Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-26 21:44:39    
Shughuli za maonesho ya utamaduni wa nchi za Asia na Afrika

cri

Katika wiki ya mwisho ya mwezi Aprili mwaka huu, idara ya lugha za Asia na Afrika katika Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing iliendesha shughuli za maonesho ya utamaduni wa nchi za Asia na Afrika, mambo muhimu ya shughuli hizo yalikuwa ni kuonesha filamu maarufu za nchi hizo, kuandaa tamasha la chakula cha nchi za Asia na Afrika, kufanya maonesho ya vivutio vya utalii na mandhari nzuri ya nchi mbalimbali, mashindano ya wanafunzi wa nchi za nje wanaosoma hapa Beijing kutoa hotuba kwa lugha ya Kichina na maonesho ya michezo ya sanaa ya Asia na Afrika. Shughuli hizo zilikuwa na lengo la kuwaonesha wanafunzi na walimu wa chuo kikuu hicho utamaduni, sanaa, mila na desturi za nchi za Asia na Afrika.

Hilo lilikuwa ni tamasha kubwa la kiutamaduni kuandaliwa na Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing. Kwenye maonesho ya michezo ya sanaa yaliyofanyika usiku wa tarehe 27 mwezi Aprili, naibu katibu mkuu wa kamati ya chama cha kikomunisti kwenye Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing Bwana Cao Wenze alisema:

"Hii ni mara ya pili kwa shughuli za maonesho ya utamaduni wa Asia na Afrika kufanyika kwenye Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing, ambazo zinafuatiliwa sana na wanafunzi na walimu wa chuo kikuu hicho. Shughuli hizo zimehimiza mazungumzo na mawasiliano kati ya ustaarabu wa China na ustaarabu wa nchi mbalimbali za Asia na Afrika, hakika zitawasaidia wanafunzi wa chuo kikuu hicho kufahamu mambo ya siasa, uchumi na utamaduni wa nchi za Asia na Afrika."

 

Idara ya lugha za Asia na Afrika ya Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing ina madarasa 12 ambayo ni pamoja na darasa la lugha ya Kiswahili, lugha ya Kihausa, lugha ya kituruki, lugha ya Srilanka, lugha ya Kiindonesia, lugha ya Kikorea, lugha ya kithai, lugha ya Kimalay. Maonesho ya michezo ya sanaa yalifanyika wakati wa ufungaji wa shughuli za maonesho ya utamaduni wa Asia na Afrika. Kwenye maonesho hayo yaliyofanyika kwa saa mbili na nusu, wanafunzi wa idara ya lugha za Asia na Afrika walikuwa wameonesha michezo 16 ya sanaa, ambayo ni pamoja na maonesho ya mavazi, ngoma na nyimbo za nchi mbalimbali za Asia na Afrika.

Mliosikiliza hivi punde ni wimbo wa Thailand uitwao "Mama", wimbo huo umeeleza mapenzi ya watoto kwa mama yao, na mwangaza wa mishumaa iliyoshikwa na wachezaji wanafunzi imeonesha upendo wa kibinadamu.

 

Darasa la lugha ya Kiswahili lina wanafunzi 24, kati yao wanafunzi 15 walikuwa wameshiriki katika maonesho ya michezo ya sanaa. Waliazima ngoma na kanga kutoka kwa ubalozi wa Tanzania nchini China, na kubuni michezo ya sanaa wao wenyewe.

Cui Chixun alishiriki kwenye maonesho ya michezo miwili ya sanaa. Katika mchezo wa kughani alisimulia uzuri wa nchi za Afrika mashariki zinazozungumza lugha ya Kiswahili. Baada ya kumalizika kwa maonesho hayo alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema:

"Nafurahi sana kushiriki kwenye shughuli hizo, ambazo zimeonesha umaalum wa idara ya lugha za Asia na Afrika kwa wanafunzi na walimu wa chuo kikuu chetu na wanadiplomasia wa nchi za nje nchini China. Naona fahari kubwa."

Maonesho hayo ya michezo ya sanaa yaliungwa mkono na balozi za nchi husika za Asia na Afrika nchini China. Wanadiplomasia na wanafunzi kadhaa wa nchi za nje walioalikwa kutazama maonesho hayo walipongeza sana maonesho hayo maalum. Bi. Mariam kutoka ubalozi wa Tanzania nchini China alisema:

"Maonesho hayo ni mazuri sana, wanafunzi ni hodari kuiga michezo ya sanaa, nafurahi sana."

Idhaa ya kiswahili 2006-05-26