Muda wa likizo ya siku ya wafanyakazi duniani ambayo hudhimishwa tarehe mosi Mei, ni siku saba nchini China, siku nyingi kama hizo ni nafasi nzuri kwa wakazi wa Beijing kufanya utalii na kuangalia maonesho ya sanaa ya nchi mbalimbali mjini humo.
Jumba la Sanaa la Beijing liliwahi kufanya maonesho ya mwaka wa utamaduni wa Ufaransa 2003 hadi 2004. Maonesho ya picha dhahania za Ufaransa yaliyofanyika kwa siku 38 katika jumba hilo yalivutia watazamaji zaidi ya laki mbili na nusu, na maonesho ya kufunga mwaka wa utamaduni wa Ufaransa yaliyofanyika katika jumba hilo yalikuwa ya aina saba ambayo yaliwapatia wakazi wa Beijing burudani safi za sanaa tofauti katika majira ya joto. Hivi sasa, maonesho ya " Majira ya Mchipuko ya Ufaransa" yakiwa kama ni sehemu ya maingiliano ya utamaduni kati ya China na Ufaransa yameanza katika jumba hilo. Mkuu wa jumba hilo Bw. Fan Di'an alisema, "Ingawa mwaka wa utamaduni wa China na wa Ufaransa ulidumu kwa miaka mitatu, lakini watu wa nchi hizi mbili wanaona hawajatosheka, kwani China na Ufaransa zote ni nchi zenye utamaduni mkubwa, na haiwezekani kuonesha vya kutosha utamaduni wote katika muda mfupi. Na maonesho ya 'Majira ya Mchipuko ya Ufaransa' yanayofanyika hivi sasa mjini Beijing ni mfululizo wa 'mwaka wa utamaduni wa Ufaransa'."
Miongoni mwa vitu vinavyooneshwa katika maonesho hayo baadhi vinatoka katika Jumba la Sanaa ya Fuwele ya Baccarat na baadhi ni picha zilizohifadhiwa katika Kituo cha Sanaa ya Pompidou ambazo zilipigwa na mpiga picha mashuhuri duniani Pompidou.
Sanaa ya fuwele ya Baccarat imekuwa na historia ya miaka 200, vitu vilivyooneshwa katika maonesho hayo, jumla viko 300, na vingi vinaoneshwa kwa mara ya kwanza nje ya Ufaransa.
Ukumbi wa maonesho ndani ya Jumba la Sanaa la Beijing ulipambwa kama kasri ya fahari, kwamba vitambaa vya shashi vilitundikwa toka darini hadi sakafuni, na chini ya mwangaza wa taa, taa za fuwele za kutundikwa, chupa za mvinyo, mabangili, vinara vya mishumaa na mashua za fuwele zilizopambwa kwa sanamu za malaika wadogo wa rangi ya dhahabu, zinameremeta na kuwafanya watazamaji wahisi kama wako katika dunia nyingine kabisa. Ukumbi mwingine ndani ya jumba hilo ulipambwa kwa mujibu wa mazingira wakati Napoleon Bonaparte na malkia walipowakaribisha kwenye chakula watu maarufu kutoka sehemu mbalimbali duniani. Juu ya meza kubwa, zilining'inia taa mbili zilizotengenezwa miaka 100 iliyopita, na kwenye meza kuna sahani za matunda, vyombo vya mvinyo, sahani za chakula, glasi. Katika mazingira hayo watazamaji wanajikuta kama wamekuwa katika historia ya zamani ya Ufaransa. Mtazamaji Hao Jingyong alisema, "Fuwele iliwahi kuwa ni kitu cha fahari katika maisha ya matajiri nchini Ufaransa. Vitu hivyo vinavyooneshwa katika mazingira halisi ya zamani vinapeleka watazamaji kwenye utamaduni mzito wa siku za zamani nchini Ufaransa."
Katika Jumba la Makumbusho la Taifa lililopo katika uwanja wa Tian An Men pia kuna "maonesho ya johari za wahenga wa Inca". Utamaduni wa ajabu wa Inca nchini Peru barani Amerika ya Kusini ni maarufu duniani. Katika miaka elfu 16 iliyopita binadamu walianza kuishi katika ardhi ya Peru. Baada ya karne nyingi kupita hadi kufikia karne ya 15 na katikati ya karne ya 16 utamaduni wa Inca ulifikia kileleni. Mkuu wa Jumba la Makumbusho la Taifa la Peru Bw. Alvaro Miro alisema, maonesho hayo ni makubwa kabisa barani Asia, na kwa makusudi wataalamu wa vitu vya utamaduni walichagua vitu vingi kote nchini na mwishowe walipata vitu 248, ambavyo vyote ni vya hazina ya taifa. Alisema, "Tunafanya maonesho hayo kwa makusudi ya kuwafahamisha Wachina historia ya kale ya Peru, vitu hivyo vilichaguliwa kwa makini na vinawakilisha halisi hali ya zamani ya Peru ili kuonesha historia ya Peru yenye miaka elfu tano."
Kwa mujibu wa maelezo, miongoni mwa vitu vilivyooneshwa, kitu cha thamani kubwa ni upanga wa Tumi. Upanga huo una umbo la nusu mwezi. Kwenye mpini wa upanga huo kuna sanamu za mtu mmoja mwenye mabawa aliyesimuliwa katika hadithi za kale, na kwenye macho, masikio na mabawa kuna mapambo ya vito. Kingine katika maonesho hayo ni fuvu la kichwa cha mwanamke mmoja, cha ajabu ni kwamba kwenye fuvu hilo kuna vitundu vitano. Mtaalamu mmoja aitwaye Bi. Dra Bertha Vargas alifahamisha kwamba vitundu hivyo vilionesha uhodari wa upasuaji katika utamaduni wa zama za kale za Inca, jambo la kushangaza ni kuwa mgonjwa huyo alipona baada ya upasuaji huo. Kwa mujibu wa kumbukumbu, mgonjwa huyo alifanyiwa upasuaji mara tano, na kila mara alipita salama, hili ni jambo lililotokea miaka mia tano iliyopita.
Katika maonesho hayo pia kuna vitu vya vigae, vya dhahabu na vitambaa, ambavyo vyote vilikuwa ni vitu vya kufanyia kafara. Vitu hivyo vimeonesha hali ilivyokuwa ya kilimo, ufugaji na maisha ya kila siku katika zama za kale za Peru. Bi. Chen Hongdi aliwahi kuishi nchini Peru kwa miaka mingi. Baada ya kuangalia maonesho hayo alisema, "Ingawa nilifanya kazi huko Peru kwa miaka mingi, lakini sikuwahi kuviona vitu hivyo. Nahisi kama nimekuwa tena nchini Peru. Nafurahi."
Katika Jumba la Makumbusho la Beijing yanafanyika maonesho mengine ya "Vitu Adimu Duniani" yaliyofanywa na Jumba la Makumbusho la Uingereza. Vitu 272 vilivyooneshwa katika maonesho hayo vyote ni mara ya kwanza kuoneshwa mjini Beijing. Vitu hivyo vimerikodi historia ya maendeleo ya binadamu tokea miaka milioni mbili iliyopita hadi mwishoni mwa karne ya ishirini, na vilipatikana kutoka Ulaya, Asia, Oceania, Amerika na Afrika, vitu hivyo vikiwa ni pamoja na sanamu, picha za kuchorwa, vito, vyombo vya dhahabu, vyombo vya shaba, vyombo vya mawe na vyombo vya udongo wa mfinyanzi. Kati ya vitu hivyo viko vyombo vya mawe vyenye miaka milioni mbili iliyopita kutoka Tanzania na picha ya "misalaba mitatu" iliyochorwa na mchoraji mkubwa wa Uholanzi, Bw. Rembrandt.
Idhaa ya kiswahili 2006-05-08
|