Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-28 15:53:13    
Ujenzi wa reli ya Qinghai-Tibet

cri
Reli ya kutoka mkoa wa Qinghai hadi mkoa wa Tibet iliyojengwa kwenye uwanda wa juu wa Qinghai na Tibet wenye mwinuko mkubwa zaidi kutoka usawa wa bahari duniani itaanza kufanya kazi tarehe 1, Julai mwaka huu. Kutokana na matatizo ya "kuganda kwa udongo", na "upungufu wa oksijeni kwenye uwanda wa juu", wataalamu wa nchi za nje waliona kuwa haiwezekani kujenga reli kwenye uwanda wa juu wa Qinghai-Tibet, lakini wachina waliondoa matatizo mbalimbali na kufanikiwa kujenga reli hiyo kwenye uwanda wa juu wenye mwinuko mkubwa zaidi duniani.

Kama wimbo huo unaoitwa "njia ya peponi" ambao unajulikana katika uwanda wa juu wa Qinghai-Tibet unavyosema, njia iliyoko kwenye uwanda huo wa juu ni yenye miujiza, na ujenzi wa reli ya Qinghai-Tibet ulikabiliwa na matatizo mengi makubwa.

Kati ya kilomita 1,142 za reli hiyo iliyoanzia Germu hadi Lhasa, zaidi ya nusu yake inapita sehemu yenye udongo ulioganda kwa miaka mingi. Halijoto ya udongo wa aina hiyo ni chini ya sentigredi 0, na kuna mawe na udongo wenye barafu ndani yake. Kutokana na hali hiyo, ujazo wa udongo unatanuka wakati inapoganda, na unapungua wakati wa majira ya joto baada ya kuyeyuka kwa barafu zilizoko ndani yake. Bw. Lin Lansheng ambaye ni mhandisi wa Kampuni kuu ya ujenzi wa reli ya China ambayo ni moja ya makampuni makubwa ya ujenzi wa reli ya Qinghai-Tibet anasema:

"Majengo yaliyojengwa juu ya udongo ulioganda yanaathiriwa vibaya kutokana na kutanuka na kupungua kwa ujazo wa udongo kwa kufuata mabadiliko ya majira."

Suala la kuganda kwa udongo ni tatizo la kidunia. Uchunguzi ulifanywa na Russia mwaka 1994 ulionesha kuwa, asilimia 27.5 ya reli iliyojengwa katika miaka ya 70 ya karne ya 20 nchini humo iliathiriwa na udongo ulioganda. Kwa kawaida mwendo wa garimoshi ni kilomita 50 tu wakati linapopita sehemu zenye udongo ulioganda. Ingawa nchi mbalimbali zikiwemo Russia na Canada pia zinakabiliwa na tatizo la udongo ulioganda, lakini hali yao ya udongo si mbaya sana kutokana na hali ya jiografia yao kwa kuwa mbali na Ikweta. Kinyume chake, uwanda wa juu wa Qinghai-Tibet wa China uko kwenye eneo la latitudo ya chini, mwinuko mkubwa kutoka usawa wa bahari, ambapo jua ni kali, hivyo matendo chini ya ardhi ya uwanda huo wa juu yanabadilika badilika, na kuweka vikwazo vikubwa zaidi kwa ujenzi wa reli ya Qinghai-Tibet.

Ili kuondoa tatizo hilo, wahandisi wa China walifanya juhudi na kupata njia ya utatuzi. Walijaza tuta la mawe lenye urefu wa mita 1 kati ya uso wa ardhi na udongo ulioganda. Bw. Lin Lansheng kutoka Kampuni kuu ya ujenzi wa reli ya China anasema:

"Tuta la mawe limefanikiwa kuepukana na mabadiliko ya halijoto ya udongo uliganda, hatua ambayo inazuia mabadiliko ya ujazo ya udongo, na kuhakikisha mafanikio ya ujenzi wa reli." Bw. Lin Lansheng alisema katika sehemu yenye urefu wa kilomita 110 wa reli hiyo yalijengwa matuta mengi ya mawe.

Hatua nyingine ya kuondoa tatizo la "kuganda kwa udongo" ni kujenga madaraja. Kwenye reli ya Qinghai-Tibet kuna madaraja mengi, na urefu wa jumla wa madaraja hayo ni zaidi ya kilomita 150. Bw. Lin Lansheng anasema:

"Katika reli ya Qinghai-Tibet, urefu wa nguzo za madaraja ni mita 20 hadi 30, na nguzo zilijengwa chini ya safu ya udongo ulioganda kutokana na unyevunyevu, hatua ambayo inaepusha athari kutokana na kutanuka na kupungua kwa ujazo wa udongo ulioganda."

Mbali na suala la kuganda kwa udongo, ujenzi wa reli ya Qinghai-Tibet vilevile ulikabiliwa na hali ngumu ya mazingira ya kimaumbile, ambapo ni muhimu kuhakikisha afya na usalama wa wafanyakazi wa ujenzi. Katika maeneo ya ujenzi ya Reli ya Qinghai-Tibet, halijoto ya chini ni sentigredi 45 chini ya sifuri, na upepo mkubwa unavuma kati ya siku 100 na 160 kwa mwaka, aidha kuna upungufu mkubwa wa oksijeni huko. Wakati reli hiyo ilipojengwa kwa kupita mlima Fenghuo, kiasi cha oksijeni ya huko kilikuwa ni asilimia 50 tu ikilinganishwa na sehemu ya tambarare, na ukosefu wa oksijeni kwenye uwanda wa juu ni tatizo kubwa lililoukabili ujenzi wa reli hiyo. Mkuu wa kundi la ujenzi la reli iliyoko chini ya mlima wa Feng Huo Bw. Ren Shaoqiang anasema:

"Kutokana na hali mbaya ya upungufu wa oksijeni kwenye uwanda wa juu, watu hupatwa na magonjwa mbalimbali, na watu huwa wana hofu kubwa kabla ya kwenda huko."

Ili kutatua suala hilo, mwanzoni wafanyakazi walifanya ujenzi wakiwa na mitungi ya oksijeni, lakini uzito wa mitungi ulikuwa unawapa wafanyakazi mizigo mkubwa. Hivyo ilibidi watafute njia nyingine ya kutatua tatizo hilo. Bw. Ding Shouquan aliyeongoza ujenzi wa reli hiyo chini ya mlima wa Feng Huo anasema:

"Tulijenga vituo vikubwa vya uzalishaji wa oksijeni katika sehemu za mwanzo na mwisho za handaki la reli kwenye mlima wa Fenghuo, na kutoa oksijeni kwenye handaki hilo kwa saa 24 kwa siku."

Bw. Ding Shouquan alimwambia mwandishi wa habari kuwa, kutokana na njia mpya ya kutoa oksijeni, hatari kwa watu kupatwa na magonjwa ya uwanda wa juu imepungua kwa asilimia 94, na hatua hiyo ilitumiwa katika ujenzi wa mahandaki mengine ya reli ya Qinghai-Tibet, ambapo yalijengwa vituo kumi kadhaa vya kutoa oksijeni, hatua ambayo iliweka msingi imara kwa mafanikio ya ujenzi wa reli hiyo, na kutatua kabisa upungufu wa oksijeni kwenye uwanda wa juu. Kutokana na hatua hiyo, hakuna mtu aliyekufa kutokana na upungufu wa oksijeni.

Bw. Ding Shouquan anasema:

"Tulichukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha watu wanaweza kuvuta oksijeni wakati wowote. Mitungi ya utoaji wa oksijeni iliwekwa mbele ya vitanda vya wafanyakazi, na kila mfanyakazi alitakiwa kuvuta oksijeni kwa saa kati ya moja na mbili kila siku. Kwenye sehemu yenye mwinuko wa mita 2800 kutoka usawa wa bahari huko Germu, idara mbalimbali zinazohusika zilihakikisha utoaji wa vyakula, huduma ya matibabu, na vitu vya maisha."

Idhaa ya kiswahili 2006-06-28