Wachina ambao wanachukua 21% ya jumla ya idadi ya watu duniani, wanaishi kwa kutegemea 7% ya rasilimali ya maji ya duniani. Pamoja na kuongezeka kwa mfululizo kwa idadi ya watu na maendeleo ya kasi ya uchumi, China inakabiliwa na changamoto kubwa la upungufu wa maji.
Tangshan ni mji muhimu wa viwanda kwenye sehemu ya kaskazini mwa China. Sekta za makaa ya mawe, usafishaji madini na vyombo vya kauri za mji huo ni maarufu sana nchini China, lakini sekta hizo zote zinatumia maji kwa wingi. Ili kudhibiti matumizi ya rasilimali ya maji, mji wa Tangshan umeweka lengo la kujenga mji unaotekeleza udhibiti wa matumizi ya maji, na kujitahidi kusafisha maji yaliyokwisha tumika na kuongeza ufanisi wa matumizi ya maji ya aina hiyo yaliyosafishwa.
Katika mji wa Tangshan, majitaka yanayotolewa na migodi 11 ya makaa ya mawe ya kampuni ya makaa ya mawe ya Kairuan ni mita za ujazo zaidi ya milioni 100 kwa mwaka. Mwaka 1992 Kampuni ya Kairuan ilijenga kiwanda cha kusafisha maji ili kutumia tena maji hayo yaliyokwisha tumika. Naibu mkuu wa kiwanda cha kusafisha maji Bw. Guo Hai alisema,
"Gharama ya kusafisha tani moja ya majitaka ni Yuan za Renminbi 1.32, lakini gharama ya kuchukua tani 1 ya maji kutoka kisimani ni Yuan 2.12. Endapo tunasafisha maji tani milioni 3.6 kwa mwaka, si kama tuna tunaweza kupunguza matumizi ya maji mengi safi, bali pia tunapunguza gharama za uzalishaji kwa Yuan karibu milioni 2.9 kwa mwaka.
Bw. Guo Hai alisema maji yaliyosafishwa sio tu yanaweza kutumika katika kunyunyizia miti na majani yaliyopandwa, bali pia yanaweza kutumiwa kuongeza uzuri wa mandhari na kuboresha mazingira.
Kampuni ya vyombo vya kauri ya Huamei ni kampuni nyingine muhimu mjini Tangshan, ili kuinua ufanisi wa rasilimali ya maji, kampuni hiyo imenunua zana za kusafisha majitaka kwa Yuan laki 2, ambazo zinaweza kusafisha tani 1,000 za majitaka kwa siku. Maji yaliyosafishwa yanaweza kutumika tena katika uzalishaji, hivyo kampuni hiyo haitoi majitaka nje.
Hivi sasa kiasi cha 65% ya majitaka ya mji wa Tangshan yanasafishwa, hatua ambayo imedhibiti vizuri matumizi ya rasilimali ya maji. Tangshan ni moja tu ya miji inayotekeleza udhibiti wa matumizi ya rasilimali ya maji nchini China. Lengo lililotolewa na serikali ya China linataka kiasi cha 10% hadi 15% ya majitaka ya miji ya sehemu ya kaskazini yenye upungufu wa maji, yasafishwe na kutumika tena, wakati miji yenye upungufu wa maji kwenye pwani ya kusini inatakiwa kusafisha 5% hadi 10% ya majitaka yanayotolewa huko.
Basi, ni kwa nini China inazingatia sana suala la udhibiti wa matumizi ya maji? Hali halisi ya rasilimali ya maji ya China ikoje?
Hivi sasa rasilimali ya maji ya China ni kiasi cha mita za ujazo trilioni 2.8, ikichukua nafasi ya 6 duniani, lakini wastani wa rasilimali ya maji kwa kila mtu ni kiasi cha mita za ujazo 2,200 tu, kiasi hicho ni kiasi cha 30% ya wastani wa rasilimali ya maji kwa kila mtu duniani.
Kutokana na kukabiliwa na changamoto kali ya namna hiyo, serikali ya China imetoa wito wa kudhibiti matumizi ya maji na kutekeleza hatua za kuinua ufanisi wa rasilimali ya maji. Katika miaka ya karibuni China imebuni sera mpya za kupanga matumizi ya rasilimali ya maji kwa mbinu ya kimasoko.
Mto Manjano ni mto muhimu unaopita kwenye sehemu ya kaskazini mwa China, mikoa inayojiendesha ya kabila la wahui wa Ningxia na Mongolia ya ndani, ambayo iko kwenye kando za mto huo, inachukua maji mengi kila mwaka kwa matumizi ya kilimo. Hususan mahitaji ya maji ya mikoa hiyo miwili yameongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na maendeleo ya kasi ya viwanda ya mikoa hiyo, lakini maji mengi yanapotea bure kutokana na hali duni ya miundo-mbinu kuhusu umwagiliaji maji mashambani, hali ambayo hawana fedha za kutosha za kufanya marekebisho.
Tokea mwaka 2003, mikoa ya Ningxia na Mongolia ya ndani inatekeleza sera mpya, ambazo viwanda vinatoa fedha za kurekebisha zana za umwagiliaji maji mashambani, na vinapata maji kulingana na kiasi cha maji yanayookolewa katika uzalishaji mazao ya kilimo ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya maji kwa viwanda. Naibu waziri wa maji wa China Bw. Hu Siyi alisema,
"Hatua hizo zinazochukuliwa zimeboresha muundo wa matumizi ya maji na ugawaji wa maji kati ya matumizi ya maji ya viwanda na kilimo, kuinua ufanisi wa matumizi ya rasilimali ya maji na kuhakikisha kutosheleza mahitaji ya maji ya maendeleo ya uchumi na jamii ya huko."
Takwimu za mwanzo zinaonesha, matumizi ya maji yaliyopungua katika umwagiliaji maji mashambani katika majira ya mpukutiko ya mwaka 2005 peke yake, yalifikia mita za ujazo zaidi ya milioni 20, ikilinganishwa na yale ya kipindi kama hiki cha mwaka uliotangulia. Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2010, viwanda vya mikoa ya Ningxia na Mongolia ya ndani vitaweza kupata maji mita za ujazo karibu milioni 600 ya matumizi ya maji yatakayopungua katika kilimo kutokana na utekelezaji wa sera hizo.
Mabadiliko ya matumizi ya maji kati ya viwanda na kilimo yametatua kwa kiwango fulani tatizo la matumizi ya ovyo ya maji ya kilimo, lakini tukikataka kupunguza matumizi ya kilimo, njia ya kimsingi kabisa ni kutegemea teknolojia ya kisasa ya kilimo. Hivi sasa mtindo wa jadi wa umwagiliaji maji mashambani bado unatekelezwa nchini China, ambapo maji yanapelekwa kwa mifereji ya udongo, na mashamba yanamwagiliwa kwa maji mengi, hivyo kiasi cha nusu ya maji yanapotea kwa kuingia ardhini kwenye mifereji ya udongo. Hivyo kubadilisha mtindo wa umwagiliaji maji mashambani ni mkazo unaotakiwa kuwekwa katika shughuli za udhibiti wa matumizi ya maji ya kilimo.
Hali ya hewa ya mkoa wa Xinjiang Uygur, ambao uko kaskazini magharibi mwa China ni ya ukame, hivyo matumizi ya maji ya kilimo yanakabiliwa na changamoto kubwa. Ofisa wa mji wa Shihezi wa mkoa huo anayeshughulikia udhibiti wa matumizi ya maji Bw. Su Jun alisema, tokea mji huo uanze kutumia teknolojia ya kumwagilia maji mashambani kwa matone ya maji juu ya mazao ya biashara mwaka 1996, ambayo maji yanapelekwa kwa mabomba na kuingia katika udongo kwenye mizizi ya mimea kwa matone ya maji, wametimiza lengo la kudhibiti matumizi ya maji na kupata mavuno mazuri zaidi.
"Hadi hivi sasa, mashamba ya mji wetu kiasi cha hekta laki 1.2, ambayo ni 60% ya mashamba yetu yote, yanamwagiliwa kwa mtindo huo mpya. Katika miaka ya karibuni tulipata mavuno mazuri ya kilimo kila mwaka, na mavuno ya kilimo ya mwaka uliopita yaliweka rekodi mpya. Teknolojia hiyo inatumika kwa mazao mengi yakiwa ni pamoja na pamba, nyanya na mizabibu. Gharama ya zana mpya za umwagiliaji maji mashambani ni kiasi cha Yuan 400 kwa hekta 0.07, ambayo ni pungufu kwa 60% ikilinganishwa na matumizi ya zana zinazoagizwa kutoka nchi za nje.
Mbali na hatua za udhibiti wa matumizi ya maji, China imebuni sera za mageuzi kuhusu bei ya maji yenye lengo la kuhimiza udhibiti wa matumizi ya maji na kuhifadhi rasilimali ya maji.
Idhaa ya kiswahili 2006-07-04
|