Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-29 14:47:52    
Utafiti wa taaluma ya Kitibet nchini China waendelea haraka

cri

Hivi karibuni watafiti zaidi ya 200 kutoka ndani na nje ya China walikusanyika mjini Beijing kuadhimisha miaka 20 tokea Kituo cha Utafiti wa Taaluma ya Kitibet kiasisiwe. Wataalamu wanaona, hivi sasa utafiti wa taaluma hiyo unaendelea haraka katika maingiliano na utafiti wa taaluma na umetoa mchango katika uchumi na utamaduni wa kabila la Watibet.

Utafiti wa taaluma ya Kitibet ni elimu kuhusu jamii, historia na utamaduni wa kabila la Watibet, utafiti huo ni pamoja na jamii, historia, siasa, uchumi, dini, fasihi, muziki na michezo ya kuigiza, na pia ujenzi, dawa na kalenda.

Kabila la Watibet liko katika sehemu ya kusini magharibi ya China. Mazingira maalumu ya kijiografia ya nyanda za juu za Qinghai-Tibet wanakokaa Watibet yalilea utamaduni wa Kitibet. Mwanzoni mwa karne ya 19 utamaduni wake ulianza kuvutia wataalamu wa Magharibi. Mtaalamu Alexander Csoma de Koros wa Hungari, alianza kujifunza lugha ya Kitibet mwaka 1823 na kutafiti kumbukumbu za Kitibet, na kwa mara ya kwanza alianza kutumia "Taaluma ya Kitibet". Katika karne ya 20, Uingereza, Ufaransa na Marekani zilipambamoto katika ufatiti wa taaluma ya Kitibet na kuifanya taaluma hiyo kuwa ni moja ya elimu duniani.

Tibet iko nchini China, ni maskani ya kufanya utafiti wa taaluma hiyo, ingawa utafiti wake ulichelewa kufanyika ikilinganishwa na nchi za nje lakini maendeleo makubwa yamepatikana kutokana na juhudi kubwa. Mtendaji mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Taaluma ya Kitibet, Bw. Lhakpa Phuntsok alisema, "Hivi sasa, aina zote za utafiti wa taaluma ya Kitibet zimekamilika, na umepata mafanikio makubwa. Vijana wenye elimu ya juu wamekuwa nguvu muhimu katika utafiti huo."

Kwa mujibu wa takwimu, hivi sasa kuna watu 2,000 wanaoshughulikia utafiti wa taaluma hiyo, na kati yao kuna watu wa makabila ya Watibet, Wahan na Wahui, na zimeanzishwa idara kumi kadhaa za utafiti, elimu na uchapishaji katika sehemu za mitaa.

Wataalamu wa taaluma ya Kitibet wanapofanya utafiti pia wanatilia maanani maingiliano na ushirikiano na nchi za nje. Kwenye mkutano wa kuadhimisha miaka 20 ya Kituo cha Utafiti wa Taaluma ya Kitibet waandishi wa habari waliona mtaalamu Fernand Meyer aliyetoka Ufaransa akizungumza na mtendaji mkuu Geleg wa kituo hicho kwa Kiingereza. Bw. Fernand Meyer pia anaweza kuzungumza lugha ya Kitibet na ametafsiri maandishi mengi ya Kitibet kwa Kifaransa. Alisema, "Katika muda wa miaka thelathini hivi iliyopita, wataalamu wa China wamepata maendeleo makubwa katika taaluma ya Kitibet. Wamechapisha vitabu vingi. Naona ni afadhali tuwe na ushirikiano badala ya mawasiliano."

Bw. Geleg atakayeshirikiana na Fernand Meyer katika utafiti alisema, hadi sasa wataalamu wa kituo cha utafiti wa taaluma ya Kitibet zaidi ya 120 wamefanya ziara katika nchi zaidi ya 40 na wameanzisha utaratibu wa mawasiliano. Pamoja na hayo, Kituo cha Utafiti wa Taaluma ya Kitibet kimepokea wataalamu zaidi ya 300 wa nchi za nje kufanya ziara nchini China, na kimetafsiri vitabu vingi vya taaluma vya nchi za nje. Bw. Geleg alisema, "Maingiliano na nchi za nje yanatusaidia kuinua kiwango cha utafiti na pia yanatuwezesha kuwaonesha watu wa nje mafanikio ya utafiti wetu watu wa nje."

Katika historia ndefu ya kabila la Watibet, Watibet wamekuwa na utamaduni mkubwa wa jadi, na utafiti wa taaluma ya Kitibet unasaidia sana kuhifadhi utamaduni huo na kuurithisha. Kwa mfano, "Maelezo kuhusu Mfalme Gesar" ni utenzi mrefu kabisa duniani uliotungwa na watu wa Tibet, na umeenea sana miongoni mwa Watibet kwa kuimbwa. Ili kuuokoa utenzi huo serikali ya China iliorodhesha utenzi huo kwenye miradi mikubwa ya taifa, na imewashirikisha wataalamu wengi kuutafiti na kuuratibu. Mkuu wa Taasisi ya Sayansi ya Jamii Mkoani Tibet Bw. Tsewang Jigme alieleza, hivi sasa kuna wasanii sitini hivi wanaoimba utenzi huo, taasisi ya sayansi ya jamii imerekodi na kuchapisha utenzi huo juzuu 24 kwa lugha ya Kitibet.

Tsewang Jigme aliongeza kusema, pamoja na kuenzi utamaduni wa Kitibet, wataalamu pia wanajitahidi kusaidia uchumi kwa kutoa matokeo ya utafiti wao kuhusu utamaduni wa kisasa wa Tibet, idadi ya watu wanaopitapita mjini Lhasa na ujenzi wa miji midogo na hifadhi ya mazingira, ili uchumi uendeshwe kwa kulingana na hali ilivyo mkoani Tibet.

Idhaa ya kiswahili 2006-05-29