Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-14 20:53:00    
Ziara ya Ofisa Mkuu Mtendaji wa NEPAD nchini China

cri

   

Kutokana na mwaliko wa katibu mkuu wa kamati inayoshughulikia utekelezaji wa mpango wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, ambaye pia ni mkuu wa idara inayoshughulikia mambo ya Afrika ya wizara ya mambo ya nje ya China Bi. Xu Jinghu, Ofisa Mkuu Mtendaji wa sekretarieti ya mpango wa ushirikiano mpya wa maendeleo ya uchumi wa Afrika NEPAD Prof. Firmino Mucavele aliongoza ujumbe wake kutembelea China kuanzia tarehe 7 hadi 14 mwezi Julai mwaka huu.

Tarehe 7 alasiri Bi. Xu Jinghu alifanya mazungumzo na Prof. Firmino Mucavele na ujumbe wake. Bi. Xu alieleza uhusiano wa ushirikiano kati ya China na Afrika na sera za China kwa Afrika, na kulaani usemi wa "tishio la China" unaosambazwa na watu fulani na ati lengo la China kupanua ushirikiano kati yake na nchi za Afrika ni kwa ajili ya kutekeleza ukoloni mamboleo barani Afrika. Alisema China inapenda kujenga uhusiano mpya wa kimkakati na kiwenzi kati yake na nchi za Afrika wa kuwa na usawa na uaminifu kisiasa, kufanya ushirikiano wa kunufaishana kiuchumi na kufundishana utamaduni.

Bi. Xu Jinghu alisema China inafuatilia na kuunga mkono mpango NEPAD, ofisi ya sekretarieti ya kamati inayoshughulikia utekelezaji wa mipango ya baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika itazidisha mazungumzo na ushirikiano na sekretarieti ya NEPAD. Alisema China inatilia maanani mkutano wa tatu wa mawaziri wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika unaotazamiwa kufanyika mwanzoni mwa Novemba mwaka huu mjini Beijing, na kuukaribisha upande wa Afrika kushiriki katika kazi za maandalizi ya mkutano huo, ili kuhakikisha mkutano huo unafanyika kwa mafanikio.

Prof. Mucavele amekubaliana na maneno ya Bi. Xu Jinghu kuhusu uhusiano kati ya China na Afrika. Alisema, katika miaka mingi iliyopita, China imeunga mkono juhudi za nchi za Afrika katika kujipatia ukombozi, ujenzi wa kiuchumi na maendeleo ya kijamii, China ni rafiki wa kweli wa watu wa Afrika, nchi za Afrika hazina wasiwasi kuhusu usemi wa "tishio la China" kama baadhi ya watu wanavyotia chumvi, bali zinataka kuimarisha ushirikiano kati yao na China katika sekta mbalimbali. Alisema mpango wa NEPAD unatilia maanani kufanya ushirikiano na nchi za Asia hasa China, na unatarajia kuwa ushirikiano kati yake na China utapata mafanikio mazuri.

Tarehe 11 asubuhi naibu waziri wa mambo ya nje wa China Bw. He Yafei alikutana na Prof Mucavele na ujumbe wake hapa Beijing. Alisema mpango wa NEPAD umechangia kuhimiza maendeleo ya uchumi na jamii ya nchi za Afrika. China inatilia maanani kufanya ushirikiano kati yake na nchi za Afrika, na kuzisaidia nchi za Afrika kwa vitendo halisi ili kuhimiza maendeleo ya pamoja. Katika muda mrefu uliopita, serikali ya China imezipa nchi za Afrika misaada bila ya masharti, ili kuzisaidia kuinua uwezo wa kujiendeleza. China inazichukua nchi za Afrika kuwa ni washirika wenye usawa na inapenda kuanzisha uhusiano mpya wa kimkakati na kiwenzi. Ushirikiano kati ya China na Afrika ni wa kunufaishana, ambao una mustakabali mzuri.

Prof. Mucavele alisema lengo lake la kuitembelea China ni kufahamu mkakati na uzoefu wa China wa kujiendeleza, kuimarisha ushirikiano kati ya NEPAD na China, kubadilishana maoni na China kuhusu kazi za maandalizi ya mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, na kuanzisha uhusiano wa moja kwa moja kati ya sekretarieti ya NEPAD na ofisi ya sekretarieti ya China. Prof. Mucavele alisema China imepata ongezeko kubwa la uchumi, na nchi za Afrika pia zinapata maendeleo mazuri.

Tarehe 12 alasiri Julai Bi. Xu Jinghu na Prof. Mucavele walisaini kumbukumbu kati ya sekretarieti ya kamati inayoshughulikia utekelezaji wa mipango ya baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika na ofisi ya sekretarieti ya NEPAD kuhusu kuimarisha mazungumzo na ushirikiano.

NEPAD ni mpango uliotungwa na kutekelezwa na nchi za Afrika zenyewe kwa ajili ya kuendeleza uchumi na jamii, hii ni mara ya kwanza kwa ofisa mkuu mtendaji wa ofisi ya sekretarieti ya NEPAD kufanya ziara nchini China. Licha ya Beijing Prof. Mucavele na ujumbe wake pia ulitembelea mkoa wa Sichuan na mji wa Shanghai kuangalia hali ya miundo mbinu ya huko, miradi ya kilimo, maji, kinga na tiba ya maradhi, utoaji mafunzo ya kazi za ufundi na elimu iliyotolewa kwenye mtandao.

Tarehe 8 Julai mwaka 2006, wizara ya mambo ya nje ya China na kundi la mabalozi wa nchi za Afrika nchini China walifanya tafrija kwenye hoteli ya Diaoyutai mjini Beijing. Mjumbe wa taifa wa China Bwana Tang Jiaxuan na waziri wa mambo ya nje wa China Bwana Li Zhaoxing walishiriki kwenye tafrija hiyo.

Bw. Li Zhaoxing alipotoa hotuba alisema mwaka huu ni mwaka wa kuadhimisha miaka 50 tangu uhusiano wa kibalozi kati ya China na Afrika uanzishwe, hivyo ni muhimu sana katika historia ya uhusiano kati ya China na Afrika. Muda sio mrefu uliopita rais Hu Jintao wa China na waziri mkuu Wen Jiabao kwa nyakati tofauti walitembelea nchi 10 za Afrika na kufikia maoni mengi ya pamoja na viongozi wa nchi mbalimbali za Afrika kuhusu namna ya kusukuma mbele ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta mbalimbali. Katika nusu ya pili ya mwaka huu, mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika utafanyika mjini Beijing, viongozi wa China na Afrika watapata fursa nyingine ya kujadiliana kuhusu jinsi ya kujenga na kukuza uhusiano mpya wa kimkakati na kiwenzi.

Bw. Li Zhaoxing alitoa pongezi kwa kufanikiwa kwa mkutano wa 7 wa wakuu wa Umoja wa Afrika akieleza kuwa, China itaendelea kama ilivyofanya siku zote kuunga mkono juhudi za Afrika katika kuleta amani na maendeleo.

Kaimu kiongozi wa kundi la mabalozi wa nchi za Afrika nchini China, ambaye pia ni balozi wa Togo nchini China Bwana T. Ama alipozungumza kwenye tafrija hiyo alisifu sana urafiki kati ya China na Afrika, alitoa shukrani kwa serikali ya China na watu wake kwa kutoa misaada kwa nchi za Afrika katika kujipatia uhuru, amani na maendeleo. Pia alipongeza mapendekezo yaliyotolewa na China ya kukuza kikamilifu uhusiano wa kirafiki kati ya China na Afrika.