Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-24 19:15:31    
Mfumo wa makazi ya kisasa wenye uwezo wa kujiendesha ni mtunza nyumba mpya wa wachina

cri

Hivi sasa wachina wengi wameanza kuzingatia kuinua ubora wa maisha yao, wanaona kuwa kujenga nyumba nzuri hakutegemei mapambo mazuri tu. Mfumo wa kisasa wa makazi yenye uwezo wa kujiendesha umekuwa mtunza nyumba mpya wa wachina na kurahisisha maisha ya watu.

Bw. Wang Xiao ni mfanyakazi wa kampuni moja inayoshughulika na biashara ya nyumba, kila siku ana shughuli nyingi. Anatamani kuwa kila siku akirudi nyumbani, akute chakula tayari kimepikwa, maji ya kuoga yawe yameandaliwa, na hata anataka kuwasha kiyoyozi kwa kutuma chombo cha remote kabla ya kufika nyumbani.

"Katika majira ya joto, ni kawaida kutumia kiyoyozi nyumbani, lakini ukiacha kiyoyozi kinafanya kazi siku nzima, gharama za matumizi ya umeme zitakuwa kubwa. Lakini kama tukiwa na uwezo wa kuwasha kiyoyozi kwa tumia simu ya mkononi nusu saa kabla ya kumaliza kazi na kufika nyumbani, basi tukifika nyumbani tayari ndani kutakuwa na hewa baridi."

Hivi sasa matumaini ya Bw. Wang yameweza kutimizwa. Tunatakiwa tu kumpigia simu "mtunza nyumba wa kielektroniki" na kutoa amri kwake, tunapofika nyumbani mambo mengi yanakuwa yameandaliwa. Kwa ufupi ni kuwa, mtunza nyumba huyo ni mfumo wa mtandao wa nyumbani, uliounganishwa na kompyuta na vyombo vyote vya umeme nyumbani. Kama mfumo huo ukiunganishwa kwenye mtandao wa Internet, tutaweza kusimamia na kuendesha vyombo vya umeme nyumbani kwa kutumia simu ya mkononi yenye software husika.

Mfumo huo si kama tu una uwezo wa kuongoza kutoka mbali (remote control), bali pia unaweza kusimamia kwa jumla vyombo mbalimbali vya umeme vikiwemo taa na vyombo vya umeme vya jikoni kwa kupitia chombo kimoja (Central Processor). Kutokana na kuwepo kwa chombo hicho, watu wanaweza kusimamia vyombo vingi vya umeme kwa chombo kimoja tu cha jumla cha kuongozea kutoka mbali. Bw. Qiu Fengxiang anayefanya kazi ya kuweka mfumo huo nyumbani alieleza,

"zamani kama tukitaka kuangalia filamu nyumbani, tulitakiwa kufanya vitendo vingi na kutumia vyombo vingi vya kuongozea kutoka mbali. Lakini hivi sasa kutokana na huduma ya kuandaa mapema ya mfumo huo wa kisasa, tunatakiwa kutumia chombo kimoja tu na vifaa vyote vinaandaliwa na mfumo huo."

Bw. Qiu Fengxiang alisema huduma hiyo ya kuandaa mapema inarahisisha kazi nyingi nyumbani. Kwa mfano wa taa, watu wakitazama filamu, mfumo huo unaweza kupunguza mwangaza wa taa na kuweka mazingira mwafaka ya kutazama filamu; watu wanapoondoka nyumbani, hawana tena haja ya kukagua na kuzima taa mojamoja katika kila chumba, ukitumia huduma ya kuzima taa zote, taa zote zitazimika zenyewe."

Lakini ni vipi mfumo huo unafanya kazi hizo zote? Bw. Qiu alisema, hivi sasa nchini China, mfumo wa kisasa wa makazi yenye uwezo wa kujiendesha una aina mbili. Aina ya kwanza ni ya mfumo uliounganishwa na vyombo vyote vya umeme kwa waya, na aina ya pili ni mfumo wa usimamizi kwa ishara ya kielektroniki bila kutumia waya. Bw. Qiu alieleza,

"vyombo vingi vya umeme kama vile televisheni, havipokei ishara ya mawimbi ya radio RF (Radio Frequency), bali vinapokea tu ishara ya mionzi (Infrared ray). Basi tunaweza kubadilisha ishara ya mawimbi ya radio kuwa ishara ya mionzi kupitia chombo cha usimamizi wa ishara ya mionzi. Aidha ishara hiyo inatakiwa ielekezwe kwenye chombo kinachoongozwa, hivyo tukitaka kuendesha televisheni ni lazima tukielekeze chombo hicho kwenye televisheni. Kama tukitumia chombo cha kuongozea kutoka mbali cha ishara ya mawimbi ya radio, hatuna haja ya kufanya hivyo tena, kwa kuwa si lazima kwa ishara ya mawimbi ya radio kuelekezwa kwenye chombo kinachoongozwa na mawimbi hayo yanaweza kupenya kwenye ukuta."

Mfumo wa kisasa wa makazi yenye uwezo wa kujiendesha si kama tu unarahisisha maisha ya watu, bali pia unaweza kuinua kiwango cha usalama wa makazi. Kampuni ya teknolojia ya Yijia ya Beijing inatoa huduma za kusanifu na kuweka mfumo huo nyumbani. Meneja mauzo wa kampuni hiyo Bw. Shi Song alisema

"mfumo huo unaweza kuinua kiwango cha usalama wa makazi. Kwa mfano, watu wakiondoka nyumbani kwa siku nyingi, mfumo huo unaweza kuwasha televisheni au taa kwa wakati kila siku, na kuifanya nyumba ionekane kama ina watu. Mfumo huo pia una uwezo wa kutishia wezi, kama wezi wakiingia nyumbani, taa zinaweza kuanza kuwaka na kuzima mara moja na vyombo mbalimbali vya umeme vikafunguliwa kwa pamoja ili kuwatishia wezi."

Bw. Shi alieleza kuwa, tukiweka kamera moja nyumbani, wezi wakiingia nyumbani, mfumo huo utafungua kamera na kupiga picha. basi tutaweza kuona mara moja vitendo vya wezi kupitia simu ya mkono au kompyuta, na pia utafunga mlango na kuwaarifu walinzi wa sehemu ya makazi hayo, basi wezi hawezi kukimbia.

Lakini huenda baadhi ya wateja wana wasiwasi kuhusu malipo makubwa ya kuweka mfumo huo nyumbani. Watu husika wamedokeza kuwa, bei ya mfumo huo imegawanyika kwa ngazi tofauti kutokana na uwezo wa mteja. Hivi sasa nchini China, tunaweza kuweka mfumo mmoja wenye uwezo wa kimsingi kwa gharama ya Yuan elfu tano tu.