Kutokana na Sensa iliyofanywa na serikali ya China mwaka 2000, miongoni mwa watoto waliozaliwa nchini China, uwiano wa idadi ya watoto wa kiume na wa kike ni 119 kwa 100, lakini wastani wa kiasi cha kawaida ni kati ya watoto wa kiume 103 na 107 kwa watoto wa kike 100.
Katika juhudi za kuzuia hali ya kutokuwepo kwa uwiano wa kijinsia, miaka mitatu iliyopita serikali ya China ilianzisha kampeni kubwa ya kuwafuatilia watoto wa kike. Hivi karibuni ofisa wa Kamati ya uzazi wa mpango ya taifa ya China alisema kampeni hiyo imepata mafanikio. Katika wilaya 24 zilizotangulia kutekeleza kampeni hiyo, ambazo kwa wastani idadi ya watoto wachanga wa kiume na kike ilikuwa 133.8 kwa 100, hivi sasa wastani huo umepungua hadi kufikia 119.6 kwa 100. Kutokana na mafanikio hayo, kampeni ya kuwafuatilia watoto wa kike itaenezwa kote nchini China mwaka huu.
Bibi Ding Xiufang ni mkulima anayeishi wilayani Wuwei, mkoani Anhui, mashariki mwa China, ambayo ni miongoni mwa wilaya 24 zinazotekeleza kampeni ya kuwafuatilia watoto wa kike mwaka 2003. Mama huyo aliposikia binti yake anamwita mama kwa mara ya kwanza baada ya miaka 12, alitokwa na machozi. Ili apate mtoto wa kiume, Bibi Ding Xiufang alimwacha binti yake mara baada ya kuzaliwa kwake akampelekea nyumbani kwa babu.
Je, kwa nini Wachina wengi wanathamini watoto wa kiume na kudhalilisha watoto wa kike? Wataalamu wanachambua kuwa, China bado ni nchi inayoendelea, ambapo wakulima wanategemea watoto wa kiume katika shughuli za kilimo. Sababu nyingine inayochangia kutokuwepo kwa uwiano wa kijinsia ni kuwa, wakulima wa China hawajalindwa na mfumo wa huduma za jamii, na kutokana na mtizamo wa jadi wazazi wazee wanawategemea kimaisha watoto wa kiume.
Mwaka 2003 kampeni ya kuwafuatilia watoto wa kike ilianza kutekelezwa katika wilaya ya Wuwei. Pamoja na kuwaelimisha wakulima kuwa "watoto wa kiume na wa kike wako sawa", maofisa wa uzazi wa mpango pia waliipa msaada wa kiuchumi familia ya Bibi Ding Xiufang. Bwana wa familia hiyo akitumia mkopo mdogo alinunua gari dogo kujishughulisha na kazi ya uchukuzi, na mama Ding alipata msaada wa fedha katika kuendeleza kilimo. Mume na mke walikuwa wanachapa kazi, katika muda wa miaka miwili tu, walipata pesa za kujenga nyumba moja ya ghorofa.
Mama Ding Xiufang aliona kuwa mtoto wa kike pia ana thamani kubwa. Akamkaribisha binti yake arudi nyumbani, zaidi ya hayo alimwandalia mtoto huyo chumba kizuri na kumtunza sana katika maisha na masomo yake.
Habari hizo kuhusu mama Ding Xiufang na binti yake zikaenea sana miongoni mwa wakulima katika wilaya ya Wuwei. Kutokana na sera ya serikali, katika wilaya hiyo familia zenye mtoto mmoja wa kike pekee au watoto wawili wa kike tu, zinaweza kupata msaada wa fedha Yuan elfu 30, sawa na dola za kimarekani karibu elfu 4 katika kipindi tangu kuzaliwa kwa mtoto wa kike mpaka anapofunga ndoa.
Kampeni ya kuwafuatilia watoto wa kike ni hatua iliyochukuliwa na serikali ili kuondoa hali ya kutokuwa na uwiano wa kijinsia. Hivi sasa tukitembelea vijiji vya China, tunakuta mabango, matangazo ya picha na vijitabu mbalimbali vinavyotoa elimu ya kuwapenda watoto wa kike na kutangaza sera nafuu mbalimbali zinazonufaisha familia zenye watoto wa kike pekee yao.
Pamoja na kuwaelimisha wakulima, idara za afya, polisi na sheria za China pia zinashirikiana katika kupambana na vitendo haramu vya kuthibitisha jinsia ya mtoto kabla ya kuzaliwa kwake na kutoa mimba, na kuwaadhibu watu waliojihusisha na vitendo hivyo.
Mkurugenzi wa Kamati ya uzazi wa mpango ya taifa ya China Bw. Zhang Weiqing hivi karibuni alisema, kampeni ya kuwafuatilia watoto wa kike imepata mafanikio makubwa katika wilaya kadhaa, kwa hiyo itatekelezwa kote nchini China. Hata hivyo ofisa huyo alisisitiza kuwa, bado kuna njia ndefu katika juhudi za kuondoa hali ya kutokuwepo kwa uwiano wa kijinsia, kwani kwa mujibu wa sensa ndogo iliyofanyika nchini China mwaka 2005, kwa watoto waliozaliwa, uwiano wa watoto wa kiume na wa kike ni 118.6 kwa 100.
Idhaa ya kiswahili 2006-07-27
|