Katika miaka ya hivi karibuni, jamii ya China inaendelea kwa haraka, ambapo harusi za Wachina pia zinabadilika na kuwa za aina mbalimbali. Kuna maharusi ambao wamejipangia harusi maalumu, ili kujiwekea kumbukumbu zisizosahaulika na pia kuwavutia wageni wanaoalikwa kuhudhuria harusi zao.
Hivi karibuni mwandishi wetu wa habari alialikwa kuhudhuria harusi ya rafiki yake iliyofanyika katika hoteli moja ya ngazi ya nyota tano hapa mjini Beijing. Tafrija ilipoanza, kwanza ilioneshwa video kuhusu maharusi walivyotembea katika pwani, ambapo picha ni nzuri na milio ya mawimbi baharini inasikika, wageni waliweza kuhisia jinsi maharusi wanavyopendana. Baadaye mishumaa mbalimbali iliwashwa ukumbini, maharusi hao walifunga ndoa kwenye mwangaza wa mishumaa.
Harusi hiyo ilimpa mwandishi wetu wa habari kumbukumbu nzuri.
Mkuu wa Shirika la shughuli za harusi la China Bw. Shi Kangning alipohojiwa alisema hivi sasa vijana wanazingatia zaidi maana ya harusi badala ya vitu halisi kwenye maandalizi ya harusi, kama vile chakula na magari ya kuwapokea bibi harusi. Alisema
"Hivi sasa watu wanazingatia zaidi umuhimu wa harusi. Kwa mfano, wameanza kufikiria kwa makini mitindo ya harusi, ama iwe ya kijadi, ama ifanyike kanisani, au iwe ya kisasa."
Kumbe kuna harusi za aina mbalimbali, kwa mfano harusi ya angani, harusi inayofanyika baharini, harusi ya mtandao wa Internet na kadhalika.
Hivi karibuni, huko Qingdao, mji wa pwani uliopo mashariki ya China, vijana wawili walifunga ndoa baharini.
Harusi hiyo ilifanyika katika bustani ya bahari ya Qingdao. Bwana harusi Wu Wei na bibi harusi Lin Teng, wakivalia nguo maalumu ya kupiga mbizi walizama kwenye maji, ambapo walishikana mikono, wakakumbatiana na kuinamishana miili yao. Harusi hiyo iliyokamilishwa katika dakika 16 ni fupi na ya kusisimua.
Katika harusi ya namna hiyo, inabidi maharusi wawe hodari katika kupiga mbizi, kwa hiyo vijana wanaoweza kufunga ndoa kwa njia hiyo ni wachache. Baada ya kukamilika kwa harusi hiyo, bibi harusi Lin Teng alimwambia mwandishi wa habari akisema,
"Mimi na Wu Wei tulikua kando ya bahari, sisi sote tunapenda kupiga mbizi na kuogelea, tunapenda sana bahari. Kwa hiyo tuliamua kufunga ndoa baharini, hayo ni matakwa yetu ya pamoja na inaweza kuzuia matumizi ovyo kwenye harusi. Jambo muhimu la kwanza ni muda mfupi wa dakika 16 tu umeweka rekodi daima katika maisha yetu."
Kulingana na harusi ya baharini, ni rahisi zaidi kufanya harusi kwenye mtandao wa Internet. Katika miji kadhaa ya kusini mwa China, harusi ya aina hiyo inawavutia vijana wengi wanaofanya kazi ofisini. Katika harusi inayofanyika kwenye mtandao wa Internet, hakuna chakula wala kupokea zawadi kutoka kwa wageni, badala yake maharusi wanaanzisha tovuti ya harusi. Wageni wakitumia mouse, wanaweza kuangalia picha mbalimbali za maharusi na video yao.
Bw. Wang Chen ni mdau wa sekta ya upashanaji habari. Alianzisha tovuti yake binafsi miaka kadhaa iliyopita. Hivi majuzi, yeye na mchumba wake walikubaliana kufanya harusi kwenye mtandao wa Internet. Alisema,
"Mimi na mke wangu tulihamia mjini Guangzhou kwa ajili ya kazi, kwa hiyo jamaa zetu wengi hawapo mjini humo. Tukiwaalika waje kuhudhuria harusi yetu huko Guangzhou, itakuwa ni vigumu kutafuta wakati na mahali panapofaa. Lakini kwa kupitia tovuti yetu ya harusi, jamaa zetu wanaweza kushuhudia utamu na mapenzi yetu."
Tovuti hiyo ya harusi inafungamana na tovuti binafsi ya Bw. Wang. Maharusi wenyewe walisanifu tovuti hiyo ya harusi, ambayo ina sehemu mbalimbali kama vile, "picha za maharusi", "safari ya fungate", na "maelezo yetu". Kwa kupitia sehemu hizo, jamaa wanafahamishwa jinsi maharusi walivyokutana mara ya kwanza na jinsi walivyopendana. Bwana harusi Wang Chen alieleza kuwa, kwa gharama kati ya Yuan 300 na Yuan 500 tu, watu wanaweza kuomba kusajili anuani ya tovuti moja, na kusanifu tovuti yenyewe.
Harusi inayofanyika kwenye mtandao wa Internet ni ya kisasa kweli, lakini inaonekana sio rasmi. Kwa hiyo licha ya kufanya harusi kwenye mtandao, maharusi wengi pia wanaandaa sherehe ya harusi.
Bibi harusi mtarajiwa Bibi Chen Zhizhi alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, ameshapanga tarehe ya kufanya harusi, pia ataonesha video ya harusi yenyewe kwenye tovuti yake ya harusi.
Kutokana na kuibuka kwa harusi mbalimbali za aina mpya, kampuni za kutoa huduma za harusi pia zimepanua huduma zao. Mbali na huduma za kawaida za harusi, pia kampuni hizo zinaweza kupanga harusi maalumu kutokana na matakwa ya maharusi. Katika miji mingi, kampuni hizo zina biashara nzuri.
Wataalamu wanachambua kuwa, kuibuka na kuenea kwa harusi za aina maalumu kunaonesha kuwa, watu wa China wanazingatia zaidi sifa ya ndoa. Hivi sasa watu wamekuwa na uwezo, wanataka kufanya harusi isiyo kawaida ili maharusi wawe na mwanzo mzuri katika maisha ya ndoa. Na mabadiliko hayo pia ni ishara ya maendeleo ya jamii ya China.
Profesa Wang Zhenyu kutoka Taasisi ya sayansi ya jamii ya China amefuatilia na kufanya utafiti wa harusi za Wachina kwa miaka mingi. Alisema
"Kuwepo kwa aina mbalimbali za harusi ni ishara ya enzi yetu ambapo jamii ya jadi inabadilika kuelekea kuwa jamii ya kisasa. Harusi ni sherehe na jambo linalojionesha hadharani, kwa hiyo mabadiliko ya harusi ni ishara dhahiri ya mabadiliko ya jamii yetu."
|