Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-31 15:46:08    
Mtihani wa kiwango cha lugha ya kichina HSK

cri
Hivi sasa, wanafunzi wengi wa nchi za nje wanaosoma nchini China wanafanya juhudi za kuinua kiwango chao cha lugha ya kichina, ili kufanya maandalizi kwa ajili ya HSK---"Mtihani wa kiwango cha lugha ya kichina" utakaofanyika miezi michache ijayo katika sehemu mbalimbali nchini China. Katika miaka ya hivi karibuni, watu wengi wa nchi za nje wamekuwa wakiufahamu mtihani huo, na baadhi ya watu wanaufahamisha na mtihani wa TOFEL.

Mtihani wa HSK wa lugha ya kichina ni kama mitihani ya TOFEL na GRE ya Marekani, ambao ni kipimo cha kuimudu lugha ya kichina kwa watu wasiotumia kichina. Mtihani huo uko katika ngazi 11, na watu wanaofikia ngazi ya juu zaidi wanaonesha kuwa kiwango chao cha kichina ni cha juu zaidi.

Profesa Wang Lujiang kutoka Chuo Kikuu cha Lugha cha Beijing amekuwa akishughulikia mtihani wa HSK kwa miaka mingi. Alikumbusha kuwa, wakati mtihani huo wa kwanza ulipofanyika nchini China mwaka 1990, wanafunzi walioshiriki kwenye mtihani huo walikuwa 2000 tu, lakini sasa hali imebadilika:

"Kabla ya katikati ya miaka ya 90, watu wengi waliokuwa wakifanya mtihani huo walikuwa wanafunzi waliojifunza lugha ya kichina kwenye vyuo vikuu nchini na nchi za nje, lakini baada ya kuingia karne ya 21, licha ya wanafunzi wa vyuo vikuu, wanafunzi kutoka shule za msingi na sekondari wanaojifunza lugha ya kichina, na watu wanaojifunza kichina wenyewe pia wanashiriki kwenye mtihani huo. Hadi kufikia mwaka 2005, watu laki 5 walioshiriki kwenye mtihani wa HSK."

Bw. Wang Lujiang ameeleza kuwa, hivi sasa mtihani wa HSK unafanyika katika vituo zaidi ya 150 katika nchi na sehemu 34 duniani, ni rahisi kwa watu wanaojifunza kichina kuushiriki kwenye mtihani huo. Kutokana na vyeti vinavyotolewa baada ya kufanya mtihani huo, watu wa nchi za nje wanaweza kutoa maombi ya kusoma katika vyuo mbalimbali nchini China. Watu wanaopata vyeti vya ngazi zaidi ya 3 wanaweza kusoma masomo ya sayansi, teknlojia na kilimo katika vyuo vikuu nchini China, na watu wanaopata vyeti zaidi ya ngazi ya 6 wanaweza kusoma kozi za utamaduni na historia.

Bw. Chris Mutz kutoka Marekani akizungumzia sababu yake ya kushiriki kwenye mtihani ya HSK anasema:

"Nashiriki kwenye mtihani huo kwa sababu nataka kufahamu kiwango changu cha kichina na upungufu wangu. Aidha, huo ni mtihani wa ngazi ya taifa ya China, napaswa kupata cheti cha ngazi ya sita ili kusoma shahada ya pili."

Katika miaka ya hivi karibuni, zaidi ya nusu ya wanafunzi kutoka Japan na Korea ya Kusini wanashiriki kwenye mtihani wa HSK kwa ajili ya kujiandaa kupata ajira nchini China. Bw. Lee Moon Kyu kutoka Korea ya Kusini ni mmoja wa wanafunzi hao. Alimwambia mwandishi wa habari kuwa, cheti cha kiwango cha kichina si kama tu kinaweza kuthibitisha matokeo ya masomo yake nchini China, bali pia kitamsaidia kupata ajira katika siku za usoni:

"Hivi sasa watu wengi wa Korea ya Kusini wanaweza kuzungumza kichina, na mtihani wa HSK ni kipimo muhimu cha lugha ya kichina tunapotoa ombi la kufanya kazi kwenye mashirika ya nchi yetu."

Habari kutoka Idara ya usimamizi wamafunzo ya lugha ya kichina kwa wanafunzi wa nchi za nje zinasema, katika miaka ya hivi karibuni, wanafunzi wanaoshiriki kwenye mtihani wa HSK wamekuwa wakiongezeka kwa asilimia 30 kwa mwaka, hali hiyo inatokana na maendeleo ya kasi ya uchumi wa China na kukuzwa kwa mawasiliano kati ya China na nchi za nje, hali ambayo inahimiza matumizi zaidi ya lugha ya kichina. Takwimu zinaonesha kuwa, wanafunzi wa sekondari kwenye majimbo mengi ya Ujerumani wanapaswa kukufanya mtihani wa kichina, na Idara ya elimu ya Uingereza imeweka utaratibu wa kufundisha lugha ya kichina kwenye shule za sekondari. Aidha, idara ya elimu ya Indonesia inajiandaa kuanzisha somo la kichina katika sekondari zaidi ya 8000 nchini humo ndani ya miaka miwili ijayo.

Ili kuwahimiza wanafunzi wa nchi za nje wajifunze kichina na kufahamu utamaduni wa China, serikali ya China inatoa msaada wa masomo kwa wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi kwenye mtihani wa HSK. Wanafunzi wanaopata msaada huo wanaweza kusoma nchini China bila ya kulipa ada ya masomo na gharama za kujiandikisha kushiriki kwenye mtihani huo na kuishi bwenini, na pia wanapewa posho ya zaidi ya RMB yuan 1000 kwa mwezi.

Wakati idadi ya watu wanaoshiriki kwenye mtihani wa HSK inaongezeka, wanafunzi vilevile wamegundua kuwa mtihani huo hauwezi kukidhi mahitaji ya wanafunzi wote ambao wanatoka nchi na sehemu tofauti. Kuhusu suala hilo, idara zinazohusika za China zinafanya juhudi za kuandaa mitihani tofauti kwa sehemu mbalimbali, zikiwemo Amerika ya Kaskazini, Japan na Korea ya Kusini, pia inapaswa kuandaa mtihani unaotolewa kwa watoto wa wachina wanaoishi katika nchi za nje. Wataalamu wanasema kuwa, mtihani mpya wa HSK utakaofanyika katika siku za usoni utaonesha kihalisi kiwango cha kichina cha wanafunzi.

Habari kuhusu mtihani mpya wa HSK utakaotolewa hivi karibuni inakaribishwa na wanafunzi wanaojifunza kichina. Bw. Lee Moon Kyu anasema, anaamini kuwa mtihani wa HSK unaotolewa kwa wanafunzi wa Korea wa Kusini utamsaidia afahamu zaidi upungufu wake na kuweza kufanya juhudi ili kuuondoa upungufu huo.

"Ni tofauti kwa watu wanaotoka Ulaya na Marekani na Korea ya Kusini kujifunza kichina. Watu wa Korea ya Kusini vilevile wanatumia maandiko yanayofanana kidogo na kichina, hivyo ni rahisi kwetu kujifunza kuandika kuliko watu wanaotoka nchi za magharibi. Ndiyo maana mtihani wa HSK unatolewa kutokana na tofauti ya sehemu mbalimbali utawanufaisha zaidi wanafunzi."

Aidha, China inajiandaa kuweka mitihani ya HSK ya biashara, utalii na wasaidizi, mitihani hiyo ni migumu zaidi kuliko mtihani wa sasa wa HSK. Bibi Li Xiaoqi anayeshughulikia mtihani wa biashara wa HSK anasema, mtihani huo uko katika ngazi 5. Bibi Li anasema:

"Mtu akipitia tu ngazi ya chini ya mtihani huo bado anakuwa hana uwezo wa kushughulikia kazi ya biashara kwa kutumia kichina, na akipata kiwango cha juu anathibitishwa kuwa anaweza kushughulikia biashara kwa kutumia lugha ya kichina sanifu. Mtihani huo unafanyika ndani ya dakika 150, ambao ni pamoja na uwezo wa kusikiliza, kusoma, kuandika makala na kuzungumza. Wanafunzi wanaopitia ngazi ya tatu ya HSK wanafaa kushiriki kwenye mtihani huo."

Je, mnajifunza kichina au mna mpango huo? Je, Kama kipindi hiki kimeongeza hamu yenu na kumhimiza muanze kufahamu na kupenda lugha ya kichina? Mkitaka kufahamu zaidi mambo kuhusu mtihani huo, mnaweza kutembelea tovuti kwenye mtandao wa Internet, anwani ni www. hsk.org.cn.

Idhaa ya Kiswahili 2006-05-31