Familia kubwa ilikuwa ni sehemu ya utamaduni wa China, ambapo wanafamilia wa vizazi vitatu hata vinne kuishi kwa pamoja ilikuwa hali ya kawaida. Lakini baada ya sera ya uzazi wa mpango kuanza kutekelezwa nchini China tokea mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita, hatua kwa hatua familia kubwa imeanza kutoweka, na hivi sasa kuna watoto na vijana karibu milioni 100 wasio na kaka wala dada kote nchini. Namna gani vijana hawa watajenga uhusiano na watu wengine, ni changamoto isiyoepukika kwao.
Uchunguzi mmoja kuhusu "upweke na upendo wa jamaa unamkabili mtoto pekee katika familia nyingi ulikamilika hivi karibuni, ambao uliowashirkisha watu zaidi ya elfu 6 nchini China. Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi huo, asilimia 61.3 ya walioulizwa waliona, mtoto pekee ana upweke zaidi ambao si rahisi kushirikiana na wengine katika kupata raha au kukabiliana na dhiki. Na asilimia 66.9 ya watu walieleza matumaini ya kupata ndugu wengine.
Sera ya uzazi wa mpango ilianza kutekelezwa miaka ya 70 ya karne iliyopita nchini China, mpaka hivi sasa watoto wasio na kaka wala dada karibu milioni 100 wamezaliwa. Na kati yao, wale waliozaliwa katika miaka ya 80 hivi sasa wamekuwa wazima, na waliozaliwa katika miaka ya 90 wameingia katika kipindi cha ujana.
Upweke ni neno linalotajwa mara kwa mara na watoto hao wasio na kaka wala dada. Ingawa wengi kabisa miongoni mwao wako karibu sana na wazazi wao, lakini wanaonekana kuwa wapweke zaidi kuliko watoto waliokuwa wanaishi katika familia kubwa za jadi hapo awali.
Katika mtizamo wa jadi nchini China, watu wakipata matatizo walitafuta misaada kutoka kwa jamaa. Lakini watoto wa hivi sasa wanatilia maanani zaidi marafiki na urafiki. Bw. Jin Long mwenye umri wa miaka 23 anasoma shahada ya tatu kwenye taasisi ya taaluma ya mwangaza ya kisasa ya Chuo kikuu cha Nankai cha China, alisema mawasiliano ya dhati kati ya marafiki ni muhimu sana. Alisema, "Nikisumbuliwa na upweke, huwa nakwenda kukutana na marafiki na tunakula chakula kwa pamoja."
Katika sekondari moja mjini Beijing, wanafunzi 10 waliohojiwa na mwandishi wa habari walieleza kuwa, ni lazima mtu awe na urafiki na upendo wa jamaa zake, ama sivyo maisha yake hayana maana yoyote. Ingawa wengi wa wanafunzi hao walieleza umuhimu wa udhati na uaminifu, lakini waliona matukio ya kukosa udhati na uaminifu yapo mengi katika dunia ya watu wazima, hususan katika uhusiano wa kibiashara.
Katika jamii ya zama za hivi sasa yenye mbinu za upashanaji habari, mtandao wa Internet ni njia muhimu ya mawasiliano kati ya watoto wengi wa China ambao ni wa pekee katika familia yao na marafiki zao. Kujenga urafiki na kupiga sofa kupitia mtandao wa Internet ni mtindo wao. Lakini kwa upande mwingine inawabidi wachukue tahadhari, kwa kuwa kwenye mtandao wa Internet kuwa vitendo vyingi vya udanganyifu. Kijana Jin Long alisema, "Hivi sasa tunaweza kupata marafiki wa aina mbalimbali, wakiwemo marafiki wa karibu, lakini wakati mwingi tunajilinda. Na si rahisi kupata marafiki wanaoongea kila kitu bila kuficha."
Kwa upande mmoja watoto hao wana hamu ya kueleweka na wengine, lakini kwa upande mwingine wanahofia kujenga uhusiano wa karibu. Wataalamu wa kijamii wanachambua kuwa, watoto hao walipata mafunzo ya jadi na kufuata vigezo vya maadili walivyofundishwa na wazazi wao, lakini pia wanaathiriwa na utamaduni wa kigeni, vikiwemo vigezo vya maadili na jinsi ya kuishi. Kwa hiyo athari za tamaduni hizo tofauti zimeonekana katika mawasiliano kati yao na watu wengine.
Mapenzi na ndoa ni mambo mawili yanayoweza kupima uhodari wa watoto hao wa kushughulikia mahusiano kati yao na wengine. Hivi sasa kizazi cha kwanza cha watoto wasio na ndugu wametimia umri wa kufanya ndoa. Uchunguzi unaonesha kuwa, kwa ujumla wanathamini mapenzi na kutilia maanani ndoa, lakini tofauti na wazazi wao, wanataka uhuru zaidi wa hisia na kuwa na mawazo wazi ya kujiamiiana kabla ya ndoa. Bw. Zhang Guo mwenye umri wa miaka 24 anayefanya kazi ya usimamizi katika Chuo kikuu cha Nankai alisema, "Natumai pande mbili za wapenzi ziwe na uhuru, bila kuingilia kati maisha ya upande mwingine, wala kutotegemea upande mwingine kifedha."
Kwa maoni ya wazazi wa watoto hao na wataalamu wa kijamii, watoto hao wanaoishi katika kipindi ambacho China inabadilika, wanapaswa kupewa mwongozo. Profesa Hao Maishou wa Taasisi ya sayansi ya jamii ya Tianjin alieleza maoni yake kuwa, kutokana na uekekazaji sahihi mwafaka, watoto hao wanaweza kuimarika kimawazo na kuwa na uwezo wa kufanya ushirikiano, na wataweza kubeba wajibu wa kijamii katika siku zijazo.
Idhaa ya Kiswahili 2006-04-20
|