Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-08 15:11:52    
Mikahawa ya chai katika mji wa Chengdu, China

cri

Wakazi wa mji wa Chengdu wana mazoea ya kucheza karata na kunywa chai, mazoea hayo ya kuishi kwa kujiburudisha yanajulikana nchini China. Katika kipindi hiki cha "safari katika China" tunawaletea maelezo kuhusu mikahawa ya chai mjini Chengdu.

Wakazi wa mji wa Chengdu wana mazoea ya kunywa chai, kwa hiyo mikahawa ya chai ni mingi mjini humo, licha ya kuwepo katika mitaa ya biashara, pia inakuwepo katika vichochoro na bustani, kwa kifupi ukitembea hatua chache tu utakuta mkahawa mmoja, na kila mkahawa huwa na watu wengi, jinsi biashara ya mikahawa inavyostawi hata unaona ajabu.

Wakazi wa mji wa Chengdu wanapenda kunyuwa chai katika mikahawa, kwa sababu huko wanaweza kupiga soga, kuzungumzia jambo lolote wanalopenda. Mkahawa ni kama jamii ndogo ambayo ndani yake kuna wafanyabiashara wanaozungumza mambo ya biashara, kuna wazee wastaafu wanaopitisha wakati, kuna marafiki wanaozungumzia mambo yao ya zamani na kuna wachumba wanaoelezana habari zao za mapenzi. Kijana Zhao Shengsheng aliyezoea kunywa chai katika mikahawa alisema, chai inaweza kukata kiu, na pia inaburudisha akili, baada ya kumaliza kikombe kimoja, akili inakuwa timamu na maneno yaliyokuwa moyoni yanabubujika bila mwisho.

"Nikipata nafasi lazima nije kunywa chai, kwani hapa naweza kufanya mazungumzo ya biashara au kuongea na marafiki zangu."

Mikahawa mjini Chengdu ni tofauti na sehemu nyingine nchini China. Mikahawa katika sehemu ya kaskazini ya China huandaa kwa meza ya kimo kirefu ya mraba na vibao vinne virefu pembeni, wanywaji wanakaa wakinyoosha migongo yao kama sanamu, kunywa chai katika mazingira kama hayo inachosha. Lakini mikahawa mjini Chengdu mazingira ni ya starehe. Meza inang'ara kwa kupanguswa mara kwa mara, kiti chenye vishikizo vya kuwekea mikono kina kiegemeo kulingana na mgongo, lakini sio sofa wala kiti cha kulalia ambacho kinamfanya mtu apate usingizi haraka, bali hupati uchovu hata ukikaa siku nzima. Wakazi wa mji wa Chengdu wanapenda kunywa chai katika mikahawa waliyoizoea. Watalii wakiwa na hamu ya kuona mikahawa ya Chengdu ilivyo, ni bora waende kwenye mikahawa iliyopo kando ya bwawa la Dujiangyan ambapo watu ni wengi, mandhari ni nzuri, miti mikubwa, na vyakula vingi vya aina mbalimbali . Wu Qing ambaye ni mmiliki wa mkahawa mmoja wa huko alisema, sifa ya mkahawa wake ni kuwafanya wateja waone starehe kama wako nyumbani kwao. Alisema,

"Tunayo chai maarufu kutoka sehemu tofauti zinazozalisha majani ya chai, wateja wanapokuwa hapa wanaona raha na starehe."

Mikahawa mjini Chengdu inavutia zaidi kwa kuwa na wahudumu hodari ambao watu huwaita "madaktari wa chai". Kwa sababu watu hao wanafanya kazi katika mikahawa kwa miaka mingi na kuwasiliana na watu wa aina mbalimbali, kwa hiyo ujuzi wao ni mwingi na habari walizosikia ni tele, wanywaji huwaita "madaktari wa chai". "Madaktari" hao ni hodari wa kuwatilia wanwaji maji ya moto ndani ya vikombe vyenye majani ya chai. Wakiwa na bilauri kubwa ya shaba yenye mdomo mrefu kama mrija, wanawatilia maji ya moto kwa ufundi mkubwa, maji yanatoka mdomoni na kujaza kikombe kutoka mbali bila maji hayo kumwagika nje ya kikombe hata tone. Kwa bilauri hiyo hata wanaweza kumimina maji ndani ya chupa ya soda kutoka mbali.

Miongoni mwa mikahawa iliyoko Chengdu, Mkahawa Wenxuange unajulikana zaidi. Mkahawa huo ni jumba la ghorofa, ghorofa ya chini ni ukumbi mkubwa uliopambwa kwa mtindo wa zamani wa Kichina. Na ghorofani ni ukumbi uliopambwa kwa mtindo wa Ulaya, michoro ya mafuta ukutani na zulia la buluu sakafuni. Kutokana na mitindo ya aina mbili, watalii wa Ulaya huwa wengi. Bi. Clandia Perle aliyetoka Uswis alisema,

"Kwangu ni mara ya kwanza kuja hapa. Kabla ya hapo niliwahi kwenda katika mikahawa mingine, lakini napenda zaidi mkahawa huu wenye mtindo wa zamani, na mazingira pia yananivutia."

Mabadiliko makubwa yaliyotokea miaka ya karibuni katika mikahawa ni vyombo vya chai. kwa kuwa wafanyabiashara wengi hufanya mazungumzo ya kibiashara katika chumba cha kupangishwa na kutaka kunywa majani ya chai yaliyo maarufu, mikahawa mingi inatumia glasi za fuwele. Majani ya chai yanayokuwa chini ya glasi baada ya kumimina maji ya moto huelea juu na kuonekana kama samaki wengi wadogo wakivuta hewa kwenye uso wa maji, na dakika chache baadaye majani hayo yanaanza kuzama pole pole.

Katika miaka ya karibuni "chai ya Kuding", ambayo ni aina mojawaoi ya majani ya chai mwitu wanayotumia wakulima pia inapendwa na wanywaji. Bi. Han Lin alisema,

"Chai hiyo ni nzuri sana, ladha yake ni chungu kidogo, inasaidia kupunguza uzito na kuyeyusha chakula. Aina za chai hiyo ni nyingi na bei ni tofauti ambayo inawawezesha wateja wa kila ngazi kuimudu."

 Kwa kifupi, mikahawa katika mji huo ni kama jukwaa la mazungumzo. Wakazi wakiwa katika mikahawa wamekuwa kama samaki waliopata maji, kwamba wanaweza kuonesha vya kutosha uhodari wao wa kuongea. Ukiwa na fursa usikose kuhisi mazingira yenyewe ndani ya mikahawa ya huko.

Idhaa ya kiswahili 2006-05-08