Bara la Afrika linajizatiti kidhabiti kuenea kwa magonjwa mbalimbali kama vile homa ya malaria, kifua-kikuu, virusi vya Ukimwi, ukambi na mengineyo, sanjani na hilo madaktari nao hawajasahau kujituma katika kidhabiti kuenea kwa maradhi tofauti tofauti ambayo huathiri figo.
Uchunguzi uliofanywa na washika-dau katika sekta ya afya nchini Kenya umeonyesha kuwa watu kama wanne ama watano hivi kati ya watu 100, hupata matatizo ya figo barani Afrika kila siku, hii ikiwa ni mara nne zaidi ya idadi ya mataifa yaliyoendelea. kadhalika watu wengine laki saba kati ya watu milioni 14 walioko nchini Kenya wakikumbwa na maradhi ya figo mwaka hadi mwaka.
Nazo takwimu zilizofanywa katika mataifa yenye ustawi mkubwa duniani, zimeonyesha kuwa watu kati ya 25 na 30 kwa kila watu milioni moja hukumbwa na matatizo ya figo.
Wengi wa waathirika wa maradhi ya figo ni kina mama. Hiyo imetokana na sababu kuwa kina mama huona haya kutafuta tiba zaidi wanapokuwa wakiuguza sehemu zao za siri, ikiwemo vibofu vya mikojo na mifereji ya kupitisha mikojo.
Shinikizo kuu la damu yaani high-blood pressure, pamoja na athari nyengine ambazo huukumba mwili, ndiyo sababu kuu zenye kusababisha ugonjwa wa figo. Wakati kinga za mwili zinapokuwa zikimenyana kudhibiti kuenea kwa maradhi mwilini, wakati mwengine hubidi figo pia kusaidia katika kupambana na kemikali hizo za maradhi na hapo kuishia kuambukizwa.
Dr. Mohammed Abdulla kutoka hospitali kuu ya Aga Khan jijini Nairobi, nchini Kenya, anasema kuwa mbali na shinikizo kuu la damu, ni kuwa sababu nyengine zinazopelekea figo kuathiriwa ni pamoja na matumizi mengi ya sukari kupita kiasi.
Amesema Dr. Abdalla, 'Baadhi ya wagonjwa wanaoguza figo zao ni kutokana na hali zao za za kimaisha. Utaona wengi wa wagonjwa ni wale wanaotumia pembe kupita kiasi. Figo huathirika mno pale mhusika anapoanza kuvuta sana sigara na kunywa pombe kupita kaisi.'
Daktari huyo pia amethibitisha kuwa baadhi ya maradhi ya figo huambukizwa kwa kuzaliwa, ambapo mtoto anaweza kuzaliwa akiwa kaambukizwa maradhi hayo na wazazi wake. Ugonjwa ambao katika taaluma ya utabibu hujulikana kama genetics, yaani urithi. Inakisiwa kuwa zaidi ya watu laki moja kote duniani huzaliwa wakiwa na figo moja pekee, lakini huwa hawajui, mpaka wanapopimwa na madaktari. Hao ndio baadhi ya wagonjwa ambao huugua maradhi bila kubaini, maarufu katika taaluma ya utabibu kama silent killers.
"Wengi wa watu huwa hawajui kuwa wana shida za figo, ama wamezaliwa na figo moja, hadi tunapowapima ndipo tunapowabainishia kuwa wana matatizo ya figo. Kina mama wengi hushindwa kujua ni kwa nini watoto wao wachanga hulia sana, na pindi wanaponyamaza wanatokwa na mkojo mwingi. Hiyo huwa dalili tosha kuwa watoto kama hao wanauguza figo zao.' Ameongeza Dr. Abdallah.
Lakini habari njema kutoka kwa daktari huyo ni kuwa nchi ya Kenya inajivunia kuwa na mitambo na vifaa madhubuti vya kutibu maradhi ya figo. Kadhalika, Kenya inajivunia kuwa na madaktari wapatao 20 kote nchini katika miji ya Nairobi, Mombasa, Nakuru na Kisumu.
'Kenya ina madaktari shupavu wa figo na hospitali kuu kama Nairobi Hospital, hospitali kuu ya Kenyatta, Aga Khan zote zina madaktari kamili za kutibu figo. Hii ndio sababu kuu inayowafanya wagonjwa kutoka katika mataifa jirani kama vile Ethiopia, Rwanda, Burundi, Uganda, Tanzania na kwengineko kuja Kenya kwa matibabu, kwa kuwa nchi hizo sio tu kuwa hazina vifaa vya kutibia figo, bali pia hazina watalaamu waliofuzu wa kutibu figo.' Alidokeza Dr. Abdallah.
Hata hivyo, Dr. Abdalla amewaasa wagonjwa wa shinikizo la damu na kisukari kuzingatia kikamilifu tiba yao na hata kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara, ili figo zao zisije zikaharibika kiasi kikubwa, na kuingia gharama kubwa ya matibabu.
Upasauji wa figo hugharimu kama dola 15, huku wale wagonjwa wenye kusafisha figo zao, hubidi kufanyiwa uchunguzi wa kama mara moja ama mbili kwa kila wiki, na kulipa dola saba kwa kila uchunguzi.
Kabla ya mtu kutolewa figo na kupewa mwingine, sharti damu zao zilingane, asiwe na maradhi ya kuambukiza, na pia figo zake zote mbili ziwe zafanya kazi kikamilifu.
Idhaa ya kiswahili 2006-04-26
|