Jamhuri ya Kongo ilipata uhuru tarehe 15 mwezi Agosti mwaka 1960, tarehe 22 Februari mwaka 1964, China na Jamhuri ya Kongo zilianzisha uhusiano wa kibalozi. Jamhuri ya Kongo ni moja kati ya nchi za Afrika zilizoko kusini mwa Sahara zilizoanzisha mapema uhusiano wa kibalozi na China. Katika miaka zaidi ya 40 iliyopita, China na Jamhuri ya Kongo ziliungana mkono na kuelewana, na ushirikiano wa kunufaishana kati ya nchi hizo mbili unaimarika siku hadi siku.
Katika miaka ya 60 ya karne iliyopita, Jamhuri ya Kongo iliiunga mkono kithabiti Jamhuri ya Watu wa China irejeshewe kiti kwenye Umoja wa Mataifa, na siku zote inashikilia sera ya kuwepo kwa China moja. Mwaka 2005, wizara ya mambo ya nje ya Jamhuri ya Kongo ilitoa taarifa kuunga mkono kupitishwa kwa sheria ya China ya kupinga ufarakanishaji.
Baada ya kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Jamhuri ya Kongo, ushirikiano kati ya nchi hizo mbili uliimarishwa sana katika sekta za siasa, uchumi, elimu na afya. Katika sekta ya siasa, viongozi wa ngazi ya juu wa nchi hizo mbili wametembeleana mara kwa mara. Rais Denis Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Kongo amewahi kuitembelea China mara nyingi. Alisema China iliipatia Jamhuri ya Kongo msaada mkubwa bila ya masharti wakati ilipokumbwa na matatizo makubwa. Nchi hizo mbili zina maoni ya pamoja katika mambo mengi, na zinaungana mkono kwenye mambo ya kimataifa. Kwenye mkutano wa pili wa mawaziri wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Desemba mwaka 2003 huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, rais Sassou Nguesso akiwa mwenyekiti wa zamu wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika ya kati alipongeza uhusiano wa kirafiki kati ya China na nchi za Afrika.
Katika sekta ya biashara, ushirikiano wa kunufaishana kati ya nchi hizo mbili unaimarishwa mwaka hadi mwaka. Kuanzia mwaka 1965 hadi leo, miradi 41 kati ya 45 ambayo ni msaada kutoka serikali ya China nchini Jamhuri ya Kongo imekamilika. Miradi hiyo ni pamoja na kituo cha radio, hospitali, uwanja wa michezo na kituo cha kuzalisha umeme. Mwaka 2001, serikali ya China ilitangaza kusamehe sehemu kubwa ya madeni ya nchi hiyo yaliyokuwa yanadaiwa na China.
Baada ya kuingia katika karne mpya, biashara kati ya China na Jamhuri ya Kongo imeongezeka kwa haraka, mwaka 2005, thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili ilikuwa zaidi ya dola za kimarekani bilioni 2.4, ikiongezeka kwa asilimia zaidi ya 45 kuliko mwaka uliotangulia wakati kama huu.
Mawasiliano na ushirikiano kati ya China na Jamhuri ya Kongo katika sekta nyingi pia yanaimarika siku hadi siku. Chini ya mpango wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, mwaka 2004 hadi mwaka 2005, China ilitoa mafunzo kwa wataalamu 107 wa aina mbalimbali wa nchi hiyo. Kuanzia mwaka 1975, China kwa jumla ilitoa misaada ya masomo kwa wanafunzi 294 wa Jamhuri ya Kongo. Baada ya kumaliza masomo yao nchini China, baadhi ya waliokuwa wanafunzi hao wameanzisha somo la Kichina kwenye shule tatu za sekondari nchini humo, ili kuwafahamisha wakazi wa huko utamaduni wa China, ambao wamechangia sana kuzidisha urafiki na maelewano kati ya watu wa nchi hizo mbili.
Zaidi ya hayo, kuanzia mwaka 1966 hadi mwaka 2005, China kwa jumla imetuma vikundi 19 vya madaktari kufanya kazi nchini Jamhuri ya Kongo, na kuipa nchi hiyo misaada ya vifaa na dawa kila baada ya muda fulani. Pia imegharamia upanuzi wa hospitali ya Talangai ya Brazzaville, ambayo ilikuwa hospitali ndogo ya kina mama na watoto, kuwa hospitali kubwa inayoweza kutoa huduma za aina mbalimbali. Hivi sasa madaktari 23 wa China wanafanya kazi katika hospitali hiyo, madaktari hao wanachaguliwa kutoka hospitali 11 za Tianjin, wamebeba jukumu la kuwahudumia wagonjwa wa hospitali hiyo.
Tarehe 20 mwezi Juni mwaka huu, waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao aliyefanya ziara nchini Jamhuri ya Kongo, alitembelea hospitali ya Talangai wanakofanya kazi madaktari wa China. Mkuu wa hospitali ya Talangai alisema, madaktari wa China wamefanya kazi vizuri sana, wanasifiwa na wakazi wa huko kama "Madaktari wa Kongo". Alisema tiba ya vitobo ya kichina yaani tiba ya akyupancha kichina ina ufanisi mzuri, inafurahiwa sana na wagonjwa wa huko, kila mwaka idara ya akyupancha ya hospitali hiyo inawahudumia wagonjwa zaidi ya 5000.
Baada ya kutembelea hospitali ya Talangai, waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao alitembelea shule ya sekondari ya Brazzaville. Shule hiyo inajulikana sana nchini Jamhuri ya Kongo kutokana na masomo yake ya lugha ya kichina. Ziara ya waziri mkuu Wen Jiabao iliwafurahisha wanafunzi wa shule hiyo.
Shule ya sekondari ya Brazzaville ni shule kubwa zaidi kuliko shule nyingine nchini Jamhuri ya Kongo, shule hiyo ya sekondari ina wanafunzi zaidi ya 4000. Kuanzia mwaka 1990 walimu wa shule hiyo walianzisha somo la lugha ya kichina kwenye madarasa ya sekondari ya juu, hivi sasa wanafunzi 158 wanajifunza lugha ya kichina. Waziri mkuu Wen Jiabao akiambatana na walimu wa shule hiyo alifika kwenye darasa la kwanza la kidato cha tatu, ambapo katika ubao wa darasani aliona maneno yaliyoandikwa kwa lugha ya kichina: Sisi ni daraja la urafiki kati ya Jamhuri ya Kongo na China. Wanafunzi wote wa darasa hilo waliongea kwa kichina kuwakaribisha wageni kutoka China. Ingawa matamshi ya kichina ya wanafunzi hao bado siyo sanifu sana, lakini sura za watoto hao zimeonesha hisia za dhati. Baada ya kujifunza lugha ya kichina na utamaduni wa China, wanafunzi wameelewa kuwa, China ni nchi yenye historia ndefu na utamaduni unaong'ara. Wanatarajia sana kutembelea China siku moja.
Idhaa ya kiswahili 2006-07-28
|