Kikosi cha kulinda amani cha China chenye wanajeshi 600 tarehe 18 mwezi huu kiliondoka Beijing kwenda Liberia kutekeleza jukumu la kulinda amani la Umoja wa Mataifa. Hii ni mara ya kwanza kwa jeshi la sehemu ya Beijing kutekeleza jukumu hilo, ambalo limetuma vikosi vitatu vya uhandisi, uchukuzi na madaktari.
Mwandishi wetu wa habari aliwatembelea wanajeshi hao kabla hawajaondoka mjini Beijing kuelekea Liberia kutekeleza jukumu la kulinda amani.
Nchi ya Liberia iliyopo magharibi ya bara la Afrika ina rasilimali nyingi, lakini kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muda mrefu, miundo mbinu ya nchi hiyo imeharibika vibaya, magonjwa mengi kama vile malaria na kipindupindu yameenea nchini kote, watu wa huko wanaishi maisha duni. Walipopata habari ya kutekeleza jukumu la kulinda amani nchini Liberia, askari na maofisa wengi wa jeshi la sehemu ya Beijing walitoa ombi la kujiunga na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa
Daktari wa idara ya mifupa ya hospitali ya jeshi la sehemu ya Beijing Bwana Liu Shuqing kwenye barua yake ya maombi alisema: "Kujiunga na jeshi la kulinda amani ni jukumu takatifu, japokuwa umri wangu ni mkubwa kidogo, lakini naamini kuwa, nitaweza kukamilisha vizuri jukumu langu, naomba nikubaliwe kujiunga na jeshi hilo."
Daktari wa idara ya neva Bw. Wang Guoqiang alipopata habari ya kukubaliwa ombi lake alifurahi sana, alisema: "Binti yangu anasoma nchini Marekani, mke wangu anafanya kazi nchini China, na mimi nitaenda Liberia kutekeleza jukumu la kulinda amani, sisi watatu tunagawanyika katika mabara matatu, kama tunaishi katika kijiji cha dunia."
Askari Chen Bingpu mwishoni mwa mwaka jana alikuwa amefanya uamuzi wa kurudi nyumbani huko Shenyang, sehemu ya kaskazini mashariki mwa China ili kufunga ndoa, familia yake ilikuwa hata imeshalipa fedha ya kuandaa karamu hotelini, na kuwaarifu jamaa kuhusu ndoa yake. Lakini mchumba wake alipaswa kuahirisha muda wa kufunga ndoa kutokana na yeye kuandikishwa kujiunga na jeshi la kulinda amani.
Ili kushiriki katika shughuli za kulinda amani nchini Liberia, askari zaidi ya 20 walipaswa kuahirisha muda wao wa kufunga ndoa, ambapo askari wengine zaidi ya 40 walipaswa kuwaomba wazee wao waje Beijing kuangalia watoto wao au kuwapeleka watoto wao nyumbani kwa wazee.
Imefahamika kuwa, kufahamu lugha ya Kiingereza ni changamoto kubwa kwa askari wengi wa China watakaokwenda nchi za nje kutekeleza jukumu la kulinda amani. Msaidizi wa kikosi cha madaktari Bwana Jia Zhende alisema kuwa, ili kuinua kiwango chao cha lugha ya Kiingereza, madaktari watakaotekeleza jukumu la kulinda amani nchini Liberia walijilazimisha kutumia lugha ya Kiingereza katika kazi na maisha ya kila siku.
Wanajeshi wa kikosi cha uhandisi na kikosi cha uchukuzi licha ya kumaliza mazoezi yaliyowekwa, pia waliongezewa mazoezi katika barabara, madaraja na milipuko ya mabomu, pia walifanya mazoezi ya kisaikolojia, ili kuongeza uwezo wa uvumilivu na kushirikiana katika kikundi.
Maandalizi ya kutekeleza jukumu la kulinda amani yalikuwa na pilika pilika nyingi. Mhusika wa ofisi inayoshughulikia mambo ya kulinda amani ya jeshi la sehemu ya Beijing alifahamisha kuwa, japokuwa kikosi cha madaktari kitaanzisha hospitali yenye kiwango cha chini tu nchini Liberia, lakini walipaswa kutayarisha vifaa vya aina elfu moja hivi, yakiwemo madawa ya aina zaidi ya 400.
Shughuli za kulinda amani ni za kisiasa,wanajeshi a China wanapaswa kuwa na uwezo wa kujitegemea na kukabiliana na mazingira magumu. Kwa hivyo wanajeshi wa vikosi mbalimbali vya jeshi la sehemu ya Beijing walikuwa wameelimishwa kuhusu jinsi ya kujikakamua, ambapo walitunga mipango ya aina mbalimbali ya utekelezaji. Kikosi cha uchukuzi pia kilitunga vijitabu kuhusu ujuzi wanaopaswa kufahamu, maswali 100 kuhusu jinsi watakavyotenda shughuli za kulinda amani na lugha ya Kiingereza kuhusu kulinda amani, kikosi cha madaktari kilijitayarisha kwa ujuzi mwingi jinsi ya kupambana na magonjwa ya kuambikizwa.
Idhaa ya Kiswahili 2006-04-20
|