Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-25 15:30:15    
Wanauchumi wa China watajirika kutokana na uvumbuzi

cri

Hivi sasa uchumi wa China unakuzwa kwa haraka, watu wanasikia habari kuhusu watu wengi wanaotajirika au kuwa mashuhuri kwa usiku mmoja. Katika kipindi hiki cha leo nitawafahamisha vijana wawili waliojiajiri katika miaka ya 80 ya karne iliyopita. Vijana hao ni wenye umri wa miaka 24 au 25 hivi, lakini walipewa mikopo ya kuwekeza vitega-uchumi kutokana na uvumbuzi wao. Hivi sasa wamekuwa matajiri wenye Yuan milioni kumi kadhaa hata mia kadhaa, hivi sasa wakati vijana chipukizi wenye umri wa miaka kama wao, wanapoanza kuingia katika jamii, hao wamekuwa mahiri katika masoko ya biashara.

Mao Kankan ana umri wa miaka 22, ni kama vijana wengi wa mijini, moja ya burudani anayopenda sana ni kwenda kuimba katika jumba la Karaoke. Lakini baada ya kufika ofisini anaonekana kama ni mtu mwingine kabisa, yeye ni ofisa mtendaji wa kwanza wa kampuni ya kazi za viwanda ya Aihang. Jambo linalostaajabisha ni kuwa hivi sasa anaongoza kampuni ya Aihang kuwekeza Yuan za Renminbi milioni 300 kujenga kituo pekee cha michezo ya tarakimu mjini Beijing.

"Mnamo alasiri ya tarehe 28 mwezi Mei, mwaka 2010 saa 9 na dakika 58, ndege moja ya kijeshi ya nchi ya A ilitunguliwa ikiwa njiani kupeleka habari muhimu za siri, na habari hizo zikapotea. Hivyo nchi mbili za A na B zikawa na mchuano mkali wa kugombea kupata habari hizo muhimu."

Bw. Mao Kankan alikuwa akieleza mchezo alioubuni yeye pamoja na kundi lake, ambao utachezwa kwenye bustani moja ya Beijing. Wazo la kubuni mchezo huo utakaochezwa na watu ni la Bw. Mao Kankan, kwa kufuata wazo lake kila mtu anayeingia kwenye bustani anatakiwa kuvaa mavazi yanayolingana na mhusika wa mchezo. Kwa kutumia teknolojia ya mwigo (dummy) ya kisasa, hatimaye kutakuwa na watu zaidi ya 100, ambao wanashindana katika kutafuta hazina ndani ya bustani.

Mchezo wa elektroniki kubadilishwa kuwa maonesho ya watu halisi, kwa Mao Kankan ni mradi mkubwa unaoweza kutimiza tumaini lake.

"Ikiwa mambo hayo yanaweza kutendeka, baada ya miaka 5 yataweza kuleta faida ya zaidi ya Yuan bilioni 1, nimekadiria faida itakuwa Yuan bilioni 1.5."

Mao Kankan mwenye umri wa miaka 22, hajawekeza hata senti moja, lakini kutokana na wazo lake hilo, atapata karibu 20% ya hisa za mradi huo, ambao utaweza kuleta faida ya Yuan bilioni 1.5 kwa mwaka. Endapo mradi huo utatekelezwa, mali ya Mao Kankan itakuwa kubwa ajabu.

Wakati watu wengi wanashangaa kuhusu mali nyingi atakayopata Mao Kankan, tunamfahamu kijana mwingine, ambaye ana umri wa miaka karibu sawa na Mao Kankan, tofauti iliyopo ni kuwa kijana huyu alishapata mali nyingi.

Kijana huyu ni Li Xiang, ofisa mtendaji wa kwanza wa tovuti ya Mapovu. Hivi sasa anaongoza tovuti ya chombo kimoja cha habari inayotoa huduma kwa aina mbalimbali za bidhaa za teknolojia ya tarakimu. Bw. Li Xiang alipozungumzia tovuti aliyoanzisha, alisema,

"Tunatoa huduma kamili, ambayo ni ya kipekee kwa hivi sasa miongoni mwa tovuti kwenye mtandao wa Internet. Pengine tovuti yetu ni tovuti inayoweza kuunganisha vizuri web 1.0 na web 2.0, na kuweza kuleta faida pia."

Mwaka 2005, pato la tovuti ya Mapovu lilikuwa Yuan zaidi ya milioni 20, na faida ilikuwa Yuan zaidi ya milioni 10, na hisa anazomiliki kijana Li Xiang ni zaidi ya 50%.

Mafanikio waliyoyapata vijana hao wawili yanawashangaza sana watu. Lakini jambo lingine linalowashangaza watu zaidi ni kuwa vijana hao wawili wote hawana elimu ya chuo kikuu. Basi, vijana Mao Kankan na Li Xiang walifanyaje hadi kupata mafanikio makubwa ya namna hii?

Mao Kankan alikosa nafasi ya kushiriki kwenye mtihani wa kuingia vyuo vikuu kutokana na mafanikio duni katika somo la jiografia alipokuwa shule ya sekondari, halafu aliacha kabisa masomo ya shuleni. Lakini alisema kutosoma katika chuo kikuu hakukuwa na maana ndiyo mwisho wa elimu yake. MaoKankan alisema, "Wakati ule watu walithamini uthibitisho wa kampuni kubwa za kimataifa ikiwemo kampuni ya Microsoft, lakini sasa kuna thibitisho za aina nyingi, hata mtu anaweza kuziokota barabarani, lakini zilipokuwa na thamani, nilizipata nikiwa na umri wa miaka 17. Bado ninakumbuka kuwa wakati ule katika bara la Asia kulikuwa na vijana wawili wenye umri wa chini ya miaka 18, nilipata thibitisho 7 au 8 hivi, karibu nilipata uthibitisho wote."

Mafanikio ya Li Xiang kwenye tovuti ya Mapovu yanatokana na shauku yake kubwa juu ya kompyuta. Alipenda sana kompyuta tangu alipokuwa anasoma katika shule ya sekondari, na alianzisha tovuti yake katika Internet ya kutoa habari kuhusu vipuri za kompyuta.

Li Xiang hakutazamia kuwa shauku yake inaweza kuleta nafasi ya biashara, wafanyabiashara wa matangazo waliwekeza kwenye tovuti ya Li Xiang, ilikuwa kiasi cha Yuan zaidi ya 6,000 kwa mwezi. Hali hiyo iliendelea kwa miaka 3, kabla ya mtihani mkuu wa kuingia chuo kikuu, Li Xiang alifanya uamuzi muhimu wa kuacha masomo ya chuo kikuu ili apate nafasi ya kushughulikia tovuti yake.

Mao Kankan hakujali sana kuhusu kukosa nafasi ya kusoma katika chuo kikuu, isipokuwa anaona masikitiko kidogo kwa kukosa uzoefu wa kipindi hicho. Lakini Mao Kankan na Li Xiang wote wanaona kuwa vijana wakitaka kupata mafanikio, kitu muhimu siyo kama kuwa shahada au la, bali ni kuona kama ameweka lengo lake au la, na kama amefanya juhudi za kutosha kutimiza lengo lake.

Ingawa Mao Kankan na Xi Xiang wamepata mafanikio ambayo vijana wengine wa rika hilo huenda hawawezi kuyapata, lakini bado kuna watu wengi ambao wana mashaka kuhusu Mao Kankan na Li Xiang kama wanaweza kusimamia vizuri kampuni zao. Vijana wenye umri wa miaka 20 na kidogo, ambao wanamiliki mali nyingi, lakini hawakupata elimu ya juu, wana uwezo wa kuepusha kampuni zao na mambo ya hatari katika masoko yaliyojaa "mawimbi na upepo mkubwa"? Li Xiang alisema, katika muda wa miaka 8 iliyopita tangu aanze kushughulikia mambo ya biashara, amepambana na shida nyingi, na amepata uzoefu muhimu wa usimamizi. Alisema, "Nilifanya makosa mengi, na nilipatwa na shida za aina mbalimbali. Lakini niliweza kuzitatua vizuri, tena nimekuwa na uwezo wa kutatua matatizo hayo, hivyo nimepanda ngazi, ninaona hilo ni jambo zuri, na sioni mambo kama hayo ni mabaya."

Kwa Mao Kankan na Li Xiang, njia yao ya mbele ni ndefu sana. Sasa hatuwezi kutabiri mustakabali wao na wa kampuni zao. Lakini matokeo ya baadaye, kwa kundi la vijana wanaotafuta mali, linalowakilishwa na Mao Kankan na Li Xiang, yatabadilisha kanuni za shughuli za masoko ya jadi ya China, na kuongeza uvumbuzi mpya wa mali.

Idhaa ya kiswahili 2006-07-25