Kwa uhakika udanganyifu ni tabia mbaya sana. Lakini pia kuna uongo mtakatifu unaoonesha upendo mkubwa. Hivi karibuni katika mji wa Changchun, kaskazini mashariki mwa China, maelfu ya wakazi wa huko walishirikiana kuandaa uongo mtakatifu kwa ajili ya mtoto wa kike mwenye kansa atimize ndoto yake.
Mtoto huyo anaitwa Xin Yue, ana umri wa miaka 8 na anakaa mjini Changchun, mji uliopo kilomita elfu moja kutoka mji mkuu wa China, Beijing. Mwaka jana mtoto huyo alipata ugonjwa wa kansa mbaya ya ubongo, na kutokana na kuzorota kwa hali ya afya yake, amekuwa hawezi kuona na ni vigumu kwake kuzungumza. Daktari aliwaambia wazazi wake kuwa, ikiwa mtoto wao anataka kitu fulani, wakidhi tu mahitaji yake, kwa kuwa maisha yake yanakaribia mwisho.
Xin Yue ana ndoto moja kubwa ya kutazama hafla ya kupandisha bendera ya taifa kwenye uwanja wa Tiananmen mjini Beijing. Lakini daktari alionya kuwa, hali ya afya yake ilikuwa mbaya sana kiasi cha kushindwa kumudu safari ndefu. Kwa hiyo baba wa Xin Yue alitafuta msaada kupitia vyombo vya habari vya huko, akiomba kuandaa hafla ya kupandisha bendera ya taifa inayofanana na ile inayofanyika kila siku mjini Beijing, ili mtoto huyo mlemavu ajione anashuhudia hafla hiyo katika mji mkuu Beijing. Gazeti moja la mji wa Changchun lilichapisha makala ya mwandishi wa habari Bibi Tao Bin, akiwaomba watu wenye huruma wamwandalie mtoto Xin Yue uongo mtakatifu.
Bibi Tao Bin alikumbusha kuwa, makala yake iliwavutia watu wengi mara baada ya kuchapishwa kwake. Anasema, "Jambo nisilotarajia ni kuwa, asubuhi ya siku iliyofuata baada ya kuchapishwa kwa makala yangu tulipokea simu zisizohesabika, ambapo watu walieleza nia ya kushiriki, ambapo watu wa shule moja ambao walipenda kufanya shule yao iwe mahala pa kufanya hafla ya kupandisha bendera ya taifa, na watu wengine walisema wangependa kuwa watazamaji kwenye 'hafla' hiyo."
Asubuhi ya tarehe 22 Machi, teksi moja iliyomchukua mtoto Xin Yue na wazazi wake ilianza safari. Wazazi wake walimwambia mtoto huyo kuwa, walikuwa wanaelekea uwanja wa Tiananmen mjini Beijing. Ili kuepuka kumchosha mtoto, teksi ilikwenda pole pole sana, ambapo Xin Yue alipatwa na usingizi.
Baada ya safari ya saa 3, teksi ilisimama na mtoto Xin Yue aliamka akadhani kuwa amewasili Beijing. Ili kufanya uongo huo uonekane kama jambo la kweli, Xin Yue aliambiwa kuwa, teksi za miji mingine haziruhusiwi kuingia moja kwa moja mjini Beijing, bali inawabidi kupanda basi namba 4 ambalo linasimama katika uwanja wa Tiananmen. Wakati huo huo, lilikuja basi moja lililokuwa limechukua watu waliojitolea kuandaa uongo huo mtakatifu.
Basi hilo lilisimama kwenye kituo, abiria na kondakta ambao wote walikuwa wamejitolea waliongea wakimpa mtoto huyo dalili kuwa, basi hilo linaelekea uwanja wa Tiananmen. Halafu walishirikiana kumsaidia Xin Yue na kiti chake cha magurudumu kupanda basi. Njiani kuelekea uwanja wa Tiananmen, basi hilo lilisimama katika vituo vinne, ambapo kulikuwa na watu waliojitolea ambao walishuka na kupanda basi, baadhi yao waliuliza njia kwa kutumia lafudhi za sehemu tofauti nchini China, na baadhi yao walizungumzia hali ya hewa ya Beijing. Kila kitu kilikuwa kinaendelea kwa taratibu, na kuonekana kuwa, basi hilo linatembea kwenye barabara za Beijing.
Hatimaye basi lilifika kwenye uwanja wa Tiananmen, ambao kweli ulikuwa uwanja wa michezo wa chuo cha mawasiliano cha Changchun. Walimu na wanafunzi wa chuo hicho walikuwa wamemsubiri mtoto Xin Yue na kuwa tayari kupandisha bendera ya taifa. Watu waliojitolea ambao walijipamba kama watalii na wachuuzi walikuwa wakijaribu kuandaa mazingira ya uwanja wa Tiananmen.
Hafla yenyewe ilianza hivi: Askari wa kulinda bendera ya taifa, ambao kweli ni watu waliojitolea walifanya gwaride na kupandisha bendera ya taifa kwa kufuata wimbo wa taifa. Kutokana na mtoto huyo kushindwa kutazama, kulikuwa na watu waliomwelezea mchakato huo.
Mwandishi wa habari Bibi Tao Bin aliyeshuhudia hafla hiyo, alisema "Ilipokaribia wakati wa kupandisha bendera ya taifa, kwa mara ya kwanza nilimwona mtoto Xin Yue akicheka kwa furaha. Halafu alipiga saluti. Ingawa alikuwa hana nguvu kutokana na ugonjwa, alipiga saluti kwa kuinua mkono wake mpaka kukamilika kwa hafla hiyo alishindwa kuushusha, kwa vile mkono ulikuwa umepooza.
Kwa mujibu wa mwandishi huyo wa habari, wakazi wa mji wa Changchun zaidi ya elfu 2 walishiriki kutunga uongo huo mtakatifu, wakiwa na lengo moja tu la kumsaidia mtoto mlemavu ambaye hawamfahamu atimize ndoto yake.
Shughuli hizo za kutunga uongo mtakatifu kwa ajili ya upendo ziliripotiwa na vyombo vingi vya habari, na kuwavutia watu wengi wakiwemo madaktari wa hospitali moja ya magonjwa ya ubongo. Mtoto Xin Yue alipelekwa mjini Beijing na kulazwa katika hospitali hiyo, ambapo wataalamu wa hospitali mbalimbali walimtibu kwa pamoja. Saa 2 na nusu, asubuhi ya tarehe 11 mwezi Aprili, mtoto Xin Yue alifanyiwa upasuaji wa ubongo. Upasuaji huo uliendelea kwa saa karibu 8 kabla ya kukamilika kwake saa 10 alasiri. Daktari wa mtoto huyo Bw. Shi Xiangen alisema upasuaji huo uliendelea vizuri. Alisema, "Kwa ujumla tunaridhika na matokeo ya upasuaji huo. Sasa mgonjwa huyo ana ufahamu, pia anaweza kuchezesha mikono na miguu yake. Hata hivyo inabidi tufuatilie hali yake. Tutafanya kila tuwezalo kumwokoa mtoto huyu."
Daktari huyo aliongeza kuwa, magonjwa mbalimbali bado yanaweza kutokea baada ya upasuaji huo, na kuna nafasi ndogo kwa macho ya mtoto huyo kurejea katika uwezo wake wa kawaida wa kuona.
Watu wengi wanamtakia kila la kheri mtoto Xin Yue, wanatarajia mtoto huyo ataushinda ugonjwa na kuleta mwujiza.
Hivi sasa mtoto Xin Yue anaendelea vizuri. Ingawa bado hajaweza kuona, tarehe 30, Aprili alipelekwa kwenye uwanja wa Tiananmen mjini Beijing na kushuhudia hafla ya kupandisha bendera ya taifa. Na safari hii ni ya kweli.
Idhaa ya kiswahili 2006-05-18
|