Katika ujenzi wa reli ya Qinghai-Tibet nchini China kuna matatizo matatu ambayo hayakuweza kuepukika, nayo ni udongo ulioganda, upungufu wa hewa ya oksijeni katika uwanda wa juu na ikolojia dhaifu. Kati ya matatizo hayo matatu, tatizo la udongo ulioganda ni kubwa zaidi. Hivi sasa ujenzi wa reli hiyo umekamilika na kuanza kutumika kwa majaribio, hii inamanisha kwamba China imetatua tatizo la udongo ulioganda.
Imefahamika kwamba udongo ulioganda katika majira ya baridi ni mgumu kama barafu, na kadiri nyuzi za jotoridi zinavyoshuka ndivyo udongo huo unavyozidi kutanuka, na msingi wa reli pia unainukainuka, katika majira ya joto, kadiri joto linavyoongezeka ndivyo udongo ulioganda unavyozidi kuyeyuka na kuufanya msingi wa reli uwe na mashimo mashimo. Mabadiliko hayo yanatokea kufuatana na mzunguko, msingi wa reli utakuwa laini na mashimo mashimo na kuleta hatari ya kutokea kwa ajali.
Wataalamu walieleza kwamba ingawa hali ya udongo ulioganda pia inatokea katika nchi za Canada na Russia, lakini kutokana na nchi hizo kuwa katika sehemu zenye baridi kali, udongo huo hauyeyuki. Lakini udongo ulioganda katika nyanda za juu za Qinghai-Tibet uko katika latitudo ya chini, mwinuko mkubwa na jua kali, hali yake inabadilika badilika kufuatana na majira.
Kutokana na hali hiyo ya udongo, katika kilomita 111 za reli hiyo limejengwa tuta lisilo la kawaida, yaani chini ya tuta hilo yamewekwa mabamba madogo ya mawe kwa maki maalumu na juu yake ni msingi wa reli uliotengenezwa kwa udongo. Tuta hilo lenye mabamba mdogo ya mawe kwa chini linaloweza kupitisha hewa ni uvumbuzi uliofanywa na China. Ni hatua nzuri ya kudhibiti udongo ulioganda, yaani katika majira ya baridi unaweza kuondoa joto la ardhini, na katika majira ya joto inakinga joto la nje.
Daraja lenye urefu wa kilomita 11.7 limejengwa kwenye mto wa Qingshuihe. Daraja hili limepita juu ya sehemu ya udongo ulioganda. Kujenga daraja refu badala ya kutandika reli moja kwa moja kwenye udongo ulioganda pia ni hatua iliyotumika katika ujenzi wa reli hiyo ili kukwepa tatizo la udongo ulioganda. Kwenye njia ya reli ya Qinghai-Tibet madaraja kama hilo jumla yalijengwa kilomita 156.7, ambayo ni kiasi cha robo ya sehemu yote ya udongo ulioganda unapopiti reli hiyo. Imefahamika kuwa ujenzi kabambe kama huo wa madaraja badala ya kutandika reli kwenye ardhi moja kwa moja pia ni mara ya kwanza kutokea duniani.
Pamoja na hayo, kwenye pande mbili za reli inayopita kwenye sehemu ya udongo ulioganda kuna safu mbili za mabomba ya chuma yenye kipenyo cha sentimita 15 na urefu wa mita mbili. Hayo ni mabomba ya kuondoa joto ardhini, lakini hayawezi kuleta joto ardhini kutoka nje. Kazi ya mabomba hayo ni kama kiyoyozi, yanaweza kuhakikisha hali ya ya udongo ulioganda isibadilike.
Mhandisi mkuu wa ujenzi wa reli ya Qinghai-Tibet Bw. Huang Difu alisema, hatua mbalimbali zimechukuliwa katika ujenzi wa reli ya Qinghai-Tibet kwa mujibu wa hali tofauti ya udongo ulioganda, na hatua hizo zimehakikisha ubora wa reli hiyo, kwenye reli hiyo garimoshi linaweza kwenda kwa kasi ya kilomita 120 kwa saa.
Idhaa ya kiswahili 2006-07-20
|