Maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa shirikisho la wachina waishio nchini Kenya, na shirikisho la kuhimiza muungano wa amani wa China nchini Kenya tarehe 12 mwezi Mei yalifanyika huko Nairobi nchini Kenya. Balozi wa China nchini Kenya Bwana Guo Chongli, naibu mkurugenzi wa ofisi inayoshughulikia wachina waishio nchi za nje ya baraza la serikali la China Bwana Liu Zepeng na wajumbe wa wachina wa makampuni ya China nchini Kenya wapatao zaidi ya 100 walihudhuria maadhimisho hayo.
Balozi Guo Chongli alipotoa risala kwenye mkutano huo alisema, shirikisho la wachina waishio nchini Kenya, na shirikisho la kuhimiza muungano wa amani wa China nchini Kenya yamefanya juhudi kubwa katika kuwahudumia, na kulinda haki na maslahi ya wachina wanaoishi nchini humo, kuhimiza mshikamano wa wachina wanaoishi nchini Kenya na kulinda muungano wa taifa la China. Hivi sasa shughuli za aina mbalimbali nchini China zinaendelea moto moto, na uhusiano kati ya China na Kenya upo katika kipindi kizuri kabisa tangu uhusiano wa kibalozi uanzishwe miaka zaidi ya 40 iliyopita. Balozi huyo pia anatumaini kuwa mashirika ya wachina waishio nchini Kenya yataimarika siku hadi siku na kutoa huduma nzuri zaidi kwa wachina waishio huko, na kuchangia zaidi katika kusukuma mbele uhusiano wa kirafiki kati ya China na Kenya.
Naibu mkurugenzi wa ofisi inayoshughulikia mambo ya wachina waishio nchi za nje ya baraza la serikali la China Bwana Liu Zepeng alisema, shirikisho la wachina waishio nchini Kenya, na shirikisho la kuhimiza muungano wa amani wa China nchini Kenya ni mashirika yaliyoanzishwa mapema zaidi na wachina waishio katika sehemu ya Afrika mashariki. Alitumai kuwa mashirika hayo yataendelea na juhudi zao na kuwa kituo cha kuenzi utamaduni wa China.
Mkuu wa shirikisho la wachina waishio nchini Kenya, na shirikisho la kuhimiza muungano wa amani wa China nchini Kenya Bwana Han Jun alisema, katika mwaka mmoja uliopita tangu shirikisho hilo liundwe, idadi ya wanachama wake inaongezeka siku hadi siku. Kazi muhimu ijayo ya shirikisho hilo itakuwa ni kuimarisha mshikamano na ushirikiano kati ya wachina waishio huko na kulinda haki na maslahi halali ya wachina waishio huko. Alisema ziara aliyofanya rais wa zamani wa China Bwana Jiang Zemin nchini Kenya mwaka 1996 ilihamasisha uwekezaji wa wafanyabiashara wa China nchini Kenya, na ziara ya rais Hu Jintao aliyofanya hivi karibuni nchini Kenya itainua uhusiano kati ya China na Kenya kwenye kiwango kipya.
Bw. Han Jun alisema shirikisho la wachina waishio nchini Kenya liko mbioni kuanzisha shule ya lugha ya Kichina na kituo cha kufundisha Kichina, na kuanzisha klabu ya mashirikisho ya wachina waishio Afrika mashariki, ili kufanya juhudi kubwa zaidi katika kuhimiza urafiki kati ya China na Afrika, na kuimarisha mawasiliano na ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika mashariki katika sekta za uchumi na utamaduni.
Shirikisho la wanafunzi na watu waliosoma China waishio huko Cape town nchini Afrika ya kusini tarehe 6 mwezi Mei lilifanya kongamano la kwanza la kitaaluma.
Konsela wa China mjini Cape town Bwana Si Weiqiang alihudhuria kongamano hilo, na alipotoa risala kwenye ufunguzi alisema, kongamano hilo lina umuhimu mkubwa katika kuhimiza mawasiliano na ushirikiano kati ya wanafunzi na watu waliosoma China waishio mjini Cape town.
Bw. Si Weiqiang alisema katika miaka ya karibuni, wachina wengi baada ya kumaliza masomo yao katika nchi za nje walirudi nchini China na kuchangia maendeleo ya mambo ya sayansi na teknolojia ya China. Serikali ya China inawahimiza wanafunzi wa China wanaosoma katika nchi za nje warudi nchini China ili kulihudumia taifa lao kwa elimu waliyopata kutoka nchi za nje, na kujitahidi kuwawekea mazingira mazuri ya kuanzisha shughuli zao nchini China.
Kwenye kongamano hilo zilisomwa makala 9 za taaluma zenye kiwango cha juu kuhusu tiba na afya, utafiti wa kijiografia, nishati za aina mpya, somo la kemikali ya elektroniki na sayansi ya kompyuta.
Mjini Cape town una vyuo vikuu vinne, hivi sasa wanafunzi 600 wa China wanasoma katika vyuo vikuu hivyo.
Idhaa ya kiswahili 2006-05-26
|