleza elimu na mafunzo ni muhimu ili kuondoa mzunguko mbaya wa umaskini na ukosefu wa elimu. Kama jumuiya ya kimataifa haitachukua hatua mwafaka, utimizaji wa malengo ya maendeleo ya milenia utakwama.

Takwimu zilizosanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali barani Afrika, Asia, Latin Amerika na Ulaya ya Mashariki zinaonesha kuwa, kutokana na ukosefu wa mafunzo na elimu, uwezo wa watu kujipatia maendeleo umepungua, na hali hiyo imehatarisha juhudi za kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia.

Ofisa wa Mfuko wa Elimu ya Wanawake Wote wa India anayehudhuria mkutano huo Bw. Mohammad Riaz Umar pia anaona kuwa, umasikini unasababisha ukosefu wa elimu, na ukosefu wa elimu unasababisha umaskini, hivyo ni muhimu sana kuendeleza elimu.

Elimu ina uhusiano wa karibu na maendeleo ya uchumi, hatuwezi kuyatenga mambo hayo mawili. Kama watu wanaweza kupata elimu katika ngazi mbalimbali, basi watu hao, hasa wanawake, watapata fursa nyingi za ajira. Ama sivyo kiwango cha maisha yao kitakuwa cha chini.

Watu waliohudhuria mkutano huo pia waliona, mambo ya elimu na maendeleo ya uchumi yanaweza kuhimizana. Katika miaka mitano iliyopita, nchi zaidi ya 30 za Asia zikiwemo China na India zilipata maendeleo katika sekta za uchumi na jamii, idadi ya watu maskini na watu wanaokosa fursa ya kwenda shule imepungua.

Habari kutoka idara za elimu za China zinasema, serikali ya China imetoa kipaumbele kwa maendeleo ya elimu, na kutenga fedha nyingi kwa elimu ya vijijini na ya wananchi wa kawaida. Hivi sasa idadi ya watu wanaopata elimu ya lazima imefikia asilimia 94 ya watu wote, na kiwango cha maendeleo ya elimu kinakaribia kiwango cha wastani cha nchi zilizoendelea kwenye kiwango cha katikatika. Licha ya hayo, katika miaka mitano ijayo, China itatenga fedha yuan bilioni 200 kwa ajili ya elimu ya lazima, na kutoa elimu ya lazima bila ya malipo vijijini ndani ya miaka miwili.

Mkuu wa ofisi ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya baraza la uchumi na jamii la Umoja wa Mataifa Bibi. Hanifa Mezoui alisema, China ni mfano mzuri ambao unashirikisha vizuri maendeleo ya elimu na uchumi. Maendeleo ya China yametoa mchango kwa utimizaji wa malengo ya maendeleo ya milenia.

Idadi ya watu maskini nchini China imepungua kuwa asilimia 10 ya mwaka 2002 kutoka asilimia 30 katika miaka ya 90 karne iliyopita. China inatimiza hatua kwa hatua malengo mbalimbali ya milenia ambayo yanapangwa kutimizwa ifikapo mwaka 2015, yakiwemo upunguzaji wa umasikini na elimu.

Ili kusukuma mbele utimizaji wa malengo ya maendeleo ya milenia, mwenyekiti wa Shirika la IAESCSI ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza la uchumi na jamii la China Bw. Wang Zhongyu alitoa mwito akiitaka jumuiya ya kimataifa iimarishe ushirikiano ili kuondoa umasikini katika miaka kumi ijayo.

Idhaa ya Kiswahili 2006-04-04