Katika hali ya kawaida lugha ya kiingereza ni chaguo la kwanza kwa watu wengi wanaotaka kujifunza lugha ya kigeni, na hivi sasa kiingereza bado ni lugha muhimu ya kimaitaifa. Lakini pamoja na kuinuka kwa uchumi na hadhi ya China duniani, watu wengi duniani wameanza kujifunza lugha ya kichina kama lugha ya pili. Takwimu husika zinaonesha kuwa, hivi sasa watu zaidi ya milioni tatu duniani ambao lugha yao ya kwanza si kichina wanajifunza Kichina, wengi wao wanaamini kuwa uwezo wa kuongea lugha ya Kichina una manufaa kwa watu binafsi na kwa mashirika katika ushindani wa kimataifa.
Bi. Kerstin Storm ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Minstel cha Ujerumani. Tangu alipokuwa mwanafunzi katika shule ya sekondari, alivutiwa sana na China na lugha ya Kichina. Lakini wakati huo somo la lugha ya Kichina lilikuwa halifundishwi katika shule hiyo, hivyo tumaini lake la kujifunza kichina halikutimizwa. Baada ya kujiunga na chuo kikuu, Kerstin Storm alichagua somo la lugha ya Kichina. Hivi sasa amejua kuzungumza kichina. Alisema:
"hivi sasa kuna fursa nyingi nchini China, makampuni mengi ya Ujerumani yameanzisha matawi nchini China, uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili umekuwa wa karibu zaidi. Hivyo nadhani kujua kuzungumza lugha ya Kichina kunasaidia kupata ajira."
Kerstin Storm alisema, watu wengi zaidi wa Ujerumani wameanza kujifunza Kichina. Wakati alipojiunga na chuo kikuu, katika kila darasa la somo la lugha ya Kichina kulikuwa na wanafunzi 10 tu, na hivi sasa kila darasa lina wanafunzi 40.
Kwa kweli, lugha ya Kichina ni lugha ngumu, hasa kwa watu wa nchi za magharibi, matamshi na maandishi ya kichina yanawatatiza sana wanafunzi wa nchi za magharibi wanaojifunza Kichina. Lakini kutokana na China kuzafungua mlango zaidi kwa nje na kuwa na ongezeko endelevu la kasi la uchumi, mawasiliano kati ya China na dunia yamepanuliwa zaidi, na watu wengi wa nchi za nje wameanza kuwa na hamu ya kujifunza kichina.
Bi. Wang Chao ni mwalimu anayefundisha kichina nchini Korea ya Kusini. alisema, hivi sasa watu wengi wa nchi hiyo wanapenda kujifunza kichina kama lugha ya pili. Alisema:
"nakumbuka bibi mmoja anayekuwa na kazi nyingi, kulikuwa na baadhi ya wakati ambapo alikuwa anachelewa kuja darasani, wakati alipofika darasani hata alikuwa anatokwa na jasho jingi usoni. Ingawa alikuwa na shughuli nyingi, lakini kila mara alikuwa anamaliza mazoezi yake. Naona watu wa Korea ya Kusini wanapenda zaidi lugha ya Kichina na kuvutiwa na China, wengi wao wanasema wanataka kufanya kazi au kutembelea nchini China. Nafurahi sana kupata fursa hiyo kujenga daraja kwa watu wa nchi hiyo kufahamu na kuelewa China kupitia kazi yangu."
Hivi sasa China ni mwenzi muhimu wa biashara kwa Korea ya Kusini, katika miaka mitano iliyopita, idadi ya watu wa nchi hiyo waliokuwa wanajifunza lugha ya Kichina imeongezeka kwa asilimia 66. hivi sasa wanafunzi laki kadhaa wa sekondari na vyuo vikuu nchini humo wanajifunza kichina. Miongoni mwa wanafunzi wa nchi za nje wanaosoma nchini China, idadi ya wanafunzi wanaotoka Korea ya Kusini inachukua nafasi ya kwanza, ikiwa ni asilimia 40 ya idadi ya jumla ya wanafunzi wote wa nchi za nje. Kwa watu wengi wa Korea ya Kusini, kuweza kuzungumza kichina kunawasaidia kwa kiasi kikubwa kupata ajira. Si nchini Korea ya Kusini tu, kwenye sehemu nyingine barani Asia na Ulaya na Marekani, lugha ya kichina kwa kiasi fulani pia imekuwa lugha mpya ambayo watu wanahitaji kuifahamu. Watu wengi zaidi wameona kuwa, lugha ya Kichina ni muhimu na imehusisha mustakabali wao wenyewe na maendeleo ya uchumi wa China.
Kutokana na kuendelea kuongezeka kwa nia ya kujifunza Kichina, serikali za nchi mbalimbali pia zimeanza kutilia maanani kazi ya elimu ya lugha ya Kichina. Ofisa wa idara ya elimu na mafunzo ya Viet Nam Bw. Vu Minh Tuan alisema:
"hivi sasa wanafunzi wengi wa Viet nam wanapenda kujifunza Kichina. Mbali na vyuo vikuu, serikali ya nchi hiyo pia imeweka taasisi nyingi za lugha ya Kichina, wanafunzi wengi wanatumia nafasi yao baada ya masomo kujifunza Kichina."
Ili kupima kiwango cha kutumia lugha ya Kichina kwa watu wa nchi za nje, kuanzia mwaka 1991, China ilianzisha mtihani wa kiwango cha uwezo wa lugha ya Kichina kwa watu ambao kichina si lugha yao ya kwanza. Hivi sasa vituo zaidi ya 150 vya mtihani huo vipo katika nchi 34 duniani, hali hiyo imewapa urahisi watu wa nchi mbalimbali wanaojifunza Kichina washiriki kwenye mtihani huo. Watu wa nchi za nje waliopewa hati ya ngazi ya uwezo wa lugha ya Kichina, wanaweza kuomba kusoma katika vyuo vikuu vya China.
Bw. Mu Xiaolong kutoka Marekani ameshiriki kwenye mtihani wa kiwango cha uwezo wa lugha ya kichina kwa sababu hiyo. Alisema:
"nashiriki kwenye mtihani huu kwa sababu nataka kujua kiwango changu kwa uwezo wa lugha ya Kichina; tena, mtihani huo ni wa kitaifa wa China, kama nikitaka kusoma shahada ya pili katika vyuo vikuu vya China, lazima nifikie ngazi ya sita katika mtihani huo."
Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na nia ya kujifunza kichina kuongezeka kote duniani, tatizo la upungufu wa walimu wa Kichina linaonekana zaidi. Katika hali hiyo, serikali ya China imeamua kuanzisha vyuo vya Confucious katika nchi za nje kama idara za kutoa mafunzo ya Kichina na kueneza utamaduni wa China katika nchi hizo. chuo cha kwanza cha Confucious duniani kilianzishwa mwaka 2004nchini Korea ya Kusini.
Mpaka hivi sasa, vyuo na madarasa zaidi ya 80 ya Confucius yameanzishwa katika nchi na sehemu 36 kote duniani. Imefahamika kuwa, hivi sasa vyuo vya Confucious vimekuwa vyombo muhimu kwa watu wa nchi za nje kujifunza Kichina na kufahamu China.
Aidha, idara husika zinashirikisha vyuo vikuu na idara husika za uchapishaji kufanya uchunguzi kuhusu mpango wa masomo ya Kichina katika nchi kadhaa za Marekani, Uingereza na Ufaransa, ili kurekebisha vitabu vya kiada vya Kichina, na kutafiti na kueneza vyombo tarakimu vya kiada vya kufundishia lugha ya Kichina.
Katika siku za baadaye, China pia itaendelea kupeleka watu wanaojitolea katika nchi mbalimbali kufundisha Kichina au kusaidia idara za elimu za huko kufanya kazi ya kufundisha Kichina. Serikali ya China pia itaharakisha kurekebisha mazingira na vifaa vya kufundisha Kichina, ili kutoa huduma bora kwa wanafunzi wa nchi za nje wanaokuja China kujifunza Kichina.
|