Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-24 14:33:43    
Mwigizaji filamu Wang Fuli

cri

Bibi Wang Fuli ni mwigizaji mashuhuri wa filamu, alipitia vipindi kadhaa vya maendeleo ya filamu nchini China na alifanikiwa kuigiza wahusika wa aina tofauti ambao waliwaingia sana akilini watazamaji katika filamu.

Bibi Wang Fuli ana umri wa miaka 57, lakini bado anaonekana kijana. Yeye ni mtu mwema, mkarimu na mchangamfu. Baba yake ni shabiki wa opera ya Kibeijing, kutokana na kuathiriwa na baba yake, Wang Fuli pia alipenda opera hiyo toka alipokuwa mtoto na alipokuwa na umri wa miaka 11 alijiunga na shule ya opera ya Kibeijing. Kutokana na werevu wake alipata maendeleo kwa haraka na baada ya kuhitimu alijiunga na Kundi la Opera ya Kibeijing mkoani Jiangsu na akawa mchezaji wa kulipwa.

Ingawa Wang Fuli alipenda sana kuangalia sinema lakini hakufikiria kwamba siku moja angeweza kuwa mwigizaji wa filam. Miaka ya 70 ya karne iliyopita, Studio ya Filamu ya Mji wa Changchun ilitaka kupiga filamu ya "Barabara ya Kufikia Maisha Bora", na ilichagua waigizaji kati ya wachezaji wa michezo ya sanaa katika miji mingi, kwa bahati Wang Fuli alichaguliwa. Katika miaka hiyo China ilitengeneza filamu chache sana, kuweza kuchaguliwa kuwa mwigizaji wa filamu ilikuwa ni bahati sana. Ingawa kwake ilikuwa ni mara ya kwanza kuwa mwigizaji wa filamu lakini mara moja akawa mtu aliyejulikana kwa Wachina wengi kutokana na uhodari wake wa uigizaji katika filamu hiyo. Kucheza katika filamu na kucheza opera ya Kibeijing jukwaani ni tofauti kabisa. Wang Fuli alisema, "Opera ya Kibeijing ni mchezo wa jukwaani, lakini uigizaji filamu ni kuonesha hali ilivyo ya kimaisha. Mwanzoni nilipocheza nilikuwa kama nilivyocheza jukwaani, mwongozaji wa filamu mara kwa mara alinikumbusha, sikutumia muda mrefu kubadilisha mazoea yangu."

Miaka kadhaa baadaye, kwenye filamu nyingine iitwayo "Mkulima Goigoi Niu Baisui" Wang Fuli aliigiza kama mwanamke mmoja mkali. Katika filamu hiyo kuna sehemu moja ambayo aligombana na mwanamke mwingine. Ili aweze kuigiza vizuri alikwenda vijijini kuanglia jinsi wakulima wa kike wanavyogombana na mwishowe aliigiza vizuri sana sehemu hiyo. Kutokana na ufanisi wake wa kumwigiza vizuri mwanamke huyo alisifiwa na watazamani na alipata tuzo ya uigizaji wa mwanamke huyo.

Filamu ya "Maajabu katika Sehemu ya Tianyunshan" iliyoendeshwa na mwongozaji mkubwa wa filamu Xie Jin ni filamu muhimu katika historia ya filamu ya China. Filamu hiyo ilipigwa mwanzoni mwa mageuzi ya uchumi nchini China mwaka 1980, ikieleza jinsi harakati za fikra za kushoto kupita kiasi zilizoenea kote nchini China zilivyomsibu msomi mmoja mwanamke. Kwenye filamu hiyo kuna sehemu moja ya kubusiana. Sehemu kama hiyo ilikuwa inazungumzwa sana katika jamii, kwa sababu wakati huo kulikuwa hakuna kitendo hicho katika filamu kwa miaka 30 hivi. Lakini jambo asiloweza kulisahau katika filamu hiyo ni kupigwa kofi la uso na mumewe. Alisema, "Mara ya kwanza nilipopigwa nilisikia shavu langu linawaka, lakini nilivumilia kwa ajili ya kuonesha hali ilivyo, lakini sikutegemea kwamba mwendeshaji filamu akasema: Pumzika kidogo kisha utaendelea, nilipigwa bumbuazi. Mara ya pili nilipigwa kwa nguvu hata nilishindwa kusimama, nikasepetuka mpaka nikashikilia meza."

Miaka kadhaa baadaye, alipokuwa anaigiza kwenye filamu ya "Mzee Xu Mao na Mabinti Zake" aliumwa na mbwa. Hili jambo ambalo analikumbuka sana. Hii ilikuwa ni filamu ya kuonesha maisha ya wakulima, filamu hiyo ilipopigwa vijijini Wang Fuli aliumwa na mbwa wakati alipobadilisha nguo, damu ilimtiririka, na baada ya kushonwa na kupigwa sindano, aliendelea kuigiza.

Wang Fuli aliigiza kwa mafanikio wahusika wengi wa aina tofauti katika filamu. Katika filamu ya "Jua Linachomoza" iliyotengenezwa kwa mujibu wa tamthilia yenye jina hilo Wang Fuli aliigiza kama kahaba mmoja aliyekuwa katika miaka ya 30 ya karne iliyopita. Ili kumwigiza kahaba anayevuta sigara alipaka meno yake kwa rangi manjano, na wakati akiigiza hakuweza kunywa maji ili rangi isitoke. Kwa ajili ya kuigiza kahaba huyo alijizoeza kuvuta sigara, lakini baadaye alizoea kuvuta sigara. Kuhusu jambo hilo Wang Fuli alisema, "Nilipoanza kuvuta sigara niliona kichefuchefu, lakini baada ya kuzoea kila baada ya chakula ilikuwa ni lazima nivute sigara moja nipate raha mstarehe, na kila baada ya kumaliza kazi ya siku na kuoga pia nilikuwa navuta sigara moja na kuona uchovu umenitoka. Lakini mchezaji lazima atunze ngozi yake na kuacha sigara, mwanzoni nilisikia vibaya sana, lakini hatimaye nimefanikiwa."

Mume wa Wang Fuli pia ni mwigizaji wa filamu, lakini hakujulikana kama Wang Fuli, maisha yao ni ya furaha. Wang Fuli alianza kujulikana katika miaka ya 80, lakini mpaka sasa anashikilia kuishi maisha ya kawaida kabisa. Hivi sasa amekuwa na wajukuu akifurahia maisha yake ya kifamilia, mara moja moja tu anashiriki kwenye uigizaji wa filamu fulani.

Idhaa ya kiswahili 2006-07-24