Kabla ya rais Hu Jintao wa China kufanya ziara ya kiserikali nchini Kenya mwezi Aprili mwaka huu, waandishi wetu wa habari walioko Kenya walifanya mahojiano na balozi wa China nchini Kenya Bwana Guo Chongli kuhusu uhusiano kati ya China na Kenya.
Balozi Guo alisema, urafiki kati ya China na Kenya ulianzia tangu enzi na dahari. Mwaka 1405 baharia maarufu wa China Bwana Zheng He aliongoza kikosi cha merikebu kusafiri baharini, ambapo walifika pwani ya bahari ya Afrika ya mashariki na kati, kutembelea miji yenye bandari ya Mombasa na Malindi. Tarehe 13 Desemba mwaka 1963, siku mbili tu tangu Kenya ipate uhuru wake ilianzisha uhusiano wa kibalozi na China. Tangu hapo, uhusiano kati ya China na Kenya umeendelea siku hadi siku. Hivi sasa mendeleo ya uhusiano huo yako kwenye kiwango kizuri zaidi katika historia. Balozi Guo alisema:
"Katika miaka ya hivi karibuni, viongozi wa China na Kenya wametembeleana mara kwa mara na kupata mafanikio dhahiri. Mwezi Oktoba mwaka 2004, spika wa bunge la umma la China Bwana Wu Bangguo aliitembelea Kenya, na kabla ya hapo, yaani mwezi Desemba mwaka 2003 naibu spika wa bunge la umma la China Bwana Han Qide alikwenda Kenya kushiriki katika shughuli za kuadhimisha miaka 40 tangu China na Kenya zianzishe uhusiano wa kibalozi."
Tarehe 17 Agosti mwaka jana rais Hu Jintao wa China alipokutana na rais Mwai Kibaki wa Kenya hapa Beijing alisema, kuimarisha uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya China na Kenya ni sehemu muhimu ya sera ya kidiplomasia ya China. China inapenda kushirikiana na nchi za Afrika ikiwemo Kenya katika kuhimiza uhusiano mpya wa kiwenzi uendelezwe kwenye kiwango cha juu zaidi. Mwanzoni mwa mwa mwaka huu serikali ya China ilitoa waraka wa sera ya China kwa Afrika. Balozi Guo alisema:
"Miaka 50 iliyopita, China na Misri zilitangulia kuwekeana uhusiano wa kibalozi, uhusiano wa kibalozi kati ya China na Afrika ulianzishwa kuanzia hapo. Mwezi Januari mwaka huu, serikali ya China ilitoa rasmi Waraka wa sera ya China kwa Afrika. Hii ni mara ya kwanza kwa China kutoa waraka kama huo."
Balozi Guo alisema, katika miaka 50 iliyopita, mabadiliko mengi yalitokea katika hali ya kimataifa na hali ya nchini China na barani Afrika, lakini msingi wa ushirikiano kati ya China na Afrika haubadiliki, pande hizo mbili zina matumaini makubwa ya kuenzi zaidi urafiki wa jadi kati ya China na Afrika katika hali ya historia mpya, ili kupata maendeleo ya pamoja. Aidha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Kenya umeendelea kwa haraka. Balozi Guo alisema:
"Mwaka 2005, thamani ya biashara kati ya China na Kenya ilifikia dola za kimarekani milioni 475, hili ni ongezeko la zaidi ya mara mbili kuliko mwaka 2003."
Tangu China na Kenya zianzishe uhusiano wa kibalozi, serikali ya China ilitoa misaada ya kiuchumi kwa serikali ya Kenya, hii ni misaada isiyo na masharti yoyote, ambayo imeeleza urafiki mkubwa wa serikali ya China na wananchi wake kwa serikali ya Kenya na wananchi wake, ambapo miradi mingi ya utoaji misaada kama vile kuchimba visima, kujenga barabara na hospitali ilisifiwa sana na serikali ya Kenya na wananchi wake. Mwanzoni mwa mwaka huu serikali ya Kenya ilipata mkopo wenye unafuu wa yuan milioni 400 uliotolewa na China katika kufanya ukarabati wa mfumo wa mawasiliano ya habari vijijini na mfumo wa umeme mijini.
Zaidi ya hayo, maingiliano kati ya China na Kenya kwenye sekta za utamaduni na elimu pia yanaongezeka siku hadi siku. Balozi Guo alisema, mwishoni mwa mwaka 2005 chuo cha Confucius kilianzishwa rasmi katika Chuo kikuu cha Nirobi, ambacho ni chuo cha kwanza cha Confucius barani Afrika. Na tarehe 28 Januari mwaka 2006, Kituo cha kwanza cha FM cha Radio China kimataifa kilianzishwa na kutangaza rasmi huko Nairobi Kenya. Balozi Guo alisema:
"Kuanzishwa kwa kituo cha FM cha Radio China Kimataifa huko Nairobi Kenya kumefungua ukurasa mpya kwa maingiliano ya utamaduni kati ya China na Kenya."
Bwana Guo Chongli alisema, kabla ya hapo, kuna vituo vitatu vya nchi za magharibi ambavyo ni shirika la utangazaji la Uingereza BBC, Sauti ya Marekani VOA na Radio Ufaransa vinatangaza nchini Kenya kwa kupitia mitabendi ya FM. Baada ya kituo cha FM cha Radio China Kimataifa kizinduliwe rasmi mjini Nairobi, wasikilizaji wa Nairobi wanaweza kusikiliza sauti kutoka upande wa mashariki, ambapo mji wa Nairobi umekuwa mji unaounganisha utamaduni wa mashariki na utamaduni wa magharibi.
Idhaa ya kiswahili 2006-05-19
|