Tetemeko kubwa la ardhi lililoukumba mji wa Tangshan miaka 30 iliyopita, ni tukio ambalo Wachina hawataweza kulisahau. Maafa hayo yalisababisha vifo vya watu laki 2 na elfu 40, na kuwafanya watoto zaidi ya elfu 4 wapoteze wazazi wao. Hivi sasa miaka 30 imepita, je, watoto hao yatima wanaendelea vipi? Mwandishi wetu wa habari aliwatembelea watoto yatima kadhaa.
Bibi huyo anayeongea kwa simu anaitwa Xu Weiwei. Yeye ni mrefu na mwenye sura ya tabasamu, hali ambayo inafanya nie vigumu kutambua kama aliwahi kukumbwa na uchungu mkubwa utotoni mwake. Maswali ya mwandishi wetu wa habari yaliamsha kumbukumbu zake, alisema "Hakika siwezi kusahau, sitasahau katika maisha yangu."
Alfajiri ya tarehe 28 Julai mwaka 1976, saa 9 na dakika 42 kwa saa za China, tetemeko kubwa la radhi lenye nguvu ya 7.8 kwenye kipimo cha Richter liliukumba mji wa Tangshan, ghafla mji huo muhimu wa viwanda katika sehemu ya kaskazini ya China ulibomolewa kabisa, ambapo watu laki 2 na elfu 40 walikufa, wakiwemo wazazi wa Xu Weiwei na dada yake mkubwa.
Xu Weiwei alikuwa na familia nzuri. Baba yake alikuwa anafanya kazi kwenye kiwanda cha chuma cha pua cha Tangshan na alikuwa analipwa mshahara mzuri, mama yake alipata ajira katika kiwanda cha kutengeneza kofia. Familia hiyo ilikuwa na mabinti watatu, na Xu Weiwei alikuwa binti mdogo.
Mwanamke huyo akikumbusha siku za utotoni mwake, alieleza kuwa kuna wakati alikuwa na tabia mbaya, akipata hasira alijifungia chumbani na kukataa kula mpaka wazazi wake waliokuwa nje walipomshawishi kwa muda mrefu. Alisema karibu na nyumba yao kulikuwa na duka moja kubwa, na katika siku za mapumziko baba yake alikuwa akimbeba mgongoni mwake huku mama akiwaongoza dada zake wawili, kutembelea duka hilo mara kwa mara.
Kuhusu usiku huo lilipotokea tetemeko la ardhi, Bibi Xu Weiwei akikumbusha alisema, hali ya hewa ilikuwa ni joto ajabu. Ili kukwepa joto dada yake mkubwa alikuwa kiwanjani akicheza mpira wa vinyoya na wanafunzi wenzie mpaka saa 7 usiku, aliporudi nyumbani kulala. Watoto hao watatu walikaa kwenye chumba kimoja, ambapo dada mkubwa alilala kwenye kitanda kidogo na Xu Weiwei na dada mwingine walitumia kitanda kingine kikubwa. Dada mkubwa aliporudi alikuta Xu Weiwei aliyekuwa amelala fofofo ameanguka sakafuni, kwa hiyo alimlaza kwenye kitanda kidogo. Hatua hiyo ilimfanya anusurike kwenye tetemeko la ardhi.
Bibi Xu Weiwei alikumbusha na kusema "Ghafla mwanga mkali ulitokea angani, nilimwuliza dada kwa nini mwanga umetokea? Akanijibu hajui. Halafu nilisikia mlio mkubwa kama radi. Tulipogundua tetemeko la ardhi limetokea, ukuta ulioko karibu nasi ulikuwa umeanza kupasuka, na nyumba ikaanza kuyumbayumba. Wakati huo nilirushwa nje pamoja na blanketi niliyokuwa nimejifunika kutoka sehemu ya ukuta iliyovunjika, nikaanguka ardhini kutoka ghorofa ya kwanza."
Xu Weiwei alisimama, aliona nusu ya jengo la ghorofa tatu alikokaa limebomoka, na kubakia kifusi, ambapo dada yake mkubwa alikuwa akitafuta ndani ya magofu, alipomwambia Xu Weiwei alilia akamwambia kuwa, baba, mama na dada yao mwingine walikuwa bado ndani.
Xu Weiwei alikumbusha na kusema "Tulikuwa tukiwatafuta, ambapo mawe yaliyokuwa yakiendelea kuanguka kutoka ghorofa yakitupiga, lakini hatukutambua hatari wala hofu, tukiwa na lengo moja tu la kuwapata wazazi wetu. Kukawa kimya bila ya sauti yoyote, wakati huo huo niliona dunia hii hakuna wengine isipokuwa sisi wawili tukilia."
Wakati huo huo kwenye kifusi kilikuwepo kwenye barabara kadhaa mbali na nyumba ya Xu Weiwei, mtoto mmoja mchanga wa miezi 6 aitwaye Dang Yuxing aliamshwa na tetemeko la ardhi, akalia kwa sauti kubwa. Huku Zhang Lizhi aliyekuwa na umri wa miaka mitano alikuwa akitambaa nje ya magofu ya nyumba yaliyopo katikati ya mji wa Tangshan. Mguu wake wa kulia ulijeruhiwa, mtoto huyo aliumia sana akalia kwa sauti kubwa, huku akiangalia kwa hofu nyumba zilizobomoka.
Bibi Zhang Lizhi akikumbusha tukio hilo alisema, "Nyumba yetu ilikuwa katika sehemu ya katikati ya mji, ambapo idadi kubwa ya watu walikufa kwenye tetemeko la ardhi. Familia ya shangazi yangu na familia yangu zilikuwa zinakaa pamoja. Nilitambaa nje ya magofu ya nyumba yetu, nikagundua kuwa watu wengine kwenye familia yangu wamekufa. Nilipoteza baba, mama, dada, bibi, baba mdogo na shangazi kwa wakati mmoja."
Watoto hao waliokolewa na wanajeshi waliotumwa huko baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi. Siku kadhaa baadaye waliaga miili ya jamaa zao.
Katika maafa hayo makubwa ya ajabu, watoto zaidi ya elfu 4 walifiwa na wazazi na kuwa yatima.
Watoto hao yatima walipewa msaada kwa haraka. Baadhi yao walipokelewa na jamaa waliokuja baada ya kupata habari kuhusu tetemeko la ardhi, kwa mfano Bibi Xu Weiwei na dada yake mkubwa walichukuliwa na bibi yao. Watoto wengine kama Dang Yuxin na Zhang Lizhi walipelekwa katika shule iitwayo Yuhong ambayo ilijengwa kwa ajili ya watoto yatima wa mji wa Tangshan, ambapo si kama tu walilelewa na kupewa elimu bure, bali pia walisaidiwa vizuri katika maisha na kupewa ajira.
Miaka 30 imeshapita, watoto hao yatima sasa ni wazima. Je wanaendeleza vipi maisha yao? Tutawaletea maelezo zaidi wiki ijayo.
Idhaa ya kiswahili 2006-08-10
|