Siku moja wakati wa mchana katika majira ya Mchipuko, mkulima mzee Zheng na mke wake walichukua mashine kongwe ya kuoneshea filamu na sanduku moja la chuma lenye rangi ya kijani kutoka kwenye nyumba yao. Halafu wakulima hao wa kijiji cha Shuiqiao, mkoani Sichuan, China walimbebesha farasi mmoja mwekundu vitu hivyo.
Baada ya maandalizi kukamilika, Mzee Zheng na mke wake walifunga safari na farasi wao, kwenda kijiji cha Laomiaozi, kilichopo kilomita 30 mbali na maskani yao kuonesha filamu, filamu moja ilihusu elimu ya kilimo na nyingine ni ya hadithi. Mzee Zheng alimwambia mwandishi wa habari kuwa, waliondoka saa 9 jioni na kufika katika kijiji hicho saa 12 jioni, halafu iliwabidi watumie muda wa zaidi ya saa moja kufunga projekta na mashine, na filamu zenyewe zingeanza kuonyeshwa saa 8 usiku. Hadi kufikia saa 5 usiku filamu zitakuwa zimemalizika, na hadi kufika saa 8 asubuhi ya siku ya pili watakuwa wamesharudi nyumbani kwao.
Mzee Zheng jina lake ni Zheng Xiaoming, na ana umri wa miaka 42. Anapenda sana filamu tangu utotoni mwake. Miaka 6 iliyopita alinunua mashine ya kuonyeshea filamu iliyotumika kwa zaidi ya Yuan elfu 2, kiasi ambacho ni sawa na dola za kimarekani 250. Alianzisha mkahawa wa kuuza chai uitwao mkahawa wa filamu, kwenye kata ambayo ni maskani yake. Katika mkahawa huo, wakulima wakitumia Yuan moja tu kununua kikombe kimoja cha chai wanaweza kutazama filamu kwa siku nzima. Katika mwaka mpya wa Kichina, mzee Zheng alikodisha sehemu moja yenye ukubwa wa mita 30 za mraba ambapo alionesha filamu mbili kwa mfululizo katika siku nzima kwa tiketi ya Yuan moja tu.
Kuanzia mwaka 2004, mzee Zheng alikuwa na wazo la kwenda sehemu za vijiji kuonyesha filamu. Wakati huo huo, serikali ya wilaya ya huko ilikuwa inatekeleza mradi mmoja wa kitaifa uitwao mradi wa 2131, ukilenga kutimiza lengo la kuonyesha filamu moja katika kila kijiji kwa mwezi kuanzia mwanzoni mwa karne ya 21. Kwa hiyo mzee Zheng alitiliana saini mkataba na kampuni ya filamu ya wilaya. Kwa mujibu wa mkataba huo, kampuni ya filamu inawajibika kutoa filamu, projekta na vifaa vinavyohitajika kuonyesha filamu, na mzee Zheng atafanya kazi ya kuonyesha filamu katika sehemu za vijiji.
Kata ya Xinchang iko mbali sana na mji mkuu wa wilaya, kata hiyo ina vijiji 25 ambavyo asilimia 80 ya vijiji hivyo vipo katika sehemu ya milimani na vinaunganishwa na njia zilizoko milimani, kwa hiyo kila anapokwenda vijijini kuonesha filamu, mzee Zheng anapaswa kukodisha farasi kwa Yuan kati ya 10 na 30 ili kusafirisha vifaa.
Ingawa mzee Zheng na mke wake wote wametimiza umri wa miaka 42, lakini safari ngumu ya saa kadhaa kwenye njia zilizoko milimani haiwezi kuathiri ukarimu wao. Mzee Zheng alieleza kuwa, kila mara alipoonesha filamu vijijini na kuwaona wanavijiji wenzake wakimiminika kuzitazama filamu na kuzifurahia, basi alijisikia vizuri sana.
Idhaa ya kiswahili 2006-04-06
|