Fasihi ya mambo ya kijeshi ni sehemu muhimu katika fasihi duniani. Ukatili wa vita, ushupavu wa askari, nidhamu kali za kijeshi na migongano ya kiutu, yote hayo huwa ni mada za maandishi ya fasihi ya kijeshi. Lakini mwandishi wa vitabu Chen Xiaodong hakuandika mada hiyo bali aliyoandika yote yanahusu chombo cha anga na wanasayansi wakubwa wa mambo ya kijeshi wa China.
Chen Xiaodong mwenye umri wa miaka 60 anasifiwa kuwa ni "mwenye kipaji cha ajabu katika jeshi" la China, licha ya kuwa hodari wa kuandika mashairi, maneno ya wimbo, tamthilia na riwaya, pia ni hodari wa kuandika taarifa za habari, lakini kati ya maandishi yake, yaliyo mengi zaidi ni taarifa kuhusu wanasayansi wa safari za anga ya juu.
Hivi sasa jambo analotamani zaidi ni tamthilia aliyoandika ya "Mwanasayansi mkubwa Qian Xuesen" itengenezwe kuwa filamu na kuoneshwa katika televisheni. Qian Xuesen amekuwa na umri wa miaka 95, ni mwanasayansi mkubwa wa elimu ya roketi ya anga na nguvu ya hewa, anasifiwa kuwa ni "baba wa safiri za anga ya juu nchini China" na "Mfme wa roketi". Tokea miaka zaidi ya 20 iliyopita mwandishi Chen Xiaodong alianza kukusanya habari zisizo za siri za mwanasayansi huyo, na aliandika mambo mengi yanayomhusu, na katika msingi wa maandishi hayo aliandika tamthilia ili ioneshwe katika televisheni. Bw. Chen Xiaodong alisema, "Mada ya tamthilia ni maelezo kuhusu Qian Xuesen. Nilimwandama karibu miaka 20 nikikusanya habari japokuwa kidogo, kwa ujumla niliandika makala sita juu yake na kila makala iliwavutia sana wasomaji, na kutokana na msingi huo nimeandika tamthilia ya kuoneshwa kwenye televisheni yenye sehemu 20 inaoitwa 'Mwanasayansi mkubwa Qian Xuesen'. Kazi ilikuwa ngumu lakini nimemaliza na sasa tamthilia hiyo iko mezani mwangu."
Bw. Chen Xiaodong alisema, watu wana hamu kubwa ya kufahamu Qian Xuesen alivyo, ingawa yeye mwenyewe amekataa kwa unyekekevu kuyafanya mambo yake kuwa tamthilia ya televisheni, lakini Chen Xiaodong akiwa mwandishi wa mambo ya kijeshi anaona ni jukumu lake kumwelezea jinsi alivyo na umuhimu mkubwa katika mambo ya anga nchini China.
Chen Xiaodong alijiunga na jeshi baada ya kuhitimu masomo ya sekondari, na tokea hapo kazi yake ilikuwa ni kuandika mambo yanayohusu wanajeshi. Katika miaka iliyopita aliwahi kuchapisha vitabu vingi ambavyo baadhi yao vinaeleza mafanikio ya sayansi na teknolojia ya safiri ya anga ya juu nchini China na vingine vinaeleza historia ya jeshi la China, na katika miongo kadhaa iliyopita alipata tuzo nyingi za kitaifa. Chen Xiaodong anaona kazi hiyo inamfaa sana. Alisema, "Kabla ya kujiunga na jeshi, nilikuwa najitokeza katika michezo ya sanaa shuleni, niliwahi kupiga fidla na filimbi. Muda mfupi baada ya kujiunga na jeshi nilihamishwa kwenye makao makuu ya divisheni, nikawa mwandishi wa mambo jeshini."
Mwaka 1984 Chen Xiaodong alijiunga na Chuo Kikuu cha Sanaa cha Wanajeshi kuendelea zaidi na masomo. Alipokuwa chuoni alisoma vitabu vingi vya zama hizi na za kale, vya nchini China na vya nchi za nje, na kati ya vitabu hivyo, vitabu vinavyoeleza vita kuu ya pili ya dunia vilimvutia zaidi. Kwa kuwa mwandishi wa mambo ya kijeshi, suala alilofikiri zaidi ni fasihi ya kijeshi ya hivi sasa. Anaona kwamba wakati wa amani, mambo yanayoonesha ushupavu wa kijeshi ni nia ya kuinua kiwango cha sayansi na teknolojia kwa ajili ya ulinzi wa taifa. Taarifa yake ndefu "Mtu anayemfuatilia Albert Einstein" imeonesha wazo lake hilo, taarifa hiyo imeeleza hadithi ya mtaalamu mmoja aliyejitolea mhanga katika utafiti wa makombora ya masafa marefu. Taarifa hiyo ilisifiwa na mwandishi mkubwa Liu Baiyu. Bw. Chen Xiaodong alisema ingawa yeye si mtu anayeongoza katika uandishi wa fasihi ya kijeshi lakini mafanikio yake yamempa faraja. Alisema, "Katika fasihi ya kijeshi, naandika zaidi wanasayansi wa mambo ya kijeshi yaani watu wanaoshughulikia sayansi na teknolojia ya ulinzi wa taifa, kitabu changu kinachoitwa 'Mtu anayemfuatilia Albert Einstein' kinavutia, na mwandishi Liu Baiyu aliposoma taarifa hiyo alitokwa machozi mara kadhaa."
Chen Xiaodong ni mmoja kati ya waandishi wachache wanaoruhusiwa kukusanya habari kuhusu mambo ya safiri ya anga ya juu nchini China. Katika muda wa miaka kumi iliyopita, alitembelea karibu idara zote husika toka viongozi hadi askari wa kawaida ili apate habari nyingi, aliyoandika kuhusu mambo ya usafiri angani yamefikia maneno milioni kadhaa.
Katika taarifa yake ya "Ndoto ya kurukia angani" alieleza mambo mengi ambayo watu walikuwa hawafahamu, aliyoyaandika ni kama ufupisho wa historia ya juhudi za wanasayansi wa safiri ya anga ya juu nchini China na imeeleza uhusiano kati ya ulimwengu, dunia na binadamu. Lakini Chen Xiaodong hakuridhika na mafanikio yake, alisema ataandika mengi zaidi. Alisema, "Nalipenda sana jeshi langu na hasa askari wetu wasiogopa shida na kupambana nayo kimya kimya. Maandishi niliyoandika katika miongo kadhaa iliyopita karibu yote yanasifu moyo wao wa kishupavu ambao pia ni moyo wa taifa letu."
Bw. Chen Xiaodong alisema, watu wengi wanaona kwamba mambo ya safiri ya anga ya juu ni mambo ya ajabu, na watu wanaoshughulikia mambo hayo hakika sio watu wa kawaida, lakini kwa kweli katika nyanja hiyo wengi ni watu wa kawaida, na kila mmoja anatoa mchango wake usiku na mchana. Alisema anawajibika kuwasifu kwa kalamu yake katika maisha yake yote.
Idhaa ya kiswahili 2006-07-31
|