Katika siku za karibuni limejitokeza duka moja la mikate na keki ya aina ya Ufaransa liitwalo "Paris Baquette" katika mtaa wa biashara ulioko mashariki ya mji wa Beijing. Duka hilo lenye nembo ya rangi ya bluu na taa zinazong'ara zenye mwangaza wa manjano, linawavutia wapita njia. Mikate na keki mpya zikiwa tayari, mwoka mikate anagonga kengele na kutangaza majina ya keki hizo. Anasema, "Croissant zilizookwa. Keki za sabuni ziko tayari."
Duka hilo la mikate na keki, ni moja kati ya maduka mengi yaliyoanzishwa hapa Beijing na Kampuni ya SPC ya Korea ya Kusini, ambayo ni kampuni kubwa ya chakula ya Korea ya Kusini kuliko kampuni nyingine za nchi hiyo, na meneja wa duka hilo Bw. Jay Mun anatoka Seoul, mji mkuu wa Korea ya Kusini.
Sasa inakabiria miaka minne tangu Bw. Jay Mun aje nchini China. Alifafanua kuwa uamuzi wake wa kufanya kazi nchini China umetokana na upendo alionao kwa China tangu utotoni mwake.
"Nilipenda kusoma riwaya za Kichina na kutazama filamu za Kichina tangu nilipokuwa mtoto, na hatua kwa hatua niliipenda China. Nilipokuwa katika chuo kikuu, nilijiunga na kitivo cha lugha ya Kichina. Baada ya kuhitimu, nilitaka kufanya kazi zinazohusiana na China."
Bw. Jay Mun alimwambia mwandishi wa habari kuwa, alipokuwa mtoto, dada yake alimfundisha kuimba wimbo mmoja wa Kichina. Alikuwa anajiamini na alisifiwa na majirani na watoto wenzake alipoimba wimbo huo. Hata hivi sasa anajua kuimba wimbo huo.
Baada ya kuhitimu chuo kikuu, Jay Mun aliichagua kufanya kazi katika kampuni ya SPC, baada ya kufahamishwa kuwa kampuni hiyo ilikuwa na nia ya kuwekeza nchini China. Miaka mitatu iliyopita, kampuni ya SPC ilianzisha duka la kwanza huko Shanghai, China ambapo Bw. Jay Mun alipata nafasi ya naibu meneja mkuu.
Duka hilo linapendwa na wateja wa Shanghai tangu kuanzishwa kwake, kutokana na kuuza mikate na keki zenye ladha halisi ya kifaransa. Na katika mwaka huo maduka ya mikate na keki ya kampuni ya SPC yaliongezeka hadi kufikia 9 huko Shanghai. Mafanikio hayo yalifanya kampuni ya SPC kutupia macho Beijing, mji mkuu wa China. Katikati ya mwezi Januari mwaka huu, lilianzishwa duka la kwanza mjini Beijing, na Bw. Jay Mun alihama Shanghai na kuanza kuishi mjini Beijing.
Soko la mikate na keki mjini Beijing lina ushindani mkali. Je, duka hilo "Paris Baguette" limewezaje kupata wateja wengi mjini Beijing? Bw. Jay Mun na wafanyakazi wenzake wana mbinu zao. Anasema, "Kumekuwepo na maduka mengi ya mikate na keki hapa Beijing. Lakini duka letu limekuwa na historia ya miaka 60, kama tunafanya bidii naamini litaweza kuwa miongoni mwa maduka ya mikate na keki yanayopendwa na wateja wengi."
Hivi sasa duka hilo linabadilisha aina za mikate na keki kila siku, na kwa jumla linaweza kuoka aina zaidi ya 250 za mikate na keki, ambazo ni pamoja na mikate inayopendwa na wazungu, pia kuna mikate yenye mboga inayowafurahisha wakazi wa Beijing na keki za aina mbalimbali.
Katika duka hilo, wateja wanaweza kuangalia jinsi waoka mikate wanavyofanya kazi kupitia kioo kikubwa kinachotenganisha chumba cha kuandaa na kuoka mikate na keki, na duka lenyewe. Pia kuna meza na viti na huduma ya kahawa.
Bibi Feng Li anafanya kazi katika kampuni iliyoko karibu. Yeye na marafiki zake kila wanapopita, wanapenda kupumzika kidogo kwenye duka hilo, ambapo wanaagiza aina fulani za kahawa na mikate na keki zilizookwa, wanapiga gumzo.
"Napenda keki za duka hili, ambazo ni tamu kupita kiasi. Pia hapa kuna keki za aina nyingi kuliko maduka mengine."
Duka hilo lina wafanyakazi wapatao 40, na wengi wao ni Wachina. Kwa mtizamo wa wafanyakazi hao, Bw. Jay Mun ni mtu mpole. Msichana Wang Yaoxin mwenye umri wa miaka 20 alitoa tathmini juu ya bosi wake, akisema "Bosi anatuchukulia vizuri. Nafurahi kufanya kazi hapa, tunashirikiana vizuri."
Bw. Jay Mun, mke wake na mtoto wao wa kiume mwenye umri wa miaka miwili wanakaa katika mtaa uitwao Wang Jing, ulioko mashariki ya mji wa Beijing, ambapo wanakaa watu wengi wanaotoka Korea ya Kusini. Kwa vile wanaweza kukutana na watu wengine wa Korea ya Kusini mara kwa mara, kwenye mtaa huo kuna mikahawa mingi ya chakula cha Kikorea, Bw. Jay Mun na familia yake hawasumbuliwi sana na hisia ya kukumbuka nyumbani. Sasa amekuwa na marafiki wengi wa China, na kiwango chake cha lugha ya Kichina pia kimeinuka sana.
Alipoagana na mwandishi wetu wa habari, alieleza kwa Kichina kuwa, angependa kuendelea kuishi hapa Beijing.
"Nina mpango wa kuishi kwa muda mrefu hapa Beijing. Nitaielewa China kwa kina, kuwa na marafiki wengi zaidi, na nitakuwa mkazi halisi wa Beijing. Pia nitafanya chini juu kulifanya duka letu liwe duka linalopendwa na wateja wa Beijing."
Bw. Jay Mun alisema kampuni yake imeamua kuanzisha maduka mengine 6 mjini Beijing mwaka huu, na pia itaeneza maduka yake katika miji mingine ya China.
Idhaa ya kiswahili 2006-04-06
|