"Huaer" ni aina ya nyimbo za kienyeji, ambazo zinaimbwa sana na watu wa kabila la Wahui wanaoishi katika sehemu ya kaskazini magharibi ya China. Nyimbo hizo hujulikana kwa sauti kubwa ya kuvuma na maneno rahisi ya nyimbo, zina umaalumu wa kikabila na kikanda. Katika miaka ya hivi karibuni, mwimbaji wa kabila la Wahui Bw. Su Erdong ametoa mchango mkubwa katika kueneza nyimbo hizo. Hivi sasa nyimbo za "Huaer" zinasikika mara kwa mara kwenye harusi na dhifa za kabila la Wahui.
Su Erdong ni mwalimu, anaishi katika mkoa unaojiendesha wa kabila la Wauyghur wa Xinjiang, kaskazini magharibi mwa China. Mbali na kazi ya ualimu, pia anapenda kutunga na kuimba nyimbo. Katika miaka 10 iliyopita, alitoa albamu tano zenye nyimbo zaidi ya 120.
Su Erdong alivutiwa na kuimba nyimbo tangu utotoni mwake. Baada ya kuhitimu kutoka kwenye chuo kikuu, alianza kutunga nyimbo, ambapo nyimbo zake zilikuwa za mitindo ya kabila la Wakhazak na kabila la Wauyghur. Akaanza kujishughulisha na utungaji wa nyimbo za "Huaer" za kabila la Wahui baada ya kukutana na marafiki zake. Kijana huyo alikumbusha akisema "Rafiki yangu mmoja aliniuliza kwa utani, 'unaimba vizuri sana nyimbo za Kikhazak na Kiuyghur, je, unaweza kuimba wimbo wa Kihui?' Huku mwingine aliongeza kuwa, 'Sijawahi kusikia wimbo wa kabila la Wahui.' Nilikasirishwa na maneno hayo, nikawaambia, 'Nani alisema kabila la Wahui halina nyimbo zao? Huaer ndizo nyimbo zetu.' Rafiki yangu alinijibu akisema, 'Ninyi hamna nyimbo za kisasa, Huaer ni nyimbo za jadi, hatuzifahamu wala hatuzipendi.'"
Ingawa alikuwa akipinga sana kauli zao, lakini baadaye Su Erdong akagundua maneno ya marafiki zake yalikuwa na ukweli fulani. Huaer ni nyimbo pekee za kabila la Wahui zinazofahamika kwa watu wengi, lakini uimbaji wake ni rahisi wa kutumia aina chache za ala na maneno ya kanda ya kaskazini magharibi ya China. Kwa hiyo idadi ya watu wa kabila la Wahui wanaoimba nyimbo za "Huaer" na wanaozifahamu inapungua siku hadi siku.
Bw. Su Erdong alifikiria kuzifanyia marekebisho nyimbo za "Huaer". Alisema "Muziki wa makabila mengine umepata maendeleo kutokana na kujifunza kutoka kwa muziki wa kimagharibi na tamaduni nyingine, halafu ukapata sura mpya. Kwa maoni yangu, kabila la Wahui linastahili kuwa na nyimbo zake za kisasa, ambazo zinaonesha utamaduni na tabia nzuri za kabila hilo."
Kijana huyo alianza kutafiti utamaduni na historia ya kabila la Wahui. Aligundua kuwa, baadhi ya watu mashuhuri katika historia ya China walitoka kabila hilo. Kwa hiyo alitunga wimbo uitwao "Wahui" akilenga kueneza sifa za watu hao.
Rafiki yake Bw. Bao Yucheng alisema anapenda sana wimbo huo. "Kwenye wimbo huo, Su Erdong anaimba vitu wanavyopenda Wahui na vitu wanavyotaka kuvifahamu. Nakubaliana naye sana. Kwa kupitia nyimbo zake, napata ufahamu mwingi kuhusu utamaduni wa kabila la Wahui."
Su Erdong anapenda muziki, lakini mwanzoni alipoanza kujishughulisha na fani hiyo alikabiliwa na matatizo mengi. aligharamia mwenyewe kutoa albamu yake ya kwanza, ambapo kutokana na kukosa pesa, aliwashirikisha mke na mwanaye wakifunga kaseti kwa pamoja.
Alipoanza kutoa albamu yake, alikuwa hana pesa za kufanya matangazo ya kibiashara, hali ambayo iliathiri mauzo ya albamu. Kutokana na hali hiyo, Su Erdong mwenyewe alifanya matangazo, popote akienda aliimba nyimbo zake, kama vile katika kiwanja cha michezo cha shule ya msingi, katika kiwanja cha mapumziko cha wakazi wa mji na mashambani. Hatua kwa hatua nyimbo zake zilitambuliwa na wengine. Rafiki yake Bw. Bao Yucheng alimwambia mwandishi wetu wa habari, akisema "Nilifuatana naye kwenda vijijini, ambapo moyo wangu uliguswa sana na jinsi wakulima walivyopenda nyimbo zake. Tuliwahi kwenda kwenye shule za kabila la Wahui, ambapo wanafunzi walikuwa wakizunguka gari lake wakiomba sahihi yake. Wanafunzi wengi walitokwa na machozi. Hivi sasa ana mashabiki wengi, mbali na watu wa kabila la Wahui, bali pia makabila mengine ya mkoani Xinjiang, kama vile Wauyghur na Wakhazak."
Bw. Ma Zheli ni wa kabila la Wahui anayekaa mjini Beijing. Alieleza kuwa, mbali na yeye mwenyewe kupenda nyimbo za Su Erdong, mwanaye mwenye umri wa miaka 16 pia ni shabiki wa mwimbaji huyo, kwani nyimbo hizo si kama tu zinaburudisha, bali pia zinatoa elimu. Alisema, "Nyimbo zake kadhaa zinaeleza historia za kabila la Wahui, baadhi yao zinatoa mafunzo ya kuwaheshimu wazee, kujipa matumaini ya maisha, kuwapenda wengine na kuhifadhi mazingira. Kwa hiyo namshauri mwanangu asikilize nyimbo zake mara kwa mara."
Wataalamu kadhaa wa muziki wanasema kuwa, nyimbo za Su Erdong zinajifunza kutoka kwa muziki wa nyimbo za "Huaer" na nyimbo za makabila mengine, zikichanganywa na mtindo wa muziki za kisasa, kwa hiyo nyimbo hizo zina sifa ya kisasa na zina uhusiano wa karibu na maisha ya watu.
Idhaa ya kiswahili 2006-08-03
|