Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-05 10:45:11    
Mwongozaji wa michezo ya kuigiza televisheni, mkulima Zhou Yuanqiang

cri

 

Yuanqiang ni mmoja wa wakulima milioni 900 wa China. Miaka 13 iliyopita aliongoza wakulima wenzake kuhariri na kutengeneza mchezo wa kuigiza televisheni kwa kamera yake ya video. Furaha yake ya kupiga picha za michezo ya kuigiza televisheni ilikuwa ikiongezeka kadiri kila anapomaliza mchezo mmoja. Hivi sasa jina lake linajulikana sana na hadithi yake imetengenezwa kuwa filamu iitwayo "Kujipatia Furaha".

Bw. Zhou Yuanqiang ni mkuu wa kituo cha utamaduni katika kijiji cha Jingcheng mkoani Jiangxi, mwaka huu ametimiza miaka 51, ana kimo cha kawaida na mwembamba. Bw. Zhou Yuanqiang anaonekana ni mkulima wa kawaida kabisa, lakini machoni mwa wakulima wa kijiji chake yeye ni mwongozaji mkubwa wa michezo ya kuigiza televisheni, na majirani wengi wanaomba nafasi za uigizaji katika michezo yake. Hadi sasa Zhou Yuanqiang amemaliza michezo yake 27 ya televisheni, miongoni mwa wakulima wenzake 1,400 wa kijiji chake, 1,300 waliwahi kuigiza katika michezo yake. Hivi sasa, watu wengi wakiwemo watu wa nchi za nje mara kwa mara wanampigia simu au kumwandikia barua wakiomba nafasi za uigizaji katika michezo yake. Tofauti na michezo yote mingine, watu wanaoigiza kwenye michezo ya kuigiza ya Zhou Yuanqiang wote ni watu wa kawaida na hawalipwi chochote kutokana na uchezaji wao. Bw. Zhou Yuanqiang alisema, "Hatuna waigizaji wa kulipwa, wanaoshiriki kwenye maigizo hawalipwi chochote lakini wanaotaka kujiunga na michezo ni wengi sana, dhamira yao sio kwa ajili ya pesa bali kwa ajili ya kujiburudisha, na furaha yao inazidi kuwa kubwa kadiri wanavyoendelea kuigiza zaidi."

Lakini mwanzoni Zhou Yuanqiang alipokuwa na nia ya kupiga picha za michezo ya kuigiza televisheni, wakulima wenzake hawakuwa na wachangamfu kama hivi sasa, walisema hawajawahi kusikia wakulima wanajipigia wenyewe picha za michezo ya kuigiza televisheni. Lakini kwa nini Bw. Zhou Yuanqiang alijiwa ghafla na fikra hizo za ajabu? Alipohojiwa na waandishi wa habari Zhou Yuangqiang alizungumzia mambo ya miaka 30 iliyopita.

Mwaka 1971, Zhou Yuanqiang alipokuwa na miaka 16, siku moja alipofanya kazi shambani aliona kurasa kadhaa za picha za hadithi za watoto. Wakati huo uchumi wa China ulikuwa bado mbaya, maisha ya kiutamaduni yalikuwa duni, na picha za kueleza hadithi zilikuwa hazionekani vijijini. Wakulima zaidi ya kumi walijitahhidi kuangalia picha hizo zilizochanika, aliguswa sana na jinsi wakulima wenzake walivyokuwa na furaha ya kuangalia picha hizo. Zhou Yuanqiang alisema, "Kutokana na hali hiyo, nilitumia pesa nilizolimbikiza kwa zaidi ya mwaka mmoja yuan thelathini nikanunua vitabu 65, karata kadhaa na chesi, na kuanzisha kituo cha utamaduni kijijini."

 

Ni sawa kusema kwamba, Zhou Yuanqiang ni mtu mwenye fikra za kutangulia kuliko wengine. Mwaka 1984, China ilipokuwa ikiendelea na mageuzi, alipata mkopo kutoka benki, alinunua kamera ya video, na televisheni ya rangi, hali yake kama hiyo ilikuwa ya kisasa katika vijiji hata si mbaya katika miji. Wanakijiji walishangaa walipoona televisheni ya rangi, watu walisongamana kituoni. Mwaka 1991, kwa mara ya pili Zhou Yuanqiang alipata tena mkopo kutoka benki, alinunua kamera ya video, ambayo pia ni kitu cha ajabu vijijjini wakati huo. Mwanzoni alitumia kamera hiyo kurekodi tu sherehe fulani za wanakijiji wake hadi siku moja ambapo alipata wazo la kupiga picha za mchezo wa kuigiza televisheni kutoka kwa mzee mmoja. Alisema, "Siku moja nilimpelekea mzee mmoja kitabu, mzee huyo alinishauri, sehemu yetu ilikuwa ni kituo cha mapinduzi katika miaka ya vita vya ukombozi wa China, watu wengi walikufa kwa ajili ya ukombozi wa taifa. Alisema, itakuwa ni jambo la maana kama kituo cha utamaduni kikiwajulisha kwa wenyeji. Na wazo jingine nililopata kutoka kwa mzee huyo ni kuwa sisi tunaangalia michezo inayoigizwa na wengine tu katika filamu na michezo ya kuigiza televisheni, lakini kwa nini tusiweze kuangalia michezo tunayoiigiza sisi wenyewe?"

Mwaka 1992 Zhou Yuanqiang alitumia fedha zote alizokuwa nazo aliwaalika wakulima kadhaa waliothubutu kuwa waigizaji, akaanza kupiga picha za mchezo wa televisheni kwa mara ya kwanza maishani mwake. Hadithi ya mchezo huo ilitungwa na wao wenyewe kwa kushauriana. Mchezo wa kuigiza kwanza waliohariri na kuchezwa na wakulima wenyewe ulimalizika mwaka 1993, jina la mchezo huo ni "Cheche za Moto katika Kijiji Chetu".

Mchezo huo ulipooneshwa watu wa kijiji kizima walifurahi. Uwanja ulioweza kukaliwa watu sitini hivi walijazana watu zaidi ya mia mbili. Mchezo kuigiza "Cheche za Moto katika Kijiji Chetu" unaeleza hadithi iliyotokea katika kijiji chetu katika miaka ya kupigania ukombozi. Watazamaji walifurahi sana walipoona waigizaji ndani ya mchezo huo ni watu wanaoishi nao kila siku, Fulani alipiga kelele akisema, "Unaona, huyu ni baba yako!" na "Tizama, mjomba wako anaiga mtu mbaya!"

Furaha ya wakulima ni ilimtia sana moyo, tokea hapo Zhou Yuanqiang alishikwa na shauku kubwa, alipiga picha za mchezo mmoja baada ya mwingine, na umekuwa mrefu kuliko uliotangulia. Watu walioshiriki kwenye michezo yake wamefikia elfu ishirini, na uigizaji wao umekuwa bora kadiri wanavyozidi kuigiza.

Ni kweli kwamba kijiji chochote alichokwenda kinachangamka kama kilivyokuwa katika sherehe fulani. Lakini hawakujua kwamba kazi yake inakabiliwa na matatizo mengi. Tatizo kubwa ni uhaba wa fedha. Kwa kawaida, mchezo wa kuigiza televisheni hugharimu yuan laki kadhaa katika matengenezo yake, ingawa yeye anatumia yuan elfu kadhaa tu kwa kila mchezo, hata hivyo, pia ni gharama kubwa kwake, kwa hiyo mara nyingine mchezo mmoja huachwa njiani mara kadhaa na unatumia hata miaka mitatu hadi minne kuukamilisha. Ili kupunguza uhaba wa fedha mara nyingi alitumia fedha za mtoto na mkewe walizopata katika kazi za kibarua mbali na nyumbani, na pia alitumia wakati mwingi kukamilisha mchezo wake kabla ya kuoneshwa. Nguvu iliyomsukuma aendelee ni furaha ya wakulima wenzake walipoangalia mchezo wake kuigiza.

Baada ya mambo yake kutangazwa na vyombo vya habari, Zhou Yuanqiang amekuwa mtu mashuhuri, waandishi wa habari wa ndani na nje ya China wanakwenda kuzungumza naye. Kwa mujibu wa hadithi yake, filamu iitwayo "Kujipatia Furaha" iliyochezwa na waigizaji mashuhuri ilitengenezwa, chuo kikuu cha tamthilia kilimwalika kufanya mihadhara. Lakini Zhou Yuanqiang alisema kwa unyenyekevu, "Kwa kweli niko mbali sana na waongozaji wakubwa wa filamu, hata sistahili kulinganishwa nao. Dhamira yangu ni kuboresha tu maisha ya utamaduni vijijini, na kuwafurahisha wakulima wenzangu."

Idhaa ya Kiswahili 2006-06-05