Maonesho ya hifadhi ya utamaduni wa jadi usioonekana yanafanyika katika jumba la taifa la makumbusho mjini Beijing. Vitu karibu 2,000 na picha zaidi ya 1,500 vinaoneshwa vikithibitisha mafanikio makubwa katika juhudi za hifadhi ya utamaduni huo.
Ndani ya jumba hilo, mashine moja kubwa ya mbao iliwavutia sana watazamaji. Mashine hiyo ina urefu wa mita sita, upana wa mita moja na urefu wa kwenda juu mita nne. Hii ni mashine ya kufumia kitambaa, mafundi wawili walikuwa wakipitisha nyuzi kutoka pande tofauti kwa kuonesha jinsi watu wa kale walivyofuma vitambaa.
Mashine hiyo ilisafirishwa kutoka Mji wa Nanjing, mji ambao ulikuwa maarufu katika utengenezaji wa hariri katika zama za kale. Mkuu wa Taasisi ya Ufumaji Nguo za Kifalem mjini Nanjing Bw. Wang Baolin alieleza kuwa, mashine kama hiyo ilikuwa ikitumika kwa ajili ya kuwafumia wafalme majoho kwa manyoya ya tausi na nyuzi za dhahabu, ufumaji unataka ufundi mkubwa na kazi inachukua muda mrefu sana, kwa siku moja inawezekana tu kufuma sentimita za mraba 40 hivi. Bw. Wang alisema, "Kitambaa kilichofumwa kwa mashine hiyo ni maridadi kutokana na kufumwa kwa ufundi mkubwa na kwa nyuzi zenye rangi hamsini."
Kutokana na kuwa kazi hiyo inachosha, vijana wa siku hizi hawataki kufanya kazi hiyo na ufundi wake unakaribia kutoweka. Ili kudumisha ufundi huo wa jadi, Taasisi ya Ufumaji Nguo za Kifalme mjini Nanjing imeandaa mafundi zaidi ya sitini wa ufundi huo, na imedhamiria kurithisha ufundi huo kwa kushirikiana na shule kufundisha wanafunzi wenye elimu ya lugha za kigeni na uchoraji, na pia itaomba UNESCO iorodheshe utamaduni huo katika urithi wa utamaduni duniani.
Ndani ya Jumba la Taifa la Makumbusho pia kuna wasichana kadhaa wa kabila la Wapumi wakishikana mikono wakiimba na kucheza kwa furaha. Kabila la Wapumi ni moja ya makabila katika mkoa wa Yunnan, kusini magharibi mwa China, hivi sasa kuna Wapumi elfu 30 tu, nyimbo zao zinapungua siku hadi siku kama idadi ya watu wa kabila hilo. Kutokana na hali hiyo Wizara ya Utamaduni ya China imeanzisha kikundi maalumu kwa ajili ya kurithisha utamaduni wao. Mmoja kati ya wasichana hao, Rong Mi, alisema, "Wimbo tulioimba hivi punde ni wimbo tuliofundishwa na babu yetu. Sisi wasichana tunapokuwa pamoja huimba nyimbo hizo ingawa bado hatujaweza kuimba zote. Sisi wanane tumechaguliwa na mwalimu wetu kwa ajili ya kueneza nyimbo hizo."
Mwalimu aliyetajwa na msichana Rong Mi ni kiongozi wa kikundi cha utamaduni huo, alisema, kikundi hicho kimeanzishwa miaka mitatu iliyopita. Alisema, "Lengo la kufanya hivyo ni kwa ajili ya kutoa mfano wa namna ya kurithisha utamaduni wa kale kwa kupitia kuwafundisha vijana ambao baada ya wao kuwa warithi wataeneza utamaduni huo baada ya kurudi vijijini."
Maonesho kama hayo ni mara ya kwanza kufanyika tokea China mpya ianzishwe. Ndani ya jumba la makumbusho kuna vitu vingi vya kuonesha utamaduni wa kikabila kama vile nguo ya ngozi ya samaki ya kabila la Wahazhe, picha za mtindo wa kabila la Watibet na kinanda cha kale cha guqin nyimbo za kale za kabila la Wamongolia na kadhalika. Na vitu hivyo vimechaguliwa kutoka kwenye vitu zaidi ya 6,000 vilivyokusanywa kutoka sehemu mbalimbali kote nchini China ambavyo kila kimoja kinawakilisha aina moja ya utamaduni wa kale uliopo miongoni mwa wananchi. Hayo ni mafanikio makubwa katika juhudi za kuhifadhi utamaduni wa kale usioonekana.
Tokea miaka ya 50 ya karne iliyopita, serikali ya China imechukua hatua nyingi za kuhifadhi utamaduni wa kale usioonekana, mathalan, kufanya uchunguzi kote nchini, kurekodi na kuratibu, kufanya utafiti na kuhifadhi, na kuchapisha juzuu nyingi za utamaduni huo hasa katika juhudi za kuhifadhi opera ya Kibeijing, opera ya Kunqu na kongfu.
Lakini kutokana na utandawazi wa uchumi unavyoendelea haraka, utamaduni wa jadi usioonekana unakabiliwa na hatari ya kutoweka. Tokea karne hii ianze serikali ya China imetilia mkazo zaidi katika juhudi za kuhifadhi utamaduni huo na imetunga sheria za hifadhi hiyo. Muda si mrefu uliopita serikali ya China iliamua kila J'mosi ya pili katika mwezi Juni iwe "siku ya urithi wa utamaduni" nchini China, ili kuwakumbusha Wachina wote wazingatie hifadhi ya urithi wa utamaduni. Naibu waziri wa utamaduni wa China Bw. Zhou Heping alisema, "Kwa maandishi na kuonesha vitu, picha na maonesho ya warithi tunataka kuwafahamisha watazamaji hali ilivyo ya utamaduni wetu wa jadi usioonekana, na mafanikio tuliyopata katika juhudi za miaka mingi."
Idhaa ya kiswahili 2006-04-17
|