Kati ya makabila madogomadogo hapa nchini China, kabila la Wahui ni kabila linalopenda Wushu. Tangu enzi na dahari, kulikuwa na desturi za kufanya mazoezi ya Wushu katika makazi wanayoishi Wahui wengi. Hapa mjini Beijing ambao ni mji mkuu wa China, hivi sasa pia kuna Wahui wengi wanaocheza Wushu.
Kwenye mtaa wa Niujie uliopo kusini ya Beijing wanapoishi watu wengi wa kabila la Wahui, kuna klabu moja ya Wushu inayowashirikisha wakazi wengi wa mtaa huo. Katika siku za kazi wakazi wa mtaa huo wanafanya kazi mbalimbali, na baada ya kazi au katika siku za mapumziko wanakutana kwenye klabu ya Wushu kufanya mazoezi kwa pamoja na kujadiliana masuala ya maisha yanayohusu mchezo wa Wushu.
Je, ni kwa nini watu wa kabila la Wahui wanapenda kucheza Wushu? Bw. Zhang Bin ambaye ni mwanachama wa klabu hiyo alituelezea kuwa, hapo zamani ili kujilinda katika vita, Wahui walikuwa wanafanya mazoezi ya kupanda farasi, kutumia pinde na mishale, kucheza na mapanga na fimbo, wakiichukulia Wushu kuwa ni mbinu muhimu ya kujilinda. Bw. Zhang alisema, "Katika historia watu kadhaa wakifanya mazoezi ya Wushu walikuwa na lengo la kujilinda."
Baba yake alikuwa anacheza Wushu, kwa hiyo Bw. Zhang Bin alishuhudia shughuli za Wushu tangu alipokuwa mtoto mdogo. Kama alivyoeleza, "Kuna baadhi ya vitendo sikujifunza kwa bidii, lakini navifahamu." Alipokuwa na umri wa miaka kati ya 17 na 18, Zhang Bin alianza rasmi kushiriki kwenye mazoezi ya mchezo wa Wushu. Hata hivyo kijana huyo alikuwa hafanyi mazoezi kwa bidii. Alipokuwa na umri wa miaka zaidi ya 20, Zhang Bin alitambua kuwa anapenda sana mchezo wa Wushu, na kuanza kufanya mazoezi kwa makini. Baadaye alishiriki kwenye mashindano mbalimbali ya mchezo wa Wushu yaliyofanyika mjini Beijing na kupata nafasi kadhaa. Mafanikio hayo yalimfanya apende zaidi mchezo huo.
Hivi sasa Bw. Zhang ni mmiliki wa kampuni moja, anakabiliwa na kazi nyingi. Hata hivyo haachi mchezo wa Wushu, bali anaendelea na mazoezi kwa kutumia muda wa mapumziko.
Kama ilivyo kwa Bw. Zhang, naibu mkuu wa klabu ya Wushu ya mtaa wa Niujie Bw. Yang Hongliang pia ni shabiki wa mchezo wa Wushu. Jamaa zake wanajua kucheza mieleka ya mtidno wa kabila la Wahui, kwa hiyo alikuwa na ndoto ya kujifunza Wushu tangu utotoni mwake. Lakini alianza kufanya mazoezi ya Wushu baada ya kutimiza umri wa miaka 20. Mwanzoni alipokuwa akicheza mchezo wa Wushu, kutokana na kutofahamu mbinu za mazoezi, Bw. Yang Hongliang aliona mchezo wa Wushu na ndoto zake zilikuwa na tofauti kubwa, na mazoezi ya Wushu yalikuwa na vitendo fulani vya kurudiwarudiwa na kuwachosha sana watu, kwa hiyo aliwahi kufikiria kuacha mazoezi. Lakini alipoelewa mbinu za mazoezi ya mchezo wa Wushu, Bw. Yang alitambua manufaa ya kucheza Wushu hatua kwa hatua. Alisema, "Kucheza Wushu kunaweza kujenga mwili. Sasa nina afya nzuri kutokana na kufanya mazoezi ya Wushu. Mbali na hayo, kutokana na kucheza mchezo huo wa Wushu, maisha yangu yamejaa furaha na pia inasaidia kujenga maadili. Nimejifunza mengi kutoka kwenye mchezo huo wa Wushu."
Bw. Yang na wenzake wanacheza mara kwa mara mchezo wa Wushu wa ngumi ya mtindo wa Bai Yuan Tong Bei. Tukitaja mtindo huo wa ngumi, ni lazima tutamzungumzia Bw. Zhang Guizeng, mwanzilishi wa klabu ya Wushu ya mtaa wa Niujie, ambaye ni bingwa wa Wushu, pia ni baba wa Bw. Zhang Bin na mwalimu wa Bw. Yang Hongliang. Bw. Zhang Guizeng alizaliwa katika mtaa wa Niujie, na alianza kujifunza Wushu alipokuwa na umri wa miaka 11. Alipata maendeleo kwa haraka sana kutokana na kipaji na bidii zake.
Lakini alipokuwa kijana, ngumi ya mtidno wa Bai Yuan Tong Bei ulikuwa uko hatarini kupotea. Bw. Zhang akishirikiana na rafiki zake waliocheza Wushu kwa pamoja, walitumia miaka 30 kutafuta mabingwa mbalimbali wa Wushu, ili kujifunza ngumi ya mtindo huo. Walikusanya data na kuweka kumbukumbu za ngumi ya mtindo huo.
Bw. Zhang Guizeng aliwapa mafunzo wanafunzi wengi. Akiondoa desturi ya kutowafundisha watu wa makabila mengine mchezo wa Wushu wa mtindo wa kabila la Wahui, si kama tu aliwafundisha Wachina wa makabila mbalimbali, bali pia alikuwa na wanafunzi wa nchi nyingine za Japan na Korea ya Kusini. Bw. Zhang alifariki dunia mwaka jana, lakini anasifiwa na watu kwa mchango aliotoa katika kueneza moyo wa Wushu ya China. Naibu mkuu wa Shirikisho la mchezo wa Wushu la Beijing Bw. Zhang Xinbin alikuwa mwanafunzi wake. Ingawa yeye anatoka kabila la Wahan, alifundishwa na mwalimu Zhang bila kufichwa.
Mtoto wa mzee Zhang Guizeng na wanafunzi wake wamerithi moyo wake wa Wushu na kueneza mchezo huo kwa mwa watu wengi. Hivi sasa katika mtaa wa Niujie, kuna watu wengi wanaofanya mazoezi ya Wushu na wanajitokeza mara kwa mara kwenye mashindano mbalimbali ya mchezo wa Wushu.
Ofisa wa mtaa wa Niujie Bibi Meng Ying alitoa maoni yake kuhusu watu hao wanaocheza Wushu, akisema "Wanashiriki katika juhudi za kuendeleza mchezo wa Wushu nchini China. Pia wanatoa mchango kwa mtaa wetu wa Niujie tunaoishi watu wa kabila la Wahui, ambapo kuanzia walimu wao wa vizazi kadhaa vilivyopita, wamekuwa wanarithi na kuendeleza Wushu ya kikabila na utamaduni wa kikabila."
Katika miaka ya hivi karibuni, sura ya mtaa wa Niujie imebadilika sana kutokana na ukarabati mkubwa. Lakini jambo ambalo bado halijabadilika ni Wushu ya huko na moyo wa Wushu ambao wachezaji wanapokezana kizazi baada ya kizazi.
|