Mwaka 2006 ni mwaka wa kuadhimisha miaka 50 tangu China na nchi za Afrika zianzishe uhusiano wa kibalozi. Katibu mkuu wa shirikisho la urafiki kati ya watu wa China na nchi za Afrika Bi. Lin Yi alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari, alisema:
"Katika miaka 50 iliyopita tangu uhusiano wa kibalozi kati ya Jamhuri ya watu wa China na Afrika uanzishwe, mabadiliko makubwa yametokea. China na nchi za Afrika zimepiga hatua kubwa katika kuimarisha urafiki wa dhati na ushirikiano wa kunufaishana, na kazi za shirikisho la urafiki wa China kwa Afrika pia zimepata mafanikio makubwa."
Bi. Lin Yi alifahamisha kuwa, mawasiliano ya kiraia kati ya watu wa China na nchi za Afrika yanaweza kugawanywa katika vipindi viwili. Kipindi cha kwanza ni kuanzia mwanzoni mwa kuasisiwa kwa China mpya hadi wakati kabla China haijaanza kufanya mageuzi na kufungua mlango kwa nchi za nje. Katika muda huo China na nchi za Afrika zilianzisha uhusiano wa kibalozi hatua kwa hatua, baadhi ya nchi za Afrika wakati huo bado zilikuwa katika mapambano dhidi ya utawala wa kikoloni wa nchi za magharibi, na kupigania ukombozi na uhuru wa taifa. Katika hali hiyo, mawasiliano ya kiraia kati ya China na nchi za Afrika yalikuwa shughuli muhimu za kidiplomasia kati ya China na Afrika. China si kama tu iliziunga mkono kwa hali na mali nchi za Afrika ambazo zilikuwa bado hazijapata uhuru na zilifanya mapambano ya kujipatia ukombozi, bali pia ilizisaidia kadiri iwezekanavyo nchi za Afrika zilizopata uhuru kuendeleza uchumi. Nchi za Afrika pia ziliiunga mkono China katika mambo ya kimataifa, mwaka 1971 kutokana na uungaji mkono wa nchi za Afrika, China ilifanikiwa kurudishiwa kiti cha halali kwenye Umoja wa Mataifa.
Mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne ya 20, baada ya China kufanya mageuzi na kufungua mlango, mawasiliano ya kiraia kati ya China na nchi za Afrika yaliingia katika kipindi kipya. Bi. Lin Yi alisema:
"Baada ya China kuanza kufanya mageuzi na kufungua mlango, hadhi ya China duniani iliinuliwa kwa kiwango kikubwa. Hivi sasa China imeanzisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi 47 za Afrika. Mawasiliano ya kirafiki kati ya watu wa China na nchi za Afrika yamepanuliwa katika sekta za uchumi, utamaduni na kati ya serikali za mikoa na miji, na kupata maendeleo makubwa."
Bi. Lin Yi alisema marafiki wa China barani Afrika wanaweza kugawanyika kuwa wa aina tatu. Aina ya kwanza ni mashirika ya kiraia, ambayo ni marafiki wa kimsingi wa China barani Afrika. Aina ya pili ni maofisa na watu mashuhuri, na wa aina ya tatu ni watu wa serikali za mitaa. Katika miaka mingi iliyopita, marafiki hao walitembelea China mara kwa mara, ambao wametia uhai mpya kwa maendeleo ya urafiki kati ya China na Afrika. Kwa mfano mwezi Januari mwaka 2003, shirikisho la urafiki kati ya China na Afrika lilimpokea waziri wa Uganda aliyeshughulikia mambo ya rais Bwana Gilbert Bukenya. Bw. Bukenya aliporudi Kampala baada ya kumaliza ziara yake nchini China, aliambiwa kuwa ubalozi wa China nchini Uganda ulifanya tamasha la kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China, hivyo aliacha kurudi nyumbani na kuelekea moja kwa moja kwenye ubalozi wa China. Alipotoa risala kwenye tamasha hilo, Bw. Bukenya alizungumzia maendeleo ya uchumi yaliyopatikana nchini China na mustakabali mzuri wa ushirikiano kati ya Uganda na China. Baada ya kuteuliwa kuwa makamu wa rais wa Uganda, Bw. Bukenya ametoa mchango mkubwa katika kuhimiza uhusiano na ushirikiano kati ya China na Uganda.
Hadi leo mikoa na miji 69 kati ya China na nchi za Afrika imeanzisha uhusiano wa kirafiki. Bi. Lin Yi alisisistiza kuwa mawasiliano na ushirikiano kati ya serikali za mikoa au miji yamechukua sehemu kubwa katika ushirikiano wa kirafiki kati ya China na Afrika, na imekuwa ni njia muhimu ya kuzidisha urafiki kati ya watu wa China na nchi za Afrika. Alisema:
"Kutokana na maendeleo ya uhusiano kati ya China na nchi za Afrika, mawasiliano kati ya serikali za mikoa na miji yamechukua sehemu kubwa ya mawasiliano ya kiraia kati yetu na nchi za Afrika. Hivi sasa idadi ya ujumbe wa mikoa na miji tunaopokea inaongezeka kwa haraka. Mawasiliano hayo yamehimiza ushirikiano kati ya serikali za mikoa au miji ya China na nchi za Afrika kwenye sekta za uchumi, biashara na utamaduni."
Kutokana na kuongezeka kwa mawasiliano kati ya China na Afrika katika sekta za siasa, uchumi, na utamaduni, wafanyabiashara na watalii wa China wanaotembelea barani Afrika wanaoongezeka siku hadi siku na bidhaa za China zimeonekana hapa na pale barani Afrika, ambapo mashirika ya kiraia yanayopenda kusukuma mbele urafiki kati ya China na Afrika pia yameongezeka.
Shirikisho la urafiki kati ya watu wa China na Afrika lilianzishwa mwaka 1960 na watu mashuhuri. Tangu lianzishwe shirikisho hilo limetoa mchango mkubwa katika kuzidisha urafiki kati ya China na Afrika, na kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali. Bi. Lin Yi alisema shirikisho la urafiki kati ya China na Afrika litaendelea kukutana na marafiki wa Afrika, na pia litajitahidi kuwafahamisha watu wa China hali ya Afrika. Alisema:
"Mwaka huu shirikisho letu litaanzisha "tuzo kwa watu wanaochangia urafiki kati ya China na Afrika", kuwasifu wachina 10 waliojishughulisha kazi za Afrika kwa muda mrefu, na wale wanaojulikana na kutambuliwa na nchi za Afrika. Isitoshe tutashirikiana na vyombo vya habari vya China ili kuwaandaa wachina wa kizazi kipya wanaopenda Afrika na kujishughulisha na kazi za Afrika."
Bi. Lin Yi alisisitiza kuwa maendeleo mazuri ya shughuli za kidiplomasia za raia kati ya China na nchi za Afrika yanaungwa mkono na serikali za China na nchi za Afrika. Mawasiliano ya ngazi ya juu ya kiserikali yataweka mazingira mazuri sana kwa mawasiliano ya kiraia. Bi. Lin Yi alisema, safari ya waziri mkuu Wen Jiabao katika nchi saba za Afrika bila shaka imesukuma mbele mawasiliano ya kiraia kati ya China na Afrika, alisema:
"Mawasiliano ya ngazi ya juu ya kiserikali huleta ufanisi mzuri, kila nchi aliyotembelea waziri mkuu Wen Jiabao imetoa habari nyingi kuhusu ziara yake nchini humo na mambo kuhusu China."
Idhaa ya kiswahili 2006-06-30
|