Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-10 15:46:23    
Mchoraji anayetamani amani ya Mashariki ya Kati, Feng Shaoxie

cri

Maonesho ya picha za mchoraji Feng Shaoxie yanayofanyika katika Jumba la Sanaa la Beijing yanayoitwa "Njiwa wa Mashariki ya Kati" yanavutia watazamaji wengi. Picha zilizochorwa zenye mada ya amani ni nadra kupatikana katika historia ya uchoraji nchini China. Picha hizo zinawavutia sana watazamaji.

Picha zinazooneshwa ni 18, na kila moja ina ukubwa wa mita 2.5 kwa mita 2. Watazamaji wanapoingia ukumbini mara wanavutiwa na picha ya "Njiwa wa Mashariki ya Kati" ikionesha njiwa aliyejeruhiwa na kulowa damu akidonoa bendeji, na nyuma ya jiwa huyo bendera mbili za Israel na Palestina zikionekana ndani ya moshi wa baruti. Picha nyingine iitwayo "Wimbo wa Amani" ikionesha karatasi ya "Wimbo wa Amani" iliyogunduliwa kutoka kwenye suti ya waziri mkuu wa zamani wa Israel aliyeuawa Yitzhak Rabin, manyoya kadhaa yenye damu yalidondoka yakimaanisha njiwa huyo wa amani amekufa. Na pia kuna picha nyingine ambazo zinaonesha watoto yatima wa Palestina na Israel wanaonekana kufadhaika, warembo wenye "bomu mwilini", waziri mkuu wa zamani wa Israel Sharon anayegeuza uso nyuma kwa hasira, kiongozi wa zamani wa Palestina Arafat anayehutubia kwa hasira, kiti cha magurudumu kilichoachwa mahali alipouawa kiongozi wa kidini wa kundi la Hamas Yasin na ukuta wa utenganishaji unaoonekana kwenye ukungu. Kumbukumbu za watu katika miaka mingi iliyopita kuhusu hali ya Mashariki ya Kati zinaoneshwa vilivyo katika picha hizo na zinawavutia sana watazamaji. Njiwa wa amani anaonekana kwa namna tofauti katika picha zote 18, na kila picha ni kauli mbiu ya amani wanayotaka watazamaji.

Mwananadharia wa uchoraji wa China na mhariri mkuu wa jarida la "Sanaa ya Uchoraji" Bw. Wang Zhong alisema, "Picha hizi za Bw. Feng Shaoxie zimeonesha jinsi wasanii wa China wanavyotamani Mashariki ya Kati iwe na amani, ni maonesho ambayo hayajawahi kuonekana nchini China katika miaka mingi iliyopita. Kwa kuwa mada ya picha hizo ni muhimu, na ni mara ya kwanza kwa wasanii kuhusisha mada hiyo muhimu ya kimataifa ambayo inafuatiliwa sana duniani kuhusu amani ya Mashariki ya Kati. Kuonesha mada hiyo kwa picha ni kazi ngumu, licha ya kuhitaji majukumu ya kijamii, fikra za kuhangaikia hatima ya binadamu, na pia inahitajika kiwango kikubwa cha uchoraji, bila kiwango hicho hata mtu akiwa na nia ya kuchora picha hizo atashindwa."

Kama Wang Zhong alivyosema, katika nyanja ya uchoraji, ni wachoraji wachache tu waliochora picha nyingi kama hizo zinazoonesha mada hiyo, hata kama wapo, basi wnachora picha moja moja tu. Bw. Feng Shaoxie alitumia miaka miwili kuchora picha hizo mfululizo zenye mada ya "Njiwa wa Mashariki ya Kati". Uwezo wake wa kuchora picha hizo unatokana na maisha yake ya usanii. Bw. Feng Shaoxie alisema, "Ni tabia yangu ya kuzingatia mambo makubwa makubwa duniani yakiwemo mambo muhimu nchini China. Katika mambo hayo kuna mambo yanayohusiana na siasa, na kuna mambo yanayohusiana na ubinadamu. Kozi niliyojifunza sio uchoraji wa picha za mafuta ya rangi, wanafunzi wengi waliosoma katika vyuo vikuu vya uchoraji wanafuata njia walizofundishwa na walimu wao, lakini mimi sivyo, pengine niliathiriwa na kazi yangu ya kisiasa nilipokuwa serikalini, nazingatia zaidi mambo ya siasa. Naona wasanii licha ya kujitahidi kuinua kiwango cha usanii wao, nao pia ni lazima wawe na majukumu ya kijamii."

Bw. Feng Shaoxie alizaliwa mwaka 1964 mkoani Guangdong, na toka alipokuwa mtoto alipenda uchoraji. Mwaka 1983 alijiunga na shule ya sanaa ya uchoraji kwenye vyombo vya kauri, lakini hakupenda, bali alifanya juhudi kubwa zaidi katika uchoraji wa picha za rangi ya mafuta kwa kujifunza mwenyewe. Muda si mrefu baada ya kumaliza shule alikuwa mkuu wa kituo cha utamaduni, kisha alikuwa naibu mkuu wa idara ya utamaduni katika mji wa Foshan. Mwaka 2003 alifanya maonesho binafsi ya picha katika Jumba la Sanaa la Beijing. Maonesho ya picha zake kwa jina la "Itupiwe Macho Hali ya Soko la Utamaduni" yalikuwa kama kioo cha kuonesha hali halisi ya jamii, kwamba katika miaka ya mageuzi, kumetokea hali isiyotakikana katika sehemu za burudani, hali ambayo ilileta taathira mbaya katika jamii, kwa hiyo watu wanamsifu kuwa ni "mchoraji anayekosoa jamii".

Ili aweze kutumia juhudi zote katika uchoraji aliacha kazi yake ya kiserikali. Hivi sasa yeye ni mwenyekiti wa Shirikisho la Wachoraji Picha la Mji wa Foshan. Ili kuinua upeo wake wa usanii alishiriki katika darasa la utafiti wa uchoraji katika Chuo cha Utafiti wa Sanaa ya China, na alijifunza na kufanya utafiti nadharia ya sanaa ya uchoraji. Katika mazoezi yake ya uchoraji alivumbua mtindo wake kipekee kwa kuchanganya uchoraji wa Kimagharibi na wa Kichina.

Mwaka 2004 Bw. Feng Shaoxie alifuatilia zaidi suala la Mashariki ya Kati, lakini kwa nini alichagua mada hiyo kutoka mambo mengi duniani? Alisema, "Kwenye matangazo ya televisheni, karibu kila siku tunasikia habari kuhusu matatizo ya Mashariki ya Kati, hiki ni kitu kilichonichochea kuchora picha hizo. Nia yangu ni kuomba jumuyia ya kimataifa ifanye juhudi na kuanzisha tena mpango wa amani ya Mashariki ya Kati na kutatua mgogoro kati ya Palestina na Israel kwa njia ya mazungumzo. Pamoja na hayo, nikiwa msanii wa China nina jukumu la kuonesha kuwa China ni taifa la kupenda amani."

Katika muda wa miaka miwili hivi Bw. Feng Shaoxie alikusanya habari nyingi kuhusu suala la Mashariki ya Kati na baadhi ni habari alizoomba wengine wamtafsirie kutoka lugha nyingine, kazi yake ilikuwa ngumu. Alisema, "Kazi ilikuwa ngumu sana, ugumu wake ulikuwa ni kusoma nyaraka nyingi, kuzielewa kwa kina, kufanya ufafanuzi, na kuhakikisha nina msimamo bila kuwa na upendeleo wowote. Kusoma na kufahamu kwa kina kuliniletea msukumo mkubwa wa kuchora picha hizo, msukumo huo ni muhimu sana, bila msukumo huo nisingeweza kuchora picha hizo za kugusa mioyo ya watazamaji."

Katika picha zake Bw. Feng Shaoxie kwa makusudi alitumia mtindo wa uchoraji wa Kichina na wa Kimagharibi, anaona ni mtindo huo tu ndio unaoweza kuonesha vizuri zaidi hisia za wasanii wa China kuhusu suala la Mashariki ya Kati. Picha yake ya mwisho katika picha zake18 inayoitwa "Pambazuko la Amani" inaeleza: Alfajiri, ukungu unaelea ndani ya msitu wa mizeituni, njiwa wa amani akiwa na tawi la mzeituni mdomoni akiruka kwenye mwangaza wa pambazuko. Lakini mwangaza huo si kama mwangaza mwekundu kabla ya jua kuchomoza. Watazamaji wanapoangalia picha hiyo wanahisi baridi kidogo kutoka ukungu huo, na wanajiuliza, lini njiwa huyo ataruka hadi juu ya anga ya Mashariki ya Kati? Bw. Feng Shaoxie alisema, "Mwangaza wa pambazuko nyuma ya msitu sio wazi, watu wanatamani kuona mwangaza safi wa pambazuko, wanatamani amani ya Mashariki ya Kati, na kutokana na juhudi za jumuyia ya kimataifa, eneo la Mashariki ya Kati litafuata njia ya amani."

Idhaa ya kiswahili 2006-07-10