Naibu waziri wa biashara wa China bibi Ma Xiuhong tarehe 8 hapa Beijing alisema, hivi sasa serikali ya China inafanya marekebisho juu ya muundo wa miradi ya uzalishaji mali iliyowekezwa na wafanyabiashara wa kigeni hapa nchini, wakati wa kuendeleza uzalishaji wa kisasa, inahimiza maendeleo ya sekta ya huduma, kufanya ushirikiano wa kiuchumi na nchi za nje na kuzielekeza kampuni za China kuwekeza katika nchi za nje.
Katika mazingira, ambayo uwekezaji wa nchi za nje unaongezeka kwa kasi, serikali ya China imekuwa ikizingatia kiwango cha kutumia mitaji ya nchi za nje. Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika tarehe 8 hapa Beijing, naibu waziri wa biashara wa China bibi Ma Xiuhong alisema, hivi sasa China inapojitahidi kuvutia mitaji ya kigeni kuendeleza sekta ya uzalishaji wa kisasa, inaboresha matumizi ya mitaji ya kigeni, katika mpango wa maendeleo ya uchumi na jamii ya miaka mitano ijayo, ambao ulitolewa hivi karibuni, serikali imetoa maelezo wazi kuhusu uboreshaji wa maendeleo ya viwanda vilivyowekezwa na wafanyabiashara wa kigeni.
"Katika miaka 5 ihayo, tunatakiwa kuboresha zaidi muundo wa uzalishaji mali uliowekezwa na wafanyabiashara wa kigeni, kuwahimiza wafanyabiashara wa kigeni wawekeze katika viwanda vya teknolojia ya kisasa, vituo vya utafiti na viwanda vya kisasa, vilevile tunawahimiza kuwekeza katika sekta ya huduma ili kuhimiza maendeleo ya sekta ya huduma ya kisasa ya China. Katika utekelezaji wa sera za kuvutia mitaji ya kigeni, tunatakiwa kuzingatia maendeleo ya uwiano ya kikanda, tunawahamasisha wafanyabiashara wa kigeni waende kuwekeza katika sehemu ya magharibi ya China, vituo vya viwanda vya zamani vilivyoko kwenye kaskazini mashariki pamoja na sehemu ya kati ya China ili kukuza umuhimu wa mitaji ya kigeni kwa maendeleo ya uchumi wa China."
Wakati China inapoendeleza ufunguaji kwa nje na kuvutia mitaji ya kigeni, pia inahimiza kampuni na viwanda bora vya China viende nchi za nje kutafuta nafasi mpya za maendeleo na kushiriki ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara duniani. Hadi mwishoni mwa mwaka 2005, mitaji iliyowekezwa na kampuni na viwanda vya China katika nchi za nje imezidi dola za kimarekani bilioni 51.7. Katika muda huo miradi inayoendelezwa ya utoaji misaada kwa nchi za nje pia imepata maendeleo.
Miradi iliyowekezwa na kampuni na viwanda vya China na yenye mafanikio katika nchi za nje ni pamoja na kampuni ya Legend kununua shughuli za uzalishaji kampyuta za kampuni ya IBM ya Marekani, kampuni ya mafuta ya asili ya petroli ya China kununua kampuni ya mafuta ya PK ya Hazakstan, kampuni ya magari ya Nanjing kununua kampuni ya Rover ya Uingereza pamoja na kampuni za Haier na TCL kujenga viwanda na vituo vya utafiti katika nchi za nje. Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika tarehe 8, naibu waziri wa biashara wa China bibi Ma Xiuhong alisema, kuhimiza kampuni na viwanda vya China kushiriki maendeleo ya uchumi duniani ni moja ya mikazo iliyowekwa katika serikali za China, mazungumzo ya 10 ya uwekezaji na biashara ya China yatakayofanyika hivi karibuni katika mkoa wa Fujian ulioko pwani ya kusini mashariki mwa China ni mahali pazuri kwa mazungumzo kati ya wawekezaji wa China na miradi ya nchi za nje:
"Tunajitahidi kuhimiza kampuni na viwanda vya China viwekeze katika nchi za nje, siyo tu katika nchi zinazoendelea, bali pia katika nchi zilizoendelea. Katika mazungumzo ya uwekezaji na biashara yaliyofanyika hivi karibuni nchini China, mashirika mengi ya uvutiaji uwekezaji kutoka Marekani na nchi za Ulaya, yalifika China kuonesha mazingira ya uwekezaji ya huko ili kuvutia kampuni na viwanda vya China kuwekeza katika nchi zao."
Bibi Ma Xiuhong alisema, katika miaka ya karibuni, serikali ya China imechukua hatua nyingi za mageuzi zikiwa ni pamoja na kuruhusu wawekezaji wenye sifa zinazotakiwa kuwekeza katika soko la hisa la China, kupunguza masharti kwa shughuli za benki za nchi za nje zilizoko nchini China na kuondoa kikomo cha mahitaji ya fedha za kigeni vinavyohitaji viwanda vya China vinavyowekeza katika nchi za nje. Hatua hizo zilizochukuliwa na serikali ya China zitafanya kazi muhimu kwa maendeleo ya uchumi duniani.
Idhaa ya kiswahili 2006-07-11
|