Bw. Duan Zhuangxin ni mkurugenzi wa idara ya macho, pua na koo katika hospitali ya wanawake na watoto wachanga ya mkoa wa Hubei, China. Aliwahi kufanya kazi nchini Lesotho kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2005. Hadi leo bado anakumbuka vizuri tukio lililomkumba la kuporwa nchini Lesotho. Alisema:
"Siku moja wakati niliporudi nyumbani kutoka kwenye zahanati nilikofanya kazi, njiani vijana wawili walinizuia na kunilazimisha niwape pesa na vitu nilivyokuwa navyo. Nilianza kutafuta pesa mfukoni huku nikiwaambia kwa lugha ya Kiingereza kuwa, mimi ni daktari wa China niliyekwenda huko kuwasaidia."
Baada ya watu hao wawili kuambiwa hivyo, punde si punde waliondoka bila kuchukua pesa alizowapa. Bw. Duan Zhuangxin alipokumbuka maisha yake ya nchini Lesotho alisema:
"Ni kweli hali ya kimaisha ya huko ni ngumu, lakini mimi na madaktari wenzangu tuliishi kwa furaha, kwa sababu watu wa huko walituhitaji na kututhamini."
Kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa na wizara ya afya ya China, katika miaka 43 iliyopita, China ilikuwa imewatuma madaktari elfu 20 kwa nchi na sehemu 47 za Afrika, ambao wamewahudumia wagonjwa milioni 200 hivi.
Mwaka 1963 Algeria ilikumbwa na ukosefu wa madaktari na dawa, na iliomba msaada wa dharura kwa jumuiya ya kimataifa. Kutokana na agizo la waziri mkuu wa zamani Bwana Zhou Enlai, serikali ya China ilituma kikundi cha kwanza cha madaktari nchini Algeria.
Bw. Chen Yunmeng mwenye umri wa miaka 65 aliwahi kufanya kazi ya ukalimani katika kikundi cha 5 cha madaktari cha China huko Zanzibar. Alisema mwaka 1974 yeye na madaktari wa China walisafiri kwa meli pamoja na dawa na vifaa vya tiba, ilichukua nusu mwezi kwao kuwasili Zanzibar. Wakati huo, Zanzibar yenye idadi ya watu laki nne ilikuwa na hospitali moja tu.
Mkurugenzi wa ofisi inayoshughulikia mambo ya Afrika katika taasisi ya sayansi na jamii ya China Profesa He Wenping alisema:
"Mradi wa kutuma vikundi vya madaktari wa China katika nchi za nje ni sehemu muhimu ya sera ya kidiplomasia ya China. China inatoa msaada wa tiba kwa nchi za Afrika siyo kwa ajili ya maslahi, bali ni kwa ajili ya kutoa msaada wa kibinadamu."
Katika nchi za Afrika zilizokumbwa na ukosefu wa dawa na madaktari, madaktari wa China wanapaswa kubeba jukumu kubwa. Daktari mmoja wa magonjwa ya wanawake aliyewahi kufanya kazi katika sehemu ya kaskazini ya Cameroon iliyoko nyuma kimaendeleo alikumbuka kuwa, katika miaka miwili kuanzia mwaka 1998 hadi 2000, kwa jumla aliwahudumia wagonjwa elfu kumi hivi na kufanya operesheni elfu moja hivi. Alisema:
"Ingawa kila siku nilikuwa na kazi nyingi sana, lakini nilijisikia vizuri kutokana na kuweza kuwasaidia wagonjwa wanaonihitaji."
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wizara ya afya ya China, katika miaka 43 iliyopita, madaktari 45 wa China walikuwa wamejitolea mhanga wa maisha yao wakati wa kuwahudumia wagonjwa wa Afrika kutokana na kuambukizwa virusi vya Ukimwi, malaria na kipindupindu.
Bw. Duan Zhuangxin aliwahi kujikata kidole chake alipokuwa anafanya operesheni. Kwa sababu zahanati aliyokuwa akifanya kazi haikuwa na mchakato wa kupima virusi vya Ukimwi kwa wagonjwa kabla ya kufanyiwa operesheni, hivyo baada ya kutokea kwa tukio hilo, Bw. Duan Zhuangxin alisumbuliwa sana na hofu ya kuambukizwa virusi vya Ukimwi. Alisema:
"Wakati huo niliamua kuwa, kama kweli niliambukizwa virusi vya Ukimwi, nitabaki huko kufanya kazi mpaka niugue hadi kufa." Kwa bahati nzuri, matokeo ya upimaji wa virusi vya Ukimwi yalikuwa ni ya kumfurahisha.
Idhaa ya kiswahili 2006-06-30
|