Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-27 16:10:00    
Kabila la Wazhuang na utamaduni wa matamasha ya nyimbo za kienyeji

cri

Tamasha la nyimbo za kienyeji la kabila la Wazhuang linajulikana nchini China. Tamasha hilo ni utamaduni maalumu wa Wazhuang wanaoishi katika mkoa unaojiendesha wa kabila la Wazhuang wa Guangxi, kusini magharibi mwa China.

Wilaya ya Wuming mkoani Guangxi ni moja kati ya sehemu za chimbuko la utamaduni wa kabila la Wazhuang. Hivi karibuni katika bustani moja wilayani humo, mwandishi wetu wa habari alishuhudia mamia ya wasichana na wavulana waliovalia mavazi ya rangi ya kibuluu ya kabila la Wazhuang waliojaa katika uwanja mmoja, ambapo vijana hao kutoka sehemu mbalimbali mkoani Guangxi walikuwa wanashindana kwa uimbaji wa nyimbo za kienyeji, hali ambayo ilibadilisha bustani hiyo kama bahari ya nyimbo.

Mbona Wazhuang ni hodari katika uimbaji wa nyimbo za kienyeji? Bw. Su Xianqing anayetoka kabila la Wazhuang, alisema Wazhuang wanapenda kueleza maoni na hisia zao kwa kuimba katika maisha yao. Alisema, "Wazee wakichoka baada ya kuchapa kazi kwa siku nzima, wanapenda kueleza maoni yao kwa kuimba nyimbo za kienyeji. Wasichana na wavulana wanabadilishana hisia za mapenzi kwa kuimba nyimbo za kienyeji, na watoto pia wanaimbaimba kwa kujieleza hisia zao."

Matamasha mbalimbali ya nyimbo za kienyeji hufanyika wilayani Wuming kila mwaka kati ya tarehe 3 Machi na tarehe 5 May kwa kalenda ya Kichina. Bw. Meng Shuisheng ambaye anajulikana kama mwimbaji bingwa anashiriki kwenye matamasha ya nyimbo za kienyeji kila mwaka. Alieleza kuwa kipindi cha kuandaa matamasha hayo kinaamuliwa kutokana na uzalishaji wa kilimo. Alisema, "Wakazi wa huko wana desturi ya kuanza kulima mashamba tarehe 5 May, kwa hiyo kuanzia siku hiyo wana kazi nyingi na matamasha ya nyimbo za kienyeji yanasitishwa. Baada ya kupata mavuno wanaanzisha tena harakati za kuimba. Hali hii inarudia kila mwaka."

Inasemekana kuwa matamasha ya nyimbo za kienyeji yanatokana na hadithi moja. Bw. Meng alisema hapo zamani kulikuwepo mwimbaji mzee wa kabila la Wazhuang, binti yake alikuwa ni mrembo sana na hodari katika kuimba nyimbo za kienyeji. Mzee alitumai kumchagua kijana aliye hodari katika uimbaji awe mume wa binti yake. Kwa hiyo vijana wa sehemu mbalimbali walikusanyika wakishindana kuimba nyimbo ili kupata mapenzi ya msichana huyo. Na kuanzia hapo matamasha ya nyimbo za kienyeji yalianza kufanyika kila mwaka.

Hivi sasa kuushindana kuimba nyimbo za kienyeji kunatawala matamasha ya nyimbo za kienyeji. Lakini mbali na hayo, pia kuna shughuli nyingine nyingi zenye umaalumu wa kabila la Wazhuang, kama vile wasichana na wavulana kutupiana mipira midogo yenye nakshi inayotengenezwa kwa vitambaa, kurusha fashifashi na kucheza ngoma ya bambuu.

Licha ya hayo, Wazhuang pia wanaandaa shughuli mbalimbali nyumbani kwao, kwa mfano wanawaalika jamaa na marafiki kula chakula kwa pamoja. Bw. Su Xianqing alieleza, "Kwa desturi ya kabila letu, inapowadia kipindi cha matamasha ya nyimbo za kienyeji, kila familia inapika wali wenye rangi tano, kuchinja kuku na taba wengi na kuandaa mapishi mbalimbali. Mpaka hivi sasa sisi watu wa kabila la Wazhuang bado tunaendelea kufuata desturi hiyo."

Mbali na chakula kizuri, pombe ni kitu kisichokosekana katika kipindi cha matamasha ya nyimbo za kienyeji. Mwimbaji bingwa wa wilaya ya Wu Ming Bw. Meng Shuisheng alisema, "Tunaimba huku tunakunywa pombe, na familia inayowavutia wageni wengi kuliko nyingine ina fahari kubwa. Ni bora kutembelewa na wageni wengi, tunawakaribisha kwa pombe, na wakishamaliza pombe zao wanaimba. Shamrashamra za namna hii zinaendelea usiku kucha."

Hivi sasa kiwango cha maisha cha watu wa kabila la Wazhuang kimeinuka sana, kwa hiyo wana hamu kubwa kushiriki kwenye matamasha ya nyimbo za kienyeji. Na jambo linawafurahisha ni kuwa matamasha hayo yametiliwa maanani na serikali ya huko. Bw. Su Xianqing alieleza maoni yake. Alisema, "Hapo awali matamasha ya nyimbo za kienyeji yaliandaliwa na wanavijiji wenyewe tu, ambayo yalikuwa ni madogo. Lakini hivi sasa ni serikali inayoshughulikia matamsha hayo, na kuwavutia wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali."

Sifa za matamasha ya nyimbo za kienyeji wilayani Wu Ming zimeenea sana katika miaka ya hivi karibuni. Matamasha hayo si kama tu yamewavutia wenyeji mkoani Guangxi, bali pia watalii kutoka sehemu mbalimbali nchini humo, ambao wanataka kushuhudia matamasha hayo na utamaduni wa kabila na Wazhuang. Katibu mkuu wa kamati ya chama ya wilaya ya Wu Ming Bw. Su Shaorong alisema, "Kuimba nyimbo za kienyeji na kushiriki kwenye matamasha ya nyimbo za kienyeji ni utamaduni wa kabila letu la Wazhuang, pia ni utamaduni wa wilaya yetu ya Wu Ming. Kutokana na jitihada za serikali, matamasha hayo yanawavutia wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali za China, zikiwemo Hong Kong, Macao na Taiwan."

Mkipata nafasi ya kutembelea China, msisahau kushiriki kwenye matamasha ya nyimbo za kienyeji ya kabila la Wazhuang, na kutembelea familia za Wazhuang zenye ukarimu mkubwa.

Idhaa ya kiswahili 2006-04-27