Haya msikilizaji 91.9 wa Radio China Kimataifa, leo hii katika makala ya elimu tunakutana na mwalimu wa fasihi kutoka shule ya upili wilayani Siayamu mkoani Nyansa, Kenya Bw. James Mnanga Adola, ambaye atatueleza kuhusu mambo matatu yanayohusiana na kazi za fasihi.
U: Wewe ni mwalimu wa fasihi kwenye shule ya upili, ni mambo gani hasa unayofundisha kuhusu fasihi?
A: Ndiyo, ni ukweli kwamba mimi ni mwalimu wa fasihi kwa jumla, lakini kuna kipengele maalum ambacho nahusika nacho zaidi, nacho ni ushairi. Kwa uhakika ninakienzi sana, kwa sababu naona naweza kukimudu zaidi, na pia kwa vile baadhi ya watu wanaona kuwa ni kigumu, mimi hupenda kufundisha na kuwaambia wengine kwamba si kigumu.
U: Ukisema ni kigumu una maana gani, yaani inachukuliwa kwamba ugumu mwingi sana katika ufundishaji wa ushairi, labda unatokana na nini?
A: Ushairi ni kazi ya sanaa inayotumia lugha ya Mkato. Watu wengi huzoea kutumia lugha ya mtiririko wakati wanapozungumza, kuandika, kusoma na kazi nyinginezo. Kwa vile kuna Mkato katika ushairi, basi inakuwa vigumu kuelewa maneno ambayo yameandikwa kwa Mkato. Na vilevile fikra ambazo zinaonekana kama neno la Mkato. Na vilevile ushairi unatengeneza picha na taswira, unatumia mbinu mbalimbali, ambazo zinafaa kuchambuliwa na mhakiki yoyote. Na ugumu huohuo unatokea katika uchambuzi.
U: Umetaja kuhusu kufinyanga taswira na vitu mbalimbali katika jamii. Tueleze kwa kifupi ufundishaji wa fasihi, hasa ushairi, kuwa vipi unaelezea uhalisi wa maisha kwa mwanafunzi na vilevile mpenzi wa ushairi kwa ujumla.
A: Mwanzo mshairi, mwandishi, malenga ni mwanajamii, na anapoandika anaandika kuhusu jamii, anaandika kuhusu falsafa ya jamii, mtizamo wa jamii na mwanajamii, mazoea yake, fikra zake, pamoja na hofu zake. Kwa hivyo kupitia kazi ya ushairi, unaweza ukaendeleza fikra, ukatumia lugha ya Mkato, kuzungumzia jamii, kuhusu ufisadi, kuhusu elimu na mambo mengine. Kwa hivyo unapitisha ujumbe, lakini kwa njia ya Mkato. Ingawa pia unajua kwamba hivi majuzi kumetokea wanamapinduzi, ambao wanasema kwamba ule mkato utoweke ili ushairi uwe wazi zaidi, na uweze kueleweka zaidi. Lakini wanamapokeo wale waliokuwa wakiandika ushairi wa zamani wanasema kwamba, ushairi lazima udumishe sheria za utunzi, la sivyo malenga wengi watajikuta wakitunga mashairi ambayo ni chapwa.
U: Na unasemaje kuhusu kazi zenu za ufundishaji ushairi, kuna vitabu vya kutosha vya kufundisha ushairi, ama kuna uhaba wa vitabu, na kama vipo vya kutosha labda ni vitabu gani, ambapo ninyi walimu wa ushairi mnatumia kufundishia wanafunzi fasihi ya ushairi.
A: Kwa ukweli hapo tuna tatizo kubwa. Kuna tatizo kubwa kweli kweli, kwa vile vitabu vingi vinavyochapishwa na taasisi nyingi za uchapishaji ni za sarufi, ama ni za mambo mengine ya sarufi, insha na kadhalika. Lakini wengi hawataki kuchapisha vitabu vya ushairi, havipo vingi kwa hakika nikijaribu kulinganisha, pengine robo moja pekee ya vitabu viliwahi kuchapishwa ni vya ushairi. Na pengine hapo kwa tatizo kwa sababu wanafunzi wengi hawawezi kusoma ushairi kwa vile kuna upungufu wa nyenzo za kufundishia, nyenzo za kusoma, na hilo ni tatizo kubwa, ni tatizo kubwa sana.
U: Na unafikiri ni kwa nini taasisi ya elimu nchini Kenya imeamua kuidhinisha baadhi ya vitabu vya ushairi kutahiniwa, ingechangia kwa wingi waandishi kuandika vitabu vya ushairi labda.
A: Kwa hakika ndiyo, na pili pengine ningesema kwamba baadhi ya malenga wanaotunga ushairi, hawaegemei nyanja zote, bahari zote, mbinu zote za waandishi wa ushairi katika kitabu kimoja, kwa hivyo wakati huohuo tuna vitabu vichache, lakini havijazungumzia kwa tafsiri ushairi. Pengine hapa utahitaji kutafuta mbinu moja katika kitabu kimoja na mbinu nyingine katika kitabu kingine, kwa hivyo vitabu havitoshelezi, kwa hivyo ningependa taasisi ya elimu ijaribu kuwezesha vitabu vingine zaidi vichapishwe vya ushairi, na vile vimesheheni tanzu zote za ushairi, mbinu zote za ushairi katika kitabu kimoja kinachoeleweka.
U: Umesema una raha kuwa mwalimu wa fasihi, mwalimu wa ushairi, nini kinakufanya useme kwamba leo una raha sana?
A: Ninafundisha ushairi, mwanzo pengine ningezungumzia jamii ambayo naiandikia, na ninauandikia ulimwengu. Ulimwengu ambao ninafahamu unasoma kazi yangu, utaweza kufurahishwa na hiyo kazi na kuelimisha, na vilevile kuwaondoa wanafunzi pamoja na walimu ile kasumba kwamba ushairi ni mgumu, kwa vile kwa hakika hakuna jambo rahisi duniani, kwa hivyo furaha yangu ni kwamba wakati ninapoandika ushairi, ninaandika kwa lengo la kuisaidia jamii kuweza kuisoma na kuepukana na mawazo potuvu, kwamba ushairi ni mgumu. Kufikia sasa nimeandika zaidi ya mistari 6,000 ya ushairi wa Kiswahili, na zaidi ya mashairi 100 kwa Kiingereza. Na ninazidi kuandika naiandikia jamii, na nina matumaini kwamba taasisi ya elimu na vyombo vingine vya uchapishaji vitaweza kuwa vizuri hatimaye kuitazama hiyo kazi na siku moja kuichapisha.
Idhaa ya Kiswahili 2006-07-26
|