Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-20 18:58:18    
Uhusiano kati ya China na Afrika waingia katika kipindi kipya

cri

Mwaka huu ni mwaka 50 tangu China na Afrika zianzishe uhusiano wa kibalozi. Je, urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika umeendelea vipi katika miaka hiyo 50? Ushirikiano wa namna hii umewaletea wananchi wa pande hizo mbili manufaa gani? Na ziara ya waziri mkuu Wen Jibao wa China katika nchi 7 barani Afrika aliyoianza tarehe 17 mwezi huu, itaboresha vipi uhusiano huo? Mtaalamu wa masuala ya Afrika Bw. Wang Hongyi alitoa maoni yake alipohojiwa na Radio China Kimataifa hivi majuzi.

Bw. Wang alisema katika miaka 50 iliyopita, uhusiano kati ya China na Afrika umefikia kilele mara mbili katika ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi. Na hivi sasa uhusiano huo umeingia katika kipindi kipya. Anasema, "Kilele cha kwanza kilikuwa kati ya miaka ya 50 na 60, ambapo Waafrika walipokuwa wanapigania uhuru. China na Afrika zilishirikiana kwa karibu katika mambo ya kisiasa. Baada ya China kutekeleza sera ya mageuzi na mlango wazi, shughuli za kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika zilikuwa zinaelekea kuimarika, na kufikia kilele cha ushirikiano wa kiuchumi. Tangu mwanzoni mwa mwaka huu China ilipotangaza taarifa ya sera yake kwa Afrika, waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Li Zhaoxing, rais Hu Jintao waliizuru Afrika kwa nyakati tofauti. Na safari hii ni ziara ya waziri mkuu Wen Jiabao. Mbali na hayo, mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano wa China na Afrika utafanyika mwaka huu. Hiyo ni ishara kuwa China na Afrika zimeshaingia kipindi cha ushirikiano wa sekta zote."

Mafanikio yamepatikana katika sekta mbalimbali za ushirikiano wa China na Afrika. Kwa mfano wa shughuli za uchumi na biashara, thamani ya biashara kati ya pande hizo mbili imeongezeka sana na kukaribia dola za kimarekani bilioni 40 kutoka dola milioni 12 za kimarekani hapo awali.

Mtaalamu huyo Wang Hongyi alieleza maoni yake kuwa, maoni na maslahi ya pamoja kati ya China na Afrika ni msingi wa ushirikiano huo, na pande mbili zote zina nia ya kuimarisha ushirikiano huo. Anasema, "Nchi za Afrika na China zote ni nchi zinazoendelea, zina historia zinazofanana, na kukabiliwa na masuala yanayofanana, ambayo ni kulinda muungano na maendeleo ya taifa, kuboresha maisha ya wananchi na kupunguza pengo la maendeleo na nchi zilizoendelea. Kwa upande wa mambo ya kisiasa, China na Afrika zinashirikiana katika kulinda maslahi ya nchi zinazoendelea, na kujitafutia nafasi zinazofaa katika jukwaa la kimataifa."

Bw. Wang alisisitiza kuwa, China imesaidiwa sana na uungaji mkono imara wa nchi za Afrika katika kupata mafanikio ya kiuchumi na hadhi yake ya kimataifa. Ndiyo maana kuimarisha mshikamano na ushirikiano na nchi za Afrika kunalingana na maslahi ya China katika siku zote. Vile vile nchi za Afrika zimenufaika na ushirikiano kati yake na China ikiwa ni pamoja na misaada ya China. Anasema, "China inafanya ushirikiano na Afrika juu ya msingi wa kuwa na usawa na kunufaishana. Misaada ya China kwa Afrika haiambatani masharti ya kisiasa, na misaada hiyo imetoa mchango kwa amani na maendeleo ya Afrika. Wachina wametapakaa huku na huko barani Afrika, na wanaleta manufaa halisi kwa watu wa Afrika."

Bw. Wang aliongeza kuwa, katika jamii ya kimataifa, China siku zote inasimama katika mstari mmoja na nchi zinazoendelea, hususan nchi zilizo nyuma kimaendeleo, na inajitahidi kulinda maslahi yao. Kwa mfano katika masuala ya umaskini na madeni, China yenyewe ni miongoni mwa nchi zinazoendelea, na bado ina watu wengi maskini, lakini China ilitoa ahadi kufuta madeni ya nchi za Afrika, na kuzishawishi nchi zilizoendelea kuchukua hatua zaidi katika masuala hayo.

Kuhusu ziara ya waziri mkuu Weng Jiabao barani Afrika, mtaalamu huyo alieleza kuwa, ziara hiyo hakika itaimarisha mawasiliano ya ngazi ya juu kati ya China na Afrika, na kusaidia kupatikana kwa mwongozo au mwelekezo wa maendeleo ya uhusiano kati ya China na Afrika kwa hivi sasa.