Uchapaji urembo kwenye nguo kwa nta ni sanaa ya aina pekee ya makabila madogo madogo kwenye sehemu ya milimani, kusini magharibi mwa China. Ingawa sanaa hiyo imekuwepo kwa miaka elfu kadhaa lakini bado ina nguvu kubwa ya uhai. Bw. Hong Fuyuan anayesanifu na kukusanya michoro ya uchapaji huo, aliita sanaa hiyo kuwa ni chemchemi ya milimani.
Uchapaji urembo kwenye nguo kwa nta ni sanaa ya mikono toka zama za kale nchini China, na sanaa hiyo ilirithiwa kizazi na kizazi hadi leo katika sehemu ya makabila madogo madogo mkoani Guizhou na imekuwa mtindo wa kipekee. Mapema katika miaka 2,000 iliyopita, uchapaji urembo kwenye nguo kwa nta tayaari ulikuwepo nchini China. Huu ni ufundi wa kuchora picha kwenye nguo kwa nta, kisha kutia rangi, na baada ya kuondoa nta picha nyeupe ikabaki na kuonekana.
Hong Fuyuan mwenye umri wa miaka 65 alizaliwa katika mji wa Anshun mkoani Guizhou. Tangu alipokuwa mtoto alipenda sana uchoraji picha na hatimaye alishabikia uchapaji urembo kwenye nguo kwa nta. Aliacha maisha yake bora mjini akaenda vijijini kukusanya, kutafiti na kusanifu picha za urembo. Alikuwa mara kwa mara anavuka milima na kufika kwenye vijiji vya makabila ya Wamiao na Wabuyi kujifunza ufundi wa uchapaji huo na kukusanya picha za urembo, aliweka uhusiano mzuri na watu hao. Bw. Hong Fuyuan alisema, "Nilipokuwa vijijini, niligundua kwamba ingawa watu wa makabila madogo madogo, hasa Wamiao na Wabuyi, wanaishi maisha magumu kidogo, lakini walithamini sana utamaduni wao, na walifanya juhudi kubwa kustawisha utamaduni wao. Kutokana na kuathiriwa nao nilianza kufanya utafiti wa utamaduni wao."
Kadiri Bw. Hong Fuyuan alivyozidi kutafiti sanaa ya uchapaji huo ndivyo alivyozidi kuipenda sanaa hiyo. Anaiona sanaa kama inawakilisha utamaduni wa kabila lao, na imeonesha hisia zao, historia yao na utamaduni wao. Sanaa hiyo inaweza kueleza hisia kwa uhuru kabisa kama unavyotaka. Bw. Hong Fuyuan alisema, "Picha za urembo ni za aina nyingi, hasa picha zenye ndege, samaki na wadudu kwa pamoja zinaonesha wazi mapatano ya maisha ya viumbe. Wamio wanaamini kuwa kila kitu kina roho yake, kwa hiyo wadudu na hata majani huchorwa kwa kuwa na hisia."
Bw. Hong Fuyuan anaona picha kama hizo za urembo ni za kipekee duniani, kwani ukiangalia kwa karibu unaona ni samaki, kipepeo, lakini ukiangalia kwa mbali unaona ni maua tu.
Nguo zilizotiwa urembo wa nta zinatumika sana maishani mwa watu wa makabila madogo madogo mkoani Guizhou kama vile shela, aproni, sketi, mwamvuli, kitambaa cha foronya, mfuko wa vitabu na mbeleko. Bw. Hong Fuyuan ameshughulika na kazi ya uchapaji huo kwa miaka 40, amesanifu picha za urembo aina karibu elfu moja. Alisanifu picha za urembo za aina mpya kutoka urembo wa jadi na utafiti wake ni wa kina kuhusu picha za urembo za makabila ya mkoa wa Guizhou. Kwenye picha yake ya "mkusanyiko wa michoro ya dragoni ya China" ni utamaduni pekee wa dragoni wa China. Bw. Hong Fuyuan alisema, "Picha niliyochora ya 'Mkusanyiko wa Michoro ya Dragoni ya China' inaanzia michoro ya dragoni katika zama za kale, baadhi yake inafanana na chura, mingine inafanana na nyungunyungu na mingine inafanana na samaki. Michoro kama hiyo iliendelea hadi enzi za Yuan, Ming na Qing, nyayo za historia yenye miaka elfu tano ya China kuhusu michoro ya dragoni imeoneshwa wazi, na michoro ya dragoni ya kila enzi inaoneshwa katika picha yangu."
Picha ya "Mkusanyiko wa michoro ya dragoni ya China" imeonesha sura za dragoni katika vipindi mbalimbali vya historia. Ili aweze kuchora picha hiyo, Bw. Hong Fuyuan alitumia miaka kadhaa kukusanya nyenzo na kuchagua michoro yenye uwakilishi. Pamoja na hayo, Bw. Hong Fuyuan alisanifu picha nyingi za uchapaji wa urembo kwenye nguo kwa nta kuonesha maisha ya makabila ya Wamiao na Wabuyi.
Ili aweze kukidhi gharama za kuendelea na shughuli zake za utamaduni huo Bw. Hong Fuyuan alianzisha biashara zinazohusiana na sanaa ya uchapaji wa urembo kwenye nguo kwa nta, kwamba katika miaka michache iliyopita alianzisha jumba la sanaa ya uchapaji kwa nta likishughulika na ufundi wa uchapaji, maonesho ya ufundi, maonesho ya usanifu mpya na kukusanya picha za urembo zilizohifadhiwa na wenyeji na kupata picha nyingi. Bw. Hong Fuyuan anaona kwamba ingawa uchumi katika sehemu ya makabila madogo madogo haujaendelea sana, lakini utamaduni wa sehemu hiyo hauko nyuma, watu wa sehemu hiyo wanathamini sana utamaduni wao, na wanarithisha utamaduni wao miaka nenda miaka rudi.
Bw. Hong Fuyuan anaona kwamba akiwa msanii ana jukumu la kuhifadhi utamaduni wa taifa, anatumai kuwa ni vizuri kama watu wengi watashiriki katika hifadhi hiyo. Alisema, "Hivi leo utandawazi unasisitizwa sana duniani, lakini utamaduni lazima uwe wa aina tofauti, kama kila nchi ikipoteza utamaduni wake, dunia haitakuwa na mng'aro, na utamaduni wa taifa ni nguvu ya muungano wa taifa, kutokana na utamaduni huo taifa linakuwepo, kwa hiyo utamaduni wa taifa lazima ulindwe.
Mwaka 1999, Hong Fuyuan alisifiwa na Wizara ya Utamaduni ya China kuwa ni "mmoja wa wasanii wakubwa kumi wa utamaduni wa jadi". Picha za sanaa yake zimehifadhiwa kwenye Jumba la Makumbusho la Taifa. katika miaka ya karibuni, Hong Fuyuan amekuwa anashughulika na kukusanya na kusanifu picha zake za sanaa na mara kwa mara anafanya maonesho nchini na nchi za nje kama Japan, Marekani na kwenye nchi nyingine.
Idhaa ya kiswahili 2006-06-26
|