Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-17 15:31:04    
Mchoraji mashuhuri wa China Bi. Liu Shuqin

cri

Mto Huanghe, ambao ni moja ya mito mikubwa nchini China, Wachina pia wanauita "Mto Mama". Mto huo unaanzia kwenye Uwanda wa Juu wa Qinghai-Tibet, magharibi mwa China, na kutiririka kwenda mashariki hadi kuingia baharini. Mabonde ya mto huo yalikuwa ni chimbuko la utamaduni wa kale wa China. Wasanii wengi wa enzi mbalimbali za China walieleza upendo wao kwa mto huo kwa njia mbalimbali, mchoraji Bi. Liu Shuqin ni mmoja kati ya wasanii hao. Alitueleza, "Kulikuwa na maonesho ya picha za kuchorwa, niliambiwa nipeleke picha zangu kwenye maonesho hayo, lakini nilikuwa na wasiwasi kama picha zangu zitafaa. Kutokana na kuona aibu, picha zangu zilipelekwa na watu wengine badala yangu. Lakini baadaye niliambiwa picha zangu zimeshinda tuzo ya kwanza katika maonesho hayo. Sikuamini masikio yangu, nilidhani walinitania, lakini ni kweli kabisa. Ufanisi huo wa mara yangu ya kwanza ulinitia sana moyo."

Bi. Liu Shuqin, mwenye umri wa miaka 50, alipokumbuka tuzo hiyo aliyopata miaka kadha iliyopita alisema alikuwa na bahati sana. Kuna usemi mmoja wa Kichina usemao, "Bahati njema humwangukia mtu anayejitayarisha". Bi. Liu Shuqin alisema alitunukiwa kwa bahati tu, lakini wengine wanaona anastahili kupewa sifa hiyo, kwani toka alipokuwa mtoto alikuwa na tumaini la kuwa mchoraji mkubwa na kwa ajili ya kutimiza tumaini hilo alifanya jitihada bila kulegalega, kwa hiyo yeye kupata tuzo lilikuwa ni jambo la kawaida, kama isingekuwa wakati huo basi angepata siku nyingine.

Liu Shuqin alizaliwa katika mji wa Zhumadian karibu na Mto Huanghe. Katika miaka ya 60 ya karne iliyopita, alikuwa kama watu wa rika yake kwamba alipelekwa vijijini kulima kwa kuitikia wito wa taifa ili ajisogeze karibu na wakulima kifikra. Bi. Liu Shuqin alisema, "Mama yangu ni mchoraji, ninapenda uchoraji tangu nilipokuwa mtoto kutokana na kuathiriwa naye. Katika miaka ambapo wanafunzi walipelekwa na kufanya kazi vijijini, nilikuwa natumia muda wa mapumziko kuchorachora mandhari na hali ya maisha, kwa hiyo nimetunza michoro mingi ambayo baadaye imekuwa chanzo cha kuchora picha zangu."

Katika miaka ya 70 Bi. Liu Shuqin alipata nafasi ya kusoma katika idara ya uchoraji ya Chuo Kikuu cha Mkoa wa Henan, hili ni jambo alilotamani sana. Alipokuwa katika chuo hicho alitumai kwamba baada ya kumaliza masomo angeweza kupewa kazi inayohusiana na uchoraji, lakini hali ilikuwa kinyume na alivyotaka, alipewa kazi katika idara ya utamaduni. Kazi za kiofisi zilimzonga kila siku. Lakini hata hivyo alijitahidi kupata nafasi za kuchora picha.

Mwishoni mwa miaka ya 70 China ilianza kufanya mageuzi ya kiuchumi, sera za mageuzi zilimpatia uhuru wa kuchagua kazi anayoipenda, watu wengi wameacha mtazamo kuwa kufanya kazi katika idara za kiserikali kuna mapato ya uhakika na kuchagua kazi nyingine walizozipenda. Mwaka 1997 Bi. Liu Shuqin aliacha kazi yake kwenye idara ya utamaduni na alikuja peke yake mjini Beijing kufuatilia ndoto yake ya kuwa mchoraji mkubwa. Alisema,

"Mwaka 1997 nilikuja Beijing na kujifunza kuchora picha kutoka kwa wachoraji wakubwa wa picha za mtindo wa Kichina, Wang Wenfang na Qi Shi, na mada ya picha nilizofundishwa ni mandhari ya Mto Huanghe. Katika miaka mingi iliyopita, picha nilizochora ni za mandhari ya mto huo tu, nikiwa na mzigo mzito mgongoni nilisafiri kufuatia mto huo toka mwanzo hadi mwisho kwa kilomita 5,640, na niliwahi kwenda mara kadhaa kwenye delta ya mto huo na chanzo cha mto huo kwenye Uwanda wa Juu wa Qinghai-Tibet ili nikusanye nyenzo na kuchora picha baadaye.

Bi. Liu Shuqin ni mchoraji wa picha za mandhari ya kweli, na picha zake ni za kimaumbile na si za kubuniwa. Aliunganisha mtindo wa uchoraji wa Kichina na mtindo wa uchoraji wa Kimagharibi. Picha zake za "Mandhari ya Autumn ya Mto Huanghe" na "Mandhari ya Spring ya Mto Huanghe" zinasifiwa sana na wachoraji wenzake.

Kutokana na Mto Huanghe kuwa mrefu na unapita kwenye maeneo mengi, mandhari huwa tofauti ikifuatia majira tofauti na hali ya hewa tofauti. Mto huo unapokuwa katika majira ya kujaa maji, maji yanakimbia kwa kasi, na katika majira ya maji machache maji yanakwenda pole pole, kwenye mwanzo wa mto maji ni safi na kwenye mwisho wa mto maji yanachafuka kwa matope, katika majira ya Autumn mandhari ni ya aina nyingi na katika majira ya baridi mandhari inaonekana ya baridi. Bi. Liu Shuqin anaona mandhari tofauti kwenye maeneo ya mto huo ni kama kiumbe chenye hisia tofauti za furaha na hasira, huzuni na uchangamfu. Alisema, "Kila mara nilipokwenda kwenye Mto Huanghe nilipata hisia tofauti, na kila nilipokwenda mara nyingi zaidi nilijihisi niko karibu zaidi na mto huo. Nilipochora mandhari ya mto huo niliona kama damu yangu imechanganywa na maji ya mto huo, na inachemka kama maji yake yanayokimbia."

Picha za Liu Shuqin zilipata tuzo mara nyingi katika maonesho ya kitaifa nchini China na ziliwahi kufanya maonesho ya mzunguko katika nchi za nje. Picha zake za "Mandhari ya Mto Huanghe Mwezi Septemba" na "Mto Huanghe Unaokimbia na Matope" zimehifadhiwa katika jumba la makumbusho. Bi. Liu Shuqin anaona kwamba yeye ni binti wa Mto Huanghe, atakuwa na safari ndefu kabla ya kuweza kuonesha mandhari ya mto huo vilivyo. Alisema, "Ingawa nimefanikiwa kwa kiasi kikubwa, lakini niko mwanzoni tu katika safari yangu ya usanii. Sijali sana tuzo, pesa au kitu chochote kingine, muhimu ni kuchora kila picha kwa makini na nitumie akili kwenye kila mchoro."

Hivi sasa, Liu Shuqin amepiga picha elfu kumi kadhaa za mandhari ya Mto Huanghe kwa kamera, na amechora rasimu za mandhari ya mto huo elfu kumi kadhaa. Alisema, kuchora picha ni jukumu lake maishani. Huenda leo anachora ndani ya chumba chake na kesho atabeba mzigo wake na kwenda kutafuta msukumo wa kuchora picha nyingine kando ya Mto Huanghe.

Idhaa ya kiswahili 2006-07-17