Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-12 16:23:23    
Walemavu wenye tatizo la kusikia na kusema wamekuwa na "mashine ya kutafsiri"

cri

Je, unafahamu ishara za walemavu wenye tatizo la kusikia na kusema? Na itakuwaje ukitaka kuongea na walemavu hao? Muda si mrefu uliopita, taasisi ya sayansi na teknolojia ya China imefanikiwa kuunda mfumo wa kutambua ishara za walemavu hao, mfumo huo unaweza kuwasaidia watu hao "kuongea" na "kufahamu" watu wa kawaida wanayosema. Hii ndio "mashine ya kutafsiri".

Mwandishi wa habari, "Hujambo!"

Sauti ya mashine, "Sijambo."

Mwandishi wa habari, "Nafurahi kukufahamu."

Sauti ya mashine, "Na mimi pia."

Mwandishi wa habari, "Umezoea kufanya nini usipokuwa kazini?"

Sauti ya mashine, "Nimezoea kutembelea madukani, kutalii au kuburudika na picha za katuni."

Amini usiamini, maongezi mliyosikia hivi punde ni "mazungumzo" kati ya mwandishi wa habari na msichana asiyeweza kusema anayeitwa Ma Yan. Usione ajabu, mazungumzo yote hayo yamepatikana kwa kupitia mfumo wa kutambua ishara za walemavu wenye tatizo la kusikia na kusema. Mfumo huo umebuniwa na taasisi ya sayansi na teknolojia ya China.

Mwandishi wa habari ametueleza kwamba mfumo huo wa kutambua ishara za walemavu wenye tatizo la kusikia na kuongea unafanya kazi kwa kompyuta moja na glavu zinazounganishwa kwenye kompyuta hiyo, ambayo inaweza kubadilisha ishara za Ma Yan kuwa sauti ya lugha na pia inaweza kubadilisha sauti ya lugha ya mwandishi wa habari kuwa ishara za walemavu, mabadiliko hayo kutoka lugha moja hadi nyingine yanatumia sekunde chache tu. Mazungumzo kati ya mwandishi wa habari na msichana huyo Ma Yan yaliendelea bila tatizo.

Mtaalamu aliyeshiriki kwenye utafiti wa mfumo huo Bw. Chen Qiang alisema, kitu muhimu katika mfumo huo ni glavu, walemavu wenye tatizo la kusikia na kusema wakivaa glavu hizo na kufanya ishara za lugha yao, ishara zinatafsiriwa na kuwa lugha ya kawaida kwa sauti. "Kazi ya glavu hizo ni kubadilisha ishara za mikono kuwa tarakimu na kuingiza kwenye kompyuta, na kompyuta inashughulikia taratimu hizo na kuzibadilisha kuwa sauti za lugha."

Bw. Chen Qiang alieleza kuwa, kwenye kila glavu kuna software 18 za transducer na software moja ya kuthibitisha aina ya ishara na kuingiza ishara hizo kwenye kompyuta ambayo inazibadilisha kuwa sauti za lugha."

Lakini msichana huyo anawezaje kufahamu maneno ya mwandishi wa habari? Bw. Chen alieleza, "Hivi sasa kuna software nyingi za kutafsiri matamshi ya lugha kuwa ishara za walemavu wenye tatizo la kusikia na kusema. Mfumo wetu wa kutafsiri matamshi ya lugha kuwa ishara unatumia mikrofoni na software ya kutambua matamshi ya lugha na kisha ishara hiyo inaoneshwa kwa picha za katuni kwenye kioo cha ya kompyuta ikiwaonesha walemavu nini kinachosemwa."

Baada ya kujaribu, 95% ya walemavu wenye tatizo la kusikia na kusema walielewa ishara za picha za katuni, kwa hiyo walemavu hao wanaweza kuongea na watu wa kawaida mambo yote wanayotaka. Imefahamika kuwa hivi sasa nchini China kuna walemavu wenye tatizo la kusikia na kusema kiasi cha milioni 20. Watu hao wanapata usumbufu mkubwa maishani mwao, kwa mfano wakienda kwenye benki kuweka akiba, au hospitali kuonana na daktari. Kwa hiyo mfumo huo hakika unawasaidia sana walemavu hao.

Mwalimu Li wa shule ya tatu ya walemavu wenye tatizo la kusikia na kusema mjini Beijing alisema, maingiliano yote kati yake na wanafunzi wake yanategemea kufanya ishara, na alitumia muda mrefu kwa ajili ya kujifunza namna ya kuongea nao kwa ishara. Sasa imekuwa rahisi kwake kuongea nao kwa mashine hiyo. Lakini alisema, si rahisi kutembea na glavu hizo kutokana na kuwa na nyaya nyingi.

Bi. Tong Wei ambaye anatatizo la kusikia anavutiwa sana na "mashine" hiyo, lakini bei ghali ilimshinda. Alisema, "Nimesikia bei yake ni yuan elfu kumi kadhaa, bei kubwa kama hiyo siwezi kuimudu."

Hivi sasa taasisi ya sayansi na teknolojia ya China imeanza kushughulikia suala la bei hiyo kubwa. Bi. Wang Lichun aliyeshiriki kwenye utafiti wa mfumo huo alisema, glavu za mfumo huo hazidumu sana na bei yake ni kubwa, kwa hiyo wanatarajia kutumia kamera ya video kwenye kompyuta badala ya glavu, namna ya kutambua ishara za mikono itakuwa ni kazi muhimu watakayoishughulikia.

Ingawa hivi sasa "mashine ya kutafsiri" ina dosari yake, hata hivyo imewawezesha walemavu hao kushiriki katika shughuli za jamii sawa na wengine. Msichana mwenye umri wa miaka 16 Tian Meng alikuwa na simanzi kutokana na tatizo la kusikia, lakini aliposikia tunda hilo jipya la sayansi na teknolojia mara aliwaeleza wengine furahi yake, "Mimi naitwa Tian Meng, mwaka huu nimetimiza miaka 16. Naona ajabu sana sayansi ya teknolojia imefikia kiwango kama hicho, kwamba inaweza kubadilisha ishara za mikono yangu kuwa sauti, na mtu asiyeweza kuongea kwa mikono pia anaweza kufahamu ninachosema."

Idhaa ya kiswahili 2006-04-12