Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-21 18:31:34    
Wanafunzi wa Uganda wanaosoma nchini China wafanya kongamano Beijing

cri

Chama cha wanafunzi Waganda wanaosoma nchini China (USAC) tarehe 16 mwezi Julai kiliandaa kongamano lililofuatiwa na sherehe ya kuwakaribisha wanafunzi wa Uganda wanaokuja nchini China kwa masomo na kuwaaga wanafunzi waliohitimu masomo yao nchini China.

Katika Kongamano hilo lililofanyika katika hotel ya Chingari iliyopo mjini Beijing, mada na hotuba mbalimbali zilitolewa na kujadiliwa. Wanafunzi hao walijadili kwa kina umuhimu wa elimu na ujuzi wanaopata wanafunzi wa Uganda nchini China ikilinganishwa na hali halisi ya nchini Uganda. Katika mada hiyo maoni mbalimbali yaliyotolewa yalisifu elimu inayotolewa na vyuo vikuu vya China. Wanafunzi hao pia walijadili hali ya maisha yao nchini China na walitoa maoni yao kuhusu ushirikiano kati ya China na Uganda ulivyo na unavyoendelea hivi sasa. Majadiliano hayo yalifuatiwa na chakula cha usiku pamoja na burudani ya muziki wa kiafrika.

Mwongozaji wa mada kuhusu elimu nchini China alikuwa ni Bw Alex Asimwe ambaye ni mhitimu wa shahada ya pili mambo ya kompyuta kutoka chuo kikuu cha Hunan. Bw. Alex alisema kuwa, elimu inayotolewa nchini China ni ya kiwango cha juu na inaweza kutosheleza na kukidhi mahitaji halisi ya fani husika za Uganda ikiwemo ya Kompyuta. Bw. Alex alisema anaridhika sana na kiwango cha elimu aliyopata nchini China na anategemea kuutumia ipasavyo ujuzi na utalaamu huo kwa maendeleo ya watu wa Uganda na bara zima la Afrika. Matarajio yake ni kuwa mhadhiri katika chuo kikuu cha makelele nchini Uganda.

Akizungumzia maisha ya wanafunzi wa Uganda nchini China, Bwana Alex Asimwe alisema, Wachina ni watu wazuri na wakarimu, katika muda wote alioishi hapa China alikuwa amepewa ushirikiano wa aina mbalimbali. Alisema hakujisikia upweke nchini China, bali anajihisi kama yupo nyumbani.

Bw. Keneth W. Buyinza ni mwanafuzi wa shahada ya kwanza ya udaktari wa binadamu katika Chuo Kikuu cha Beijing, yeye pia ni mwenyekiti wa chama cha wanafunzi Waganda wanaosoma nchini China. Bwana Keneth aliishukuru sana serikali ya China kwa udhamini wa masomo inaowapatia wanafunzi wa Uganda. Alisema:

Baada ya kuishi nchini China kwa miaka kadhaa, Bw. Kenethy Buyinza anaweza kuzungumza vizuri lugha ya Kichina. Alisema:

"Naishukuru sana China kwa kupata fursa ya kusoma hapa China, uhusiano mzuri wa kirafiki kati ya China na Uganda umetupatia sisi fursa nzuri ya kuja China kupata elimu na ujuzi wa aina mbalimbali, natumaini kuwa wanafunzi wa Uganda na nchi za Afrika mashariki watatumia ujuzi wanaoupata hapa China kuchangia ujenzi wa mataifa yao."

Wakizungumzia uhusiano kati ya China na Uganda, Bwana Eleza ambaye ni mwanafunzi wa shahada ya pili katika Chuo Kikuu cha Beijing alisema, anafurahishwa sana na uhusiano uliopo kati ya China na Uganda, matunda ya uhusiano huo ni pamoja na udhamini wa masomo alioupata yeye. Alsema kuwa biashara kati ya Uganda na China imekuwa ikiendelea kukua siku hadi siku, ambapo Waganda wengi sasa wamekuwa wakija China kununua bidhaa na makampuni ya kichina yamekuwa yakienda Uganda kuwekeza. Bw Eleza alisema

Msichana Shiera amekuwa nchini China kwa miaka zaidi ya miwili, mwanzoni alikuwa hajui kuongea Kichina hata kidogo, hivyo ilikuwa si rahisi kwake kuishi nchini China, lakini walimu na marafiki wa China walimtendea vizuri na kumpa msaada mwingi. Sasa anaweza kuongea Kichina, hivyo anasikia vizuri kuishi na kusoma nchini China. Anaishuruku sana serikali ya China kwa kumpa fursa hiyo ya kusoma nchini China na pia anashukuru ukarimu wa China kwa msaada wote aliopewa.

Naye Mhadhiri kutoka katika kitengo cha tiba ya binadamu katika Chuo Kikuu cha Beijing aliyealikwa kuhudhuria sherehe hizo alisema,

"Mwaka huu wanafunzi wanne wa Uganda wanasoma katika idara yetu, baadhi yao wamemaliza masomo na kurudi nchini Uganda, wengine wameenda katika vyuo kikuu vingine kuendelea na masomo ya shahada ya pili, na baadhi yao bado wako katika hospitali wakiwa katika mafunzo ya vitendo. Wanafunzi hao wote wanajifunza kwa bidii, kwa mfano wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Sars hapa Beijing, wanafunzi wengi waliokuwa wanafanya mafunzo ya vitendo hospitalini walirudi shuleni kutokana na hofu ya kuambukizwa, lakini mwanafunzi mmoja kutoka Uganda anayeitwa Msenga alipoona upungufu wa madaktari hospitalini alibaki kwa hiari. Kitendo chake cha kujitolea kilisifiwa na madaktari wa hospitali na walimu wa chuoni."

Hili ni kongamano la kwanza la wanafunzi wote wa Uganda wanaosoma nchini China kufanyika nchini China, ambapo wanafunzi wa Uganda walioko katika sehemu mbalimbali nchini China kama vile Beijing, Hunan, Tianjin, Shandong na Nanjing walihudhuria kongamano hilo.

Mgeni rasmi katika sherehe hizo alikuwa balozi wa Uganda nchini China ambaye aliwakilishwa na Mr. Jack Wamai.