Katika maendeleo ya miaka mingi ya viwanda na biashara nchini China, yaliibuka maduka mengi maarufu. Kati ya maduka hayo ni lile lenye historia ndefu zaidi lililoanzishwa karibu zaidi ya miaka 500 iliyopita. Maduka hayo yamekuwa shahidi wa maendeleo ya viwanda na biashara ya China, na kubahatika kuendelea kuwepo hadi hivi leo. Maduka hayo yalifanya kazi muhimu sana katika uendelezaji wa utamaduni wa China na maingiliano ya kimataifa. Hivi sasa machoni mwa watu wengi, thamani ya maduka hayo maarufu na yenye sifa nzuri, ni kubwa kiasi ambacho ni vigumu kuikadiria. Katika kipindi cha leo tunawafahamisha namna maduka hayo yanavyojiendeleza kuendana na wakati, na kuweza kujitafutia nafasi ya maendeleo katika mageuzi.
Maduka hayo maarufu na yenye sifa nzuri mengi yalianzishwa katika miaka mingi iliyopita. Baada ya kuendelezwa kwa karne moja, na hata kwa karne kadhaa, maduka hayo yamekuwa yakijulikana hapa nchini na hata sehemu nyingine duniani. Katika jamii ya biashara ya kisasa, kitu muhimu kwa maduka hayo maarufu yenye karakana zake, ni kuzalisha bidhaa bora zinazopendwa na yenye wafanyakazi wapya wanaorithi ufundi wa jadi, ambayo inaleta nafasi kubwa ya biashara na mali nyingi. Mtafiti wa taasisi ya utafiti ya uchumi ya chuo cha sayansi ya jamii cha China, Bw. Yang Chun alisema,
"Thamani kubwa ya biashara ya maduka maarufu ni sifa yake, ambayo ni mali isiyoonekana. Umuhimu kwa uchumi wa biashara wa China ni utamaduni wa jadi wa biashara wa China, ambao ni uaminifu na kutekeleza ahadi. Hivi sasa kuendeleza maduka hayo maarufu ni jambo muhimu sana."
Ingawa maduka yenye sifa nzuri ni kama yenye nembo ya dhahabu, lakini nembo hiyo ya dhahabu haikupatikana kirahisi. Hadi hivi leo maduka hayo bado yanapita kwenye njia yenye shida nyingi, ambapo mengi yake yametoweka katika mawimbi makubwa ya uchumi wa soko huria. Takwimu zisizokamilika zinaonesha kuwa, hivi sasa nchini China kuna maduka maarufu yenye karakana zake zaidi ya 5,000, na mengi yake yanakabiliwa tatizo la kutokuwa na uwezo wa kutosha wa uvumbuzi na nguvu duni ya hifadhi ya haki-miliki ya kielimu, na kudidimia kwenye masoko baada ya kupita katika mabadiliko mengi ya utaratibu na ushindani mkali wa uchumi wa soko huria.
Duka la vitambaa vya hariri la Qianxiangyi mjini Beijing lilianzishwa mwaka 1830, na linajulikana sana hapa nchini na hata katika nchi za nje. Katika zaidi ya karne moja iliyopita duka la Qianxiangyi limekuwa likiaminiwa na watu wa sekta mbalimbali za jamii kutokana na kutekeleza kanuni ya kuuza bidhaa bora kwa bei nafuu, na kutowadanganya hata wazee na watoto. Hapo zamani waimbaji mashuhuri wa opera ya Kibeijing Bw. Ye Shengzhang na Bw. Mei Lanfang walikwenda mara kwa mara kwenye duka hilo kununua vitambaa vya hariri. Wakati Duka la Qianxiangyi lilipokuwa na ufanisi mkubwa, lilianzisha matawi 27 katika miji mingi ikiwemo Beijing, Tianjin na Osaka, Japan. Lakini baada ya kupita vipindi vya kuwa na ubia na serikali, uchumi wa kimpango na umilikaji wa hisa, hali yake ya hivi sasa siyo ya kufurahisha sana. Naibu meneja mkuu wa duka la Qianxiangyi Bw. Gao Shenchang alisema,
"Katika kipindi hiki, shughuli za duka zimezorota kidogo. Tulikuwa na wasiwasi kubadilisha njia yetu, tena tuna idadi kubwa ya wafanyakazi. Baada ya kubadilishwa kwa utaratibu huo, wafanyakazi wamekuwa wenye hisa za duka, hata hivyo fedha zetu bado siyo nyingi. Tumebuni mipango yetu, lakini hatua ya maendeleo si kubwa, tena kuna baadhi ya dosari katika shughuli zetu."
Hivi karibuni maduka mengi maarufu yalilazimika kuhama kutoka sehemu ya Qianmen, ambayo ni maarufu kwa biashara katika historia kutokana na marekebisho ya sehemu hiyo. Watu waliopata habari hiyo walimiminikia kwenye duka la Qianxiangyi, na duka lilipata faida kubwa kutokana na wingi wa wateja, lakini jambo hilo halikumfurahisha Bw. Gao Shenchang, ambaye alionekana mwenye mawazo mazito kutokana na kufikiria maendeleo ya siku za baadaye ya duka. Anaona kama duka lao litahamishiwa sehemu nyingine tena, basi baadhi ya wafanyakazi wao watakosa ajira. Licha ya hayo, utoaji kiinua mgongo kwa wafanyakazi wastaafu pia ni tatizo kubwa. Baada ya duka kuhamishwa kutoka sehemu ya zamani, siyo rahisi kupata mahali mwafaka kwa biashara ya duka. Mikataba mingi ya uagizaji vitambaa imetiwa sahihi, kiasi cha fedha zinazolipwa kabla ya kupata vitambaa walivyoagiza ni zaidi ya Yuan milioni 1, tena kama watarejea kwenye sehemu ya zamani baada ya ujenzi wa marekebisho kukamilishwa, duka litakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha.
Hali ya shida ya duka la Qianxiangyi inaonesha sehemu ndogo ya shida zinazoyakabili maduka maarufu ya miaka mingi. Hebu tuangalie hali ya kiwanda cha mikasi cha Wangmazi, ambacho kilianzishwa zaidi ya miaka 352 iliyopita, katika muda mrefu mikasi inayotengenezwa kwenye kiwanda cha Wangmazi ilichukua nusu ya nafasi ya soko hilo kutokana na mikasi ya kiwanda hicho yenye ukali sana. Lakini kutokana na uendeshaji hafifu, kuathiriwa na bidhaa za utapeli na kutoweza kulipa fedha za madeni yaliyofikia muda wake, mwaka 2003 kiwanda hicho kilitangaza kufilisika.
Mtafiti wa taasisi ya utafiti wa uchumi ya chuo cha sayansi ya jamii cha China, Bw. Yang Chunxue anaona kuwa, chanzo muhimu kwa kuzorota kwa maduka na viwanda vingi maarufu ni upungufu wa uwezo wa uvumbuzi, na yaliweza kuanzisha maeneo mapya ya uzalishaji yenye mustakabali mzuri kwa kutumia nembo yao maarufu ya zamani. Anaona kuzorota kwa maduka hayo maarufu ya miaka mingi ni sawasawa na hali ya kuzorota kwa viwanda vya jadi vya serikali. Maduka hayo maarufu ya zamani miaka mingi yanatakiwa kuimarisha uwezo wa uvumbuzi na kurekebisha utaratibu wa uendeshaji, ili yapate nafasi ya kuishi katika ushindani wa masoko ya kisasa. Alisema,
"Maendeleo ya maduka maarufu ya miaka mingi yanategemea jinsi yanavyoendana na hali mpya ya ushindani wa masoko. Maduka maarufu ya miaka mingi yanatakiwa kujifunza uzoefu wa viwanda vya serikali vyenye mafanikio katika mabadiliko ya utaratibu."
Kutokana na kuwa maduka maarufu ya miaka mingi yana thamani kubwa zisizoonekana, hivi sasa serikali ya China na jumuiya zisizo za kiserikali, zinazingatia kuhifadhi na kustawisha maduka maarufu ya miaka mingi, na shughuli hizo zinafanyika kwa juhudi katika sehemu mbalimbali za nchini. Maduka maarufu ya miaka mingi ni sehemu moja muhimu ya mji wa Beijing, ambayo ni mabaki maarufu ya utamaduni na historia duniani. Pamoja na kufanikiwa kwa ombi la kuandaa michezo ya Olimpiki, wazo la kuandaa michezo ya Olimpiki ya utamaduni limekubaliwa na watu wengi, kuokoa na kustawisha maduka maarufu ya miaka mingi ya Beijing kumewekwa kwenye ratiba ya shughuli za idara husika. Tarehe 19 mwezi Mei mwaka 2005, jumuiya ya maduka maarufu ya zamani ya mji wa Hangzhou, sehemu ya pwani ya mashariki mwa China ilitoa mswada wa sheria ya kuhifadhi na kuendeleza maduka maarufu ya miaka mingi ya Hangzhou, ambao ni mswada wa kwanza wa sheria kuhusu hifadhi na uendelezaji wa maduka maarufu ya miaka mingi.
Idhaa ya kiswahili 2006-05-30
|