Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-12 09:58:32    
Kuacha tabia ya kuvuta sigara

cri

Utafiti wa sayansi umeonesha kuwa, tumbaku ikiwashwa inatoa aina zaidi ya 4000 ya vitu vyenye sumu kwa binadamu ambavyo vitaweza kusababisha magonjwa ya saratani, tatizo la mishipa ya moyo na tatizo la mifupa osteoporosis. Kila mwaka watu wapatao milioni 5 wanakufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na tumbaku. Watu wengi wenye tabia ya kuvuta sigara wanapenda kuacha tabia hiyo lakini ni wachache tu wanaoweza kufanya hivyo. Hivi sasa watu bilioni 1.1 duniani wana tabia ya kuvuta sigara, na nusu kati yao wanataka kuacha tabia hiyo. Naibu mkurugenzi wa taasisi ya kinga na udhibiti wa magonjwa ya China ambaye ni mtaalamu mashuhuri wa afya ya umma Bi. Yang Gonghuan alisema:

"kuacha tabia ya kuvuta sigara kwanza kunahitaji nia thabiti, na nia hiyo lazima iungwe mkono na jamaa na marafiki. Kama jamii ingekuwa na mazingira ya kuhamasisha kuacha tabia hiyo, basi ingekuwa ni rahisi zaidi kuacha tabia hiyo. Kwa watu wanaotawaliwa na uvutaji wa sigara, huenda wanahitaji uungaji mkono wa dawa. Hivyo kwa ufupi, kuacha tabia ya kuvuta sigara kunahitaji nia thabiti, mazingira mwafaka na uungaji mkono wa dawa."

Kama alivyosema Bi. Yang Gonghuan, nia thabiti, mazingira mwafaka na uungaji mkono wa dawa ni mambo matatu muhimu ya kuacha tabia ya kuvuta sigara. Ukitaka kuwa na nia imara, kwanza unapaswa kufahamu madhara makubwa kwa afya yanayosababishwa kutokana na kuvuta sigara, pia unapaswa kufahamu kuwa kuvuta sigara ni kitendo kisicho na maadili. Mkazi mmoja wa Beijing Bi. Li Guizhen alisema,

"kuvuta sigara ni tabia mbaya kwa wazee. Nikikohoa, hata makohozi yanakuwa na rangi nyeusi."

Inasemekana kuwa idadi ya vijidudu vilivyoko kwenye midomo ya watu wanaovuta sigara ni ndogo sana kuliko watu wasiovuta sigara. Pia inasemekana watu wanaovuta sigara wakiacha uvutaji wa sigara wataumwa.

Maana hiyo potofu inaweza kuathiri nia ya watu kutaka kuacha tabia ya kuvuta sigara. Hivyo kuna haja kubwa ya kufahamu ujuzi unaohusika. Kwa ukweli, majaribio mengi ya kisayansi yameonesha kuwa, uvutaji wa sigara hauna manufaa yoyote kwa afya ya watu bali unaleta madhara tu; Bila kujali una umri wa miaka mingapi au umevuta sigara kwa miaka mingapi, kuacha tabia ya kuvuta sigara ni jambo zuri; kuacha kuvuta sigara huenda kutaleta karaha kwa muda mfupi lakini hakutasababisha magonjwa.

Pamoja na nia imara, mazingira mwafaka kwa kuacha kuvuta sigara pia ni muhimu sana. Mazingira hayo ni pamoja na mazingira makubwa ya kijamii na mazingira yanayokuzunguka, kwanza inapaswa kuboresha mazingira makubwa ya kijamii.

Hivi sasa nchi zaidi ya 190 zimejiunga na mkataba wa udhibiti wa tumbaku duniani, matangazo ya tumbaku yamepigwa marufuku kuoneshwa kwenye vyombo vya habari vya umma, sheria za kupiga marufuku tumbaku zimetolewa katika nchi mbalimbali, na mazingira makubwa ya kuhimiza kuacha uvutaji wa sigara yameanza kujengwa.

Mbali na mazingira makubwa ya kijamii, pia ni muhimu kuandaa mazingira yanayokuzunguka ya kuhimiza kuacha uvutaji wa sigara. Iambie jamii, majirani, marafiki zako kwamba umeanza kuacha kuvuta sigara, na kutaka uungaji mkono wao. Pia unaweza kutafuta watu wengine wanaotaka kuacha tabia hiyo basi mnaweza kuungana mikono, hivyo jambo hilo litakuwa rahisi zaidi.

Kwa watu wanaotawaliwa na uvutaji wa sigara, mbali na hatua hizo, pia wanahitaji uungaji mkono wa dawa. Dawa hizo zinaweza kupunguza dalili mbaya zinazotokea baada ya kuacha kuvuta sigara.

Hivi sasa, dawa za kusaidia watu kuacha kuvuta sigara zina aina tatu. Dawa ya kawaida kabisa ni peremende ya kutafuna, manufaa yake ni kwamba inaweza kupunguza mara moja kiu ya sigara. Nyingine ni vidonge vya nicotin. Nicotin iliyo ndani ya sigara inawafanya watu watake kuendelea kuvuta sigara, lakini haitasababisha magonjwa, hivyo ukitumia vidonge vya nicotin badala ya kuvuta sigara, utaacha tabia hiyo polepole. Ya tatu ni wellbutrin, hii ni dawa mpya, kazi yake inafanana na vidonge vya nicotin.

Hayo ni mambo matatu muhimu katika juhudi za kuacha tabia ya kuvuta sigara. Lakini kumbukeni tu kama umeacha kuvuta sigara kwa muda wa zaidi ya miezi 6, basi lazima ujizuie na kuendelea kuwa mbali na sigara, usije ukavuta sigara tena.

Bi. Lu Xiuxia ni mwalimu, ambaye alivuta sigara kwa miaka 30. mwaka 2004 alianza kuacha kuvuta sigara, lakini baada ya mwaka mmoja tu, amerejea na tabia hiyo, na kuvuta sigara zisizopungua nne kila siku. Bi. Lu Xiuxia alisema:

"marafiki zangu waliniuliza mbona unavuta sigara tena? Basi nikawajibu kuwa sina tabia mbaya katika maisha yangu ila tu kuvuta sigara."

Lakini kurejea kuvuta sigara ni jambo la kawaida kwa watu wanaojaribu kuacha kuvuta sigara, hakuna haja ya kujisikia vibaya, kuvunjika moyo au kuwa na wasiwasi kuhusu uwezo wako wa kuacha tabia hiyo. Watu wengi wanaotaka kuacha tabia hiyo wana uzoefu wa kukatisha tamaa zaidi ya mara moja, hatimaye wataweza kufanikiwa kuacha kabisa tabia hiyo. Takwimu husika zimeonesha kuwa, kwa wastani mtu mmoja baada ya kujaribu mara saba kuacha tabia ya kuvuta sigara, ataweza kufanikiwa kikamilifu. Hata kama ukirejea kuvuta sigara baada ya kuiacha kwa muda, lazima uendelee kushikilia nia ya kuacha tabia hiyo, na kuanza tena kuacha kuvuta sigara mapema.