Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-20 15:34:01    
Kuna "mlima wa dhahabu" kusini mwa Shanghai

cri

Jinshan ni sehemu iliyopo kwenye kiunga cha mbali, kusini mwa Shanghai, ambao ndio mji wa kwanza kwa shughuli za viwanda na biashara nchini China. Katika lugha ya kichina jinshan ni mlima wa dhahabu. Lakini katika muda mrefu uliopita kiwango cha maendeleo ya uchumi wa Jinshan kiko nyuma sana kikilinganishwa na sehemu nyingine za Shanghai, hata kiko chini ya wastani wa kiwango cha sehemu ya mashariki ya China. Lakini hali ya namna hiyo imepata mabadiliko katika miaka ya karibuni, ambapo ustawi unaonekana kwenye sehemu hiyo ya vijijini.

Tokea muda mrefu uliopita, pato la wakazi wa sehemu ya Jinshan lilikuwa dogo sana kutokana kwamba kilimo kilikuwa ndio shughuli muhimu zaidi ya kiuchumi katika eneo hilo. Hali ya familia ya mkulima Song Jie ilikuwa duni pia. Bw. Song Jie alimwambia mwandishi wetu wa habari, hapo zamani alisumbuliwa na wazo zito la kutafuta fedha ya kusaidia matumizi ya familia yake, lakini sasa ameondokana na usumbufu huo, kwani maisha ya wanakijiji wa kijiji chake yamekuwa mazuri mwaka hadi mwaka.

"Hapo awali, wanakijiji wengi waliishi katika nyumba rahisi za kawaida, lakini hivi sasa wanaishi katika maghorofa. Mbali na hayo, mawasiliano ya barabara yamekuwa mepesi sana, ambapo barabara za lami zinafikia nyumba za wanakijiji. Hivi sasa vijiji vyote vimejenga vyumba vya burudani vya wazee, zahanati na vyumba vya mazoezi ya mwili, na wanavijiji wanapata huduma hizo palepale vijijini mwao."

Mabadiliko hayo ni maendeleo makubwa kwa sehemu ya Jinshan, ambayo eneo lake ni kilomita 580 na yenye idadi ya watu ni laki 8 tu, katika muda wa miaka mitatu, Jinshan imebadilika kuwa mahali pazuri kwa uwekezaji vitega-uchumi na kufikia hatua ya mwanzo ya kuwa mji mdogo wenye viwanda kutoka hali yake ya zamani ya kushughulikia uzalishaji mazao ya kilimo peke yake. Ofisa husika wa serikali ya huko Bw. Liu Zhengxian alisema,

"Mwaka jana, pato la sehemu ya jinshan kutokana na uzalishaji wa viwanda lilikuwa Yuan bilioni zaidi ya 61, na wastani wa ongezeko la pato la Jinshan ulikuwa 33.8% kwa mwaka katika miaka 5 iliyopita. Mfumo wa uzalishaji wenye shughuli muhimu za kemikali, madawa, mitambo, elektroniki, nguo, magari na vipuri vya magari umeundwa kwa jumla. Hivi sasa ujenzi wa mji wa Jinshan umefikia kiwango cha zaidi ya 55%."

Mbona viwanda vya huko vinaweza kuwa na maendeleo ya kasi namna hiyo? Nikitaka kukueleza suala hilo, sina budi kukufahamisha shughuli za viwanda vya kemikali vya Jinshan.

Hata katika mwaka 1979, mji wa Shanghai ulianza kujenga kampuni ya kemikali ya usafishaji wa mafuta ya asili ya petroli, ambayo ilikuwa moja ya kampuni na viwanda vichache vikubwa katika sehemu ya Jinshan. Katika miaka ya karibuni, serikali ya huko imeona umuhimu wa viwanda vya kemikali kwa maendeleo ya uchumi wa jinshan, hivyo iliamua kuweka kipaumbele kwa uzalishaji mali wa sekta ya kemikali yenye nyongeza kubwa ya faida vikiwemo viwanda vya kemikali vinavyohusika na utengenezaji wa madawa, nguo na kazi nyepesi za viwanda.

Kwa kufuata mpango uliowekwa, ifikapo mwaka 2010, Jinshan itakuwa na eneo la uzalishaji mali wa kikemikali lenye kilomita za mraba 60, mafuta yaliyosafishwa na ethene utafikia tani milioni 30 na milioni 4. Aidha, Jinshan itaharakisha ujenzi wa vituo vya usambazaji bidhaa za kemikali na miradi ya utoaji huduma. Hivi sasa, taasisi ya utafiti wa kazi za kemikali ya Shanghai, kampuni ya Henkel ya Ujerumani, kampuni ya APATURE ya Marekani na kampuni ya cinnamene ya Shanghai zimewekeza katika sekta ya kemikali ya Jinshan.

Hata hivyo, maendeleo ya kasi ya viwanda vya kemikali hayakuwa chanzo pekee kilicholeta mabadiliko makubwa kwenye sehemu ya Jinshan. Mwaka 2003, Jinshan iliweka mpango wa kujenga eneo la viwanda vya teknolojia ya kisasa, na kujitahidi kuendeleza sekta za mawasiliano ya habari ya elektroniki, utengenezaji wa mitambo, madawa na aina mpya ya vifaa vya ujenzi. Serikali ya Jinshan inatarajia kuhimiza maendeleo ya uchumi kwa kutumia nafasi hiyo.

Mkurugenzi wa kamati ya usimamizi ya eneo la viwanda la Jinshan Bw. Sun Yinliang alipomweleza mwandishi wetu wa habari kuhusu umaalumu wa eneo hilo la viwanda, alisema,

"Eneo letu hilo lilisanifiwa kwa kufuata mambo ya kisasa, yenye umaalumu wa kwetu hapa na uendelezaji wa mazingira ya kutegemeana kwa viumbe. Kwa kawaida, kila eneo la viwanda hujenga nyumba za kuishi karibu na karakana za viwanda, lakini eneo letu lilijenga vituo 8 vya huduma, na kila kituo cha huduma kinaweza kuwahudumia wafanyakazi wanaoishi kwenye eneo la kilomita 5. Wafanyakazi hao wanaishi pamoja wanapata huduma za mapumziko, burudani, chakula na maduka. Hivyo tunaweza kudhibiti matumizi ya rasilimali na kupunguza gharama za makampuni na viwanda. Hiyo ni sifa kubwa sana ya mpango wetu."

Bw. Sun Yinliang alisema, tangu kujengwa eneo la viwanda la Jinshan, serikali ya huko imetenga fedha zaidi ya Yuan bilioni 1 katika ujenzi wa miundo-mbinu ya mawasiliano, upashanaji habari, maji na nishati, hatua ambayo imeongeza nguvu ya ushawishi ya eneo hilo na kutoa huduma bora kwa makampuni na viwanda vilivyowekeza katika eneo hilo. Hadi hivi sasa, eneo la viwanda la Jinshan limekamilisha 20% ya ujenzi wake.

Kitu kinachofurahisha ni kuwa wakati viwanda vinapopata maendeleo ya kasi, Jinshan haikuharibu mazingira na rasilimali zake. Ofisa husika wa serikali ya Jinshan Bw. Liu Zhengxian alisema, idara husika zinajitahidi kudhibiti uchafuzi wa mazingira ili kuwa na maendeleo endelevu ua uchumi na jamii. Aliongeza, "Jinshan inatekeleza 'mpango wa vitendo wa miaka 3' wa hifadhi ya mazingira ya asili, imejenga vituo vya upimaji wa ubora wa hewa, imerekebisha maboila yanayotumia nishati ya makaa ya mawe ya viwanda 39, upandaji miti kwa wingi, kuendeleza misitu inayotunza rasilimali ya maji na misitu ya kiuchumi hekta zaidi ya 1,000 na kurekebisha mito 7 muhimu. Baada ya kuchukua hatua hizo, anga ya Jinshan imekuwa ya rangi ya buluu zaidi, ardhi kuwa na miti na majani mengi zaidi na maji yamekuwa safi zaidi."

Mbali na hayo, Jinshan inafuatilia maendeleo ya uchumi wa utalii kwa kutumia ubora wake wa kuwa karibu sana na bahari, Jinshan imejenga pwani yenye mandhari nzuri, michezo ya mazoezi ya mwili, maonesho ya biashara na usambazaji wa bidhaa. Tokea mwaka 2004, Jinshan imefanikiwa kwa miaka miwili mfululizo kuendesha mechi za mpira wa wavu za nchini China na mashindano ya mpira wa wavu ya ufukwe duniani, jambo ambalo limeongeza sifa za Jinshan. Takwimu inaonesha kuwa pato la Jinshan la mwaka jana kutokana na mambo ya utalii lilifikia Yuan za Renminbi milioni 250, kupokea watalii zaidi ya laki 4 na elfu 50 na kuweka rekodi mpya ya pato la utalii. Wakazi wa Jinshan wanaona kuwa mabadiliko makubwa yaliyotokea kwao katika miaka ya karibuni ni hatua ya mwanzo tu. Wanaamini kuwa kadiri mpango wao wa maendeleo unavyotekelezwa, Jinshan itakuwa sehemu inayofuatiliwa na watu wa Shanghai hata watu wa China nzima katika uwekezaji.

Idhaa ya kiswahili 2006-06-20