Tiger ni chui mkubwa mwenye milia. Hivi sasa wanyama hao hawapo barani Afrika, hata barani Asia tiger pori ni wachache sana kiasi ambacho wanyama hao wako hatarini kutoweka. Hali hiyo inafuatiliwa na watu wengi, na mmoja wao ni Bibi Quan Li, ambaye alianzisha mfuko mmoja wa kimataifa wa kuwaokoa tiger wa kichina.
Hivi karibuni mwandishi wetu wa habari alifanya mahojiano na Bibi Quan Li nyumbani kwake huko mashariki ya mji wa Beijing.
Baada ya kuingia kwenye nyumba yake ya ghorofa, vitu vinavyohusu tiger vinaonekana hapa na pale na vinawavutia sana watu, ambapo picha ya tiger imetundikwa ukutani, wanasesere wa tiger wanaowekwa kwenye kochi na vitabu kuhusu wanayama hao vimewekwa kwenye rafu. Ni rahisi kutambua kuwa, mwenye nyumba hiyo anawapenda sana tiger.
"Nilizaliwa na upendo kwa tiger. Naona hao ni wanyama wasio na madosari. Wana milia inayopendeza na wana tabia mbili zinazopingana kwa wakati mmoja, wanaweza kuwa wakali sana na pia ni wapole sana. Tiger ni wanyama wa kupendeza sana."
Mwanamke huyo ana mambo mengi ya kuongea kuhusu tiger. Hivi sasa Bibi Quan Li amejikita katika shughuli za kuwalinda tiger wa kichina, si kama tu inatokana na upendo wake kwa wanyama hao, bali pia ametambua umuhimu mkubwa wa kazi ya kuwalinda tiger. Alifafanua kuwa, "Katika dunia ya viumbe, tiger wapo katika ngazi yajuu, kwa hiyo wanajulikana kama wafalme wa wanyama. Ukiwaokoa tiger, maana yake umeokoa mazingira ya viumbe. Kwa sababu kuwepo kwa tiger kunategemea wanyama wanaokula majani, halafu inabidi miti na maji viwepo. Kwa hiyo ni sehemu mbalimbali zinazotegemeana, hii ndiyo dunia ya viumbe."
Bibi Quan Li alianza kuwafuatilia tiger mwaka 1999. Aliwasiliana na maofisa wa Idara ya misitu ya taifa ya China, na kufahamishwa kuwa, tiger wa Huannan ambayo ni aina moja ya tiger wanaopatikana tu nchini China na kwa hiyo kupewa jina la tiger wa China, wako hatarini kutoweka kabisa.
Tangu mwaka 1980, serikali ya China ilianza kuchukua hatua mbalimbali zinazolenga kuwaokoa tiger wa China. Hatua hizo ni pamoja na kupiga marufuku uwindaji, kuanzisha eneo la hifadhi na kusimamisha biashara za mifupa ya tiger. Hata hivyo uchunguzi kadhaa ulionesha kuwa, idadi ya tiger wa China ilikuwa inaendelea kupungua, kiasi ambacho katika miaka karibu 20, tiger wa aina hiyo hawakupatikana porini.
Bibi Quan Li aliona kuwa anabidi kuwasaidia wanyama hao. Alisema "Wanyama hao ni aina ya tiger wanaopatikana nchini China tu, sasa wapo hatarini kutoweka kabisa. Naona nikiwa Mchina, inanibidi kuwasaidia kadiri niwezavyo."
Kutokana na uungaji mkono wa Idara ya misitu ya China, Quan Li aliamua kutoa dola zaidi ya laki moja za kimarekani kuanzisha mfuko wa kimataifa wa kuokoa tiger wa Kichina. Mfuko huo umepata ufadhili kutoka kwa watu wa sehemu mbalimbali duniani.
Bibi Quan Li alisema "Niliwahi kupokea barua moja yenye paundi 17.9 za kiingereza. Aliyenitumia fedha hizo kwenye barua yake alisema 'mimi natoka kwenye ngazi ya chini katika jamii, nafanya kazi ya kuzoa takataka. Pia nasafisha ofisi mbalimbali baada ya kazi. Katika kazi yangu niliokota hela mara kwa mara ambazo si zangu, kwa hiyo naamua kuyachangia mashirika ya hisani. Naona wanyama wanahitaji fedha hizo zaidi kuliko binadamu, na tiger wanastahili kupata pesa hizo kuliko wanyama wengine.'"
Nchini Uingereza, watoto wengi wa shule za msingi walikusanya fedha kwa kuuza mapambo wanayotengeneza ili kutoa mchango kwa mfuko huo. Huku nchini China, watu wanaojitolea walimsaidia Bibi Quan Li kuanzisha tovuti kwenye mtandao wa Internet, kutafsiri nyaraka mbalimbali na kuanzisha shughuli husika.
Mfuko huo umepata uungaji mkono kutoka kwa watu wengi, akiwemo mume wa Quan Li, Bw. Stuart Bray, ambaye ni Mmarekani anayefanya kazi nchini Uingereza.
Quan Li alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, hatua ya kwanza katika uokoaji wa tiger wa Kichina ni kuwasaidia tiger wanaoishi kwenye bustani ya wanyama wawe na uwezo wa kuishi porini. Tiger mmoja wa porini anaishi katika eneo lenye ukubwa wa kati ya kilomita 15 hadi 1,000 za mraba. Lakini ni vigumu kupata eneo kubwa la namna hii nchini China. Kwa ajili ya kuunga mkono kazi ya Quan Li, mume wake Bw. Bray alichangia dola milioni 4 za kimarekani kununua ardhi lenye ukubwa wa kilomita 300 za mraba barani Afrika, ikiwa ni kituo cha kuzaliana kwa tiger wa Kichina na kufanya mazoezi ya kuishi porini kwa tiger. Hivi sasa, tiger watatu wa Kichina wanaotoka kwenye bustani ya wanyama nchini China wanaishi katika kituo hicho.
Jitihada za Bibi Quan Li zimesifiwa na serikali ya China. Ofisa wa Idara ya misitu ya China anayeshughulikia utafiti na maendeleo ya wanyama pori Bw. Lu Jun alisema "Kutokana na ushirikiano kati ya idara yetu na Bibi Quan Li, kazi ya hifadhi ya tiger wa Kichina inafuatiliwa na watu wengi duniani. Hatua hii ni jaribio zuri katika hifadhi ya wanyama na mimea ambayo ipo hatarini kutoweka."
Idhaa ya kiswahili 2006-06-22
|