Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-07 15:04:06    
Kundi la kwanza la vitabu vya kale vilivyogunduliwa katika mapango ya Dunhuang nchini China vyachapishwa upya

cri

Kundi la kwanza la vitabu 30 kati ya vitabu vya kale vilivyogunduliwa katika mapango ya Dunhuang nchini China na kuhifadhiwa katika maktaba ya taifa ya China vimechapishwa kwa kupigwa picha. Kuchapishwa kwa vitabu hivyo ili wasomaji waweze kusoma badala ya kuvihifadhi kumeonesha maendeleo makubwa ya teknolojia yaliyopatikana katika juhudi za kurejesha hali ya awali ya vitabu vya kale.

Mwaka 1900, ndani ya mapango ya Dunhuang mkoani Gansu kaskazini magharibi mwa China, viligunduliwa vitabu vingi vya kale vilivyoandikwa kati ya karne ya tano hadi ya 11. Vitabu hivyo viliandikwa hali ya dini, unajimu na jiografia, historia, mila na desturi na utamaduni kwa kugha za Kichina (lugha ya kabila la Wahan), Kitibet na Sanskrit, ambavyo ni msaada mkubwa katika utafiti wa hali ya jamii ya kale ya Asia ya kusini mashariki. Lakini baada ya habari za kugunduliwa kwa vitabu hivyo kuenea, katika muda wa miaka 20 hivi vitabu hivyo vingi vilichukuliwa na nchi za nje katika vurugu za vita, hivi sasa nchi zaidi ya 40 zina baadhi ya vitabu hivyo, kati ya nchi hizo, Uingereza, Ufaransa, Russia na Japan zinamiliki vitabu vingi zaidi.

Maktaba ya taifa ya China mjini Beijing ni makavazi kubwa ambayo imehifadhi vitabu hivyo 16,000, yaani theluthi ya jumla ya vitabu vya mapango ya Dunhuang. Kutokana na miaka mingi kupita, vitabu vimechakaa na kuharibika vibaya. Tokea miaka ya 80 ya karne iliyopita maktaba hiyo ilianza kukarabati vitabu hivyo. Hivi sasa kazi ya kukarabati imepata mafanikio makubwa, maktaba ya taifa imeamua kuchapisha vitabu hivyo katika juzuu 150 kwa kupiga picha. Kwa makadirio uchapishaji wa vitabu hivyo utakamilika kabla mwishoni mwa mwaka 2007. Naibu mkutubi mkuu wa maktaba hiyo Bw. Chen Li alisema, kuchapisha vitabu hivyo ni tumaini kubwa la miaka mingi la wataalamu wa nchini China na wa nchi za nje. Alisema, "Urithi wa utamaduni ukihifadhiwa tu bila kuweza kuenziwa na kuuoneshwa hadharani hauna maana. Katika miaka kadhaa iliyopita tulifanya juhudi za kuinua teknolojia ili kuzifanya nyaraka za kale ndani ya maktaba ziweze kusomwa na wataalamu na huku zinahifadhiwa kwa uhakika."

Bw. Chen Li alieleza, maktaba ya taifa ya China ilianzisha idara maalumu ya kuhifadhi vitabu vilivyopatikana katika mapango ya Dunhuang katika miaka ya 30 ya karne iliyopita na kuanzia miaka ya 80 ilianza mandalizi ya kuchapisha vitabu hivyo.

Mkurugenzi wa idara maalumu ya kuhifadhi vitabu hivyo Bw. Zhang Zhiqing, ambaye pia ni mtaalamu mkubwa wa hifadhi ya nyaraka za kale alieleza kuwa, kazi za kukarabati vitabu vya mapango ya Dunhuang ni nyingi na zinafanyika kwa utaratibu, ni ufundi wa jadi wa China, kifurushi kidogo cha karatasi kikirudishwa katika inayofanana na hali yake ya awali pengine kitahitaji kazi ya fundi mmoja kwa miezi kadhaa. Ufundi tunaotumia ni tofauti na wa nchi za nje, na sifa ya ufundi huo ni kuweza kufuta kwa urahisi alama iliyokarabatiwa na kukarabati upya kama ufundi mzuri zaidi ukipatikana baadaye. Ufundi wetu tunaotumia unasifiwa na nchi za nje, maktaba nyingi za nchi za nje zilituma watu kuja kujifunza ufundi wetu. Vitabu 30 vilivyochapishwa hivi karibuni vinasomeka vizuri sana. Bw. Zhang Zhiqing alisema, "Jukumu letu ni kuvifanya vitabu hivyo vya kale viwe safi baada ya kuchapwa. Kutokana na vitabu hivyo kuwepo kwa miaka mingi, vitabu vingi vimeharibika na karatasi zimekuwa na madoa madoa na kubadilika kuwa njano, kazi ya kuonesha maneno vizuri ni ngumu sana, lakini kwa kufanya juhudi nyingi tumefanikiwa kuhakikisha vitabu vinavyochapishwa vinakuwa safi."

Bw. Zhang alieleza kwamba karatasi zilizotumika katika kuchapisha vitabu hivyo ni nyepesi ili kurahisisha kupekua. Hii inaonesha kwamba kiwango cha uchapaji wa vitabu hivyo ni cha juu. Hata hivyo hatumaanishi kwamba kazi ya kuhifadhi vitabu vya kale nchini China tayari imeridhisha. Mwanasayansi wa kuhifadhi vitabu vya kale katika maktaba ya taifa ya China Bw. Lin Shitian alisema, katika mambo ya kuhifadhi vitabu vya kale China inahitaji kujifunza mambo mengi kutoka nchi za nje. Bw. Lin alisema, "Kwa ushirikiano na nchi za nje tunaweza kupata uzoefu mkubwa kutoka nchi za nje, lakini naona kitu muhimu zaidi tunachotaka kujifunza kutoka kwa wenzetu wa nchi za nje ni namna ya kutilia mkazo zaidi kazi ya kuhifadhi vitabu vya kale. Kwa mfano katika nchi za nje mafundi wa ukarabati wanapewa mafunzo kila baada ya muda na wote ni watu wenye elimu ya miaka mingi."

Bw. Lin alieleza kwamba hapo kabla, ufundi wa ukarabati wa nyaraka za kale ulifundishwa kwa midomo tu na kurithishwa kizazi kwa kizazi. Mwaka 2003 maktaba ya taifa ya China ilianzisha faili la kurekodi hali ya kila kitabu kabla na baada ya kukarabatiwa ili watu wa baadaye waweze kufahamu.

Kuchapishwa kwa vitabu vya mapango ya Dunhuang kumewawezesha watafiti wa elimu ya urithi wa mapango ya Dunhuang kuvisoma. Na hii ni sehemu moja tu ya kazi za kuhifadhi vitabu vya mapango ya Dunhuang. Prof. Hao Chunwen wa idara ya historia katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Mji Mkuu wa Beijing alisema, katika miaka ya karibuni, wataalamu wa taaluma ya elimu ya mapango ya Dunhuang wameanza kushiriki katika utafiti wa kimataifa kuhusu elimu ya mapango ya Dunhuang. Utafiti wa elimu ya mapango ya Dunhuang hakika utapata maendeleo makubwa zaidi katika siku za usoni." Aliongeza kusema, "Sayansi kwenye mapango ya Dunhuang ni elimu ya kimataifa toka mwanzo. Elimu yake ni ya pande mbalimbali, na kila mtafiti ana mkazo wake wa utafiti wa elimu fulani, na mafanikio ya kila mmoja yakikusanywa pamoja ujuzi wetu utakuwa mkubwa zaidi. Hivi sasa elimu ni ya watu wote duniani, halikadhalika, elimu ya Dunhuang. Kwa sababu vitu vya mapango ya Dunhuang ni urithi kutoka kwa wahenga wa China, kwa hiyo ni lazima sisi Wachina tufanye utafiti wa kina zaidi."

Prof. Hao alisema, watafiti wa China wana sifa zao, na watafiti wa nchi za nje pia wana sifa zao wenyewe, anatumai watafiti wa nchi za nje watashiriki kwenye utafiti wa China kwa kusaidiana na kufundishana ili kuimarisha utafiti na hifadhi ya vitabu vya mapango ya Dunhuang.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-07