Wachina huzingatia ujirani mwema, kuna methali ya Kichina inayosema "Majirani huweza kukusaidia kuliko jamaa walioko mbali". Lakini hivi sasa wakazi wa miji ya China ya zama tulizo nazo wameona kuwa, uhusiano wa karibu kati ya majirani unapotea siku hadi siku. Kutokana na hali hiyo, miaka 7 iliyopita siku ya majirani ilianzishwa na wakazi wa mtaa mmoja huko Tianjin, mji wa pwani ulioko kaskazini mwa China, kwa lengo la kuimarisha ujirani mwema. Sasa siku ya namna hii inafuatiliwa na wakazi wa miji kumi kadhaa ya China.
Neno "jirani" linawapa Wachina hisia nzuri mioyoni, kwani kutokana na desturi ya China, ujirani ni uhusiano wa karibu sana, kiasi ambacho unaweza kulingana na uhusiano kati ya jamaa.
Hapo awali wakazi wa miji ya China walikuwa wanaishi katika nyumba zisizo na ghorofa, ambapo familia kadhaa hata zaidi ya 10 ziliishi pamoja kwenye nyumba moja kubwa. Kwa wale wachache waliobahatika kukaa katika nyumba ya ghorofa, wakazi wa familia mbalimbali walitumia jiko na msala kwa pamoja. Kwa hiyo majirani walikuwa na uhusiano wa karibu, wakiwa kama jamaa ambao walitembeleana mara kwa mara.
Sambamba na maendeleo ya jamii ya China, wakazi wa miji walifuatana kuhamia kwenye nyumba za ghorofa, hali ya kutumia kwa pamoja jiko na msala kwa familia tofauti imepungua sana. Mbali na hayo, kasi ya mtindo wa maisha mijini na kuongezeka kwa mtazamo wa kulinda siri na familia, vimechangia kupungua kwa maingiliano kati ya majirani.
Mkazi wa Beijing Bw. Zhong Changzheng alisema"Baada ya kazi, nakwenda kwenye michezo ya kujenga mwili. Licha ya hayo, naongea na mke wangu, kutizama televisheni na kutembelea mtandao wa Internet. Maingiliano na majirani ni machache sana, au hata hakuna kabisa."
Huko Shanghai, mji mkubwa wa viwanda na biashara hapa nchini China, uchunguzi mmoja uliofanywa na serikali ya mji huo unaonesha kuwa, asilimia 24 tu ya familia zinawasiliana mara kwa mara na majirani, huku karibu nusu ya wakazi hawajui majina ya majirani na wala kazi zao.
Uchunguzi wa namna hiyo uliofanywa huko Shenzhen, mji wa kusini mwa China unaonesha kuwa, zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa mji huo wana nia ya kutambulishana na kuwasiliana na majirani, na kujenga ujirani mwema wa kusaidiana.
Wataalamu wanasema ujirani mwema una umuhimu mkubwa kwa afya ya mwili na kisaikolojia kwa kila mkazi, na kwa kudumisha utulivu wa jamii. Profesa Hao Maishou wa Taasisi ya sayansi ya jamii ya Tianjin alisema "Uhusiano mbaya kati ya majirani unaweza kuzuia upashanaji wa habari na mawasiliano ya kihisia, hata kuleta upweke na hisia za kukosa usalama. Aidha kutokana na kukosa mawasiliano na maingiliano, ni rahisi kutokea kwa makwaruzano na migongano isiyo lazima miongoni mwa majirani kwa sababu ya mambo madogomadogo."
Miaka 7 iliyopita ili kuhimiza ujirani mwema, siku ya majirani ilianzishwa katika mtaa wa Tianta, mjini Tianjin. Shughuli za siku hiyo za wiki moja zinafanyika katika majira ya mpukutiko ya kila mwaka. Katika siku hiyo, shughuli mbalimbali za kuwashirikisha wakazi wa mtaani zinazofanyika ni kama vile kucheza chesi, mashindano ya kuimba, kuwasaidia majirani wenye shida za kiuchumi n.k., vile vile kila mwaka wakazi waliodumisha ujirani mwema wanapewa tuzo. Imefahamika kuwa, katika miaka 7 iliyopita tangu ianzishwe siku ya majirani, katika mtaa huo wenye wakazi wapatao elfu 60, familia 700 zimepewa tuzo ya "majirani wema".
Mama Ma Shimin mwenye umri wa miaka 78 ni mkazi wa mtaa huo. Anapenda kuwasaidia majirani kwa kadiri anavyoweza, kwa mfano kuwasilisha ujumbe na kusafisha sehemu zinazotumiwa na watu wengi. Mama huyo akipata shida fulani, majirani pia wanajitolea kumsaidia. Mwaka 2004, mume wake mwenye umri wa miaka 80 aliugua, ambapo mama Ma Shimin alishukuru sana misaada kutoka kwa majirani. Alisema "Aliugua wakati watoto wetu hawapo, basi ningefanyaje? Majirani walijitolea, walishirikiana kumpelekea mume wangu hospitali. Katika hospitali, majirani walilipa gharama za matibabu na dawa. Bila majirani, labda mume wangu angekuwa amefariki. Hata mpaka hivi sasa kila nikikumbuka msaada wao nawashukuru sana."
Hivi sasa siku ya majirani imeenezwa katika miji mingine ya China. Kwa mfano wa mji maarufu wa utalii, Hangzhou siku ya majirani inafanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba kila mwaka. Wakati inaposherehekea siku hiyo, utepe wa rangi ya manjano ambao ni ishara ya baraka na masikilizano unapeperuka kote mjini, ambapo karibu mitaa yote inaandaa harakati mbalimbali, zikiwemo michezo ya majirani, na sherehe za dansi.
Katika siku ya majiraniyla mwaka jana, mtaa mmoja uliandaa tafrija iliyowashirikisha wakazi wote kwenye kiwanja cha mtaa huo, ambapo zaidi ya familia mia moja zilileta vyakula vyao. Akikumbusha siku hiyo mkazi mmoja Bibi Fan Fengdi alisema "Watu wote walifurahi sana. Tulikula kwa pamoja. Mtaa wetu ni kama familia kubwa. Harakati hiyo iliongeza maelewano na moyo wa kusaidiana kati ya majirani."
Ingawa shughuli za siku ya majirani zilifanyika kwa siku kadhaa tu, lakini urafiki uliooneshwa kwenye shughuli hizo unakumbukwa kila siku ya maisha ya majirani hao.
Idhaa ya kiswahili 2006-07-27
|